Mazishi ya Jenista yaibua kero ya barabara Mbinga

Mbinga/Dar.  Wakati aliyekuwa mbunge wa Peramiho (CCM), Jenista Mhagama akihitimisha safari yake ya mwisho duniani kwa kuzikwa, kero ya barabara imeibuliwa kwenye maziko yake na kutafutiwa ufumbuzi.

Jenista aliyefariki dunia Alhamisi, Desemba 11, 2025 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma, kwa ugonjwa wa moyo, amezikwa leo Jumanne, Desemba 16, 2025 katika Makaburi ya Senta B yaliyopo Kijiji cha Ruanda, Wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma.

Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi ameongoza waombolezaji kwenye safari hiyo ya mwisho ya Jenista aliyekuwa mbunge wa Perahimo kuanzia mwaka 2005 hadi kifo kilipomkuta.

Wakati wa maziko hayo, Serikali iliagizwa kuchukua hatua za haraka kuhakikisha ujenzi wa barabara eneo la Kitai-Ruanda–Lituhi unakamilika kwa wakati, kufuatia malalamiko ya wananchi na viongozi wa dini kuhusu ucheleweshwaji wa mradi huo wenye umuhimu mkubwa kiuchumi.

Akizungumza katika tukio hilo, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amesema amepokea hoja ya barabara hiyo na kusisitiza miradi inayowasumbua wananchi inapaswa kupewa kipaumbele.

Amesema ameshuhudia hali ya ujenzi kuanzia Kitai hadi Ruanda, Ruanda hadi Lihuti na Kitai hadi Lutuhi, na kubaini kuwa kasi ya utekelezaji hairidhishi.

Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas amuite mkandarasi husika na kumtaka awajibike, akisisitiza kuwa mkandarasi huyo tayari alipokea fedha za Wizara ya Ujenzi.

“Kwa utaratibu wa Serikali, mkandarasi anatakiwa amalize kazi kwa fedha alizopokea kabla ya kuomba nyingine. Tabia ya kupokea fedha na kuzipeleka kwenye miradi mingine haikubaliki,” amesema.

Amesema endapo mkandarasi atashindwa kutekeleza majukumu yake, hatua kali zichukuliwe ikiwamo kuzuiwa kusafiri kwa kushikilia pasi yake ya kusafiria hadi kazi ikamilike.

Waziri Mkuu pia ameagiza Wizara ya Ujenzi kukamilisha haraka taratibu za ununuzi kwa Barabara ya Ruanda–Lituhi, akisema eneo hilo lina fursa kubwa ya kuchochea uchumi na kuongeza mapato ya Taifa.

Pia, amesisitiza kuwa atakapofanya ziara nyingine, anatarajia kuona mabadiliko ya wazi kwenye utekelezaji wa mradi huo.

Wakati huohuo, Dk Nchimbi ameipongeza kauli na msimamo wa Waziri Mkuu, akisema ndivyo anavyopaswa kuwa kiongozi mkuu wa Serikali.

 Amesema amefurahishwa na hatua hizo na kusisitiza kuwa, uongozi ni utumishi kwa wananchi, siyo unyanyasaji.

Makamu wa Rais pia ametumia fursa hiyo kutoa heshima kwa marehemu Jenista Mhagama, akimtaja kuwa mtumishi wa kweli wa umma na mtu aliyetoa mchango mkubwa kwa Taifa na Chama cha Mapinduzi.

“Jenista aliwahi kuwa mbunge kwa takribani miaka 20 na waziri kwa zaidi ya miaka 10, akitumikia kwa kujituma na uadilifu mkubwa. Serikali na chama tumepoteza mtu muhimu sana, lakini tutaendelea kuenzi mchango wake,” amesema.

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mussa Zungu amesema hoja ya barabara, hata kama haikutajwa moja kwa moja, imesikika na imechukuliwa kwa uzito unaostahili.

Mwili wa aliyekua Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama ukishushwa kaburini leo Jumanne Desemba 16, 2025 katika kijiji cha Ruanda wilayani Mbinga, Ruvuma. Picha na Joyce Joliga

“Eneo hili ni kitovu cha mali na biashara, ucheleweshaji wa miundombinu unaathiri moja kwa moja uchumi,”  amesema.

Hata hivyo, spika ameahidi kuwakutanisha viongozi wa eneo hilo, wakiwamo wabunge, viongozi wa dini na waziri husika ili kujenga hoja ya pamoja itakayoharakisha utekelezaji wa mradi.

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga, John Ndimbo amesema licha ya majonzi ya kumpoteza Jenista, kiimani bado yupo hai kwa kuwa ameweza kuwakusanya na kuwaunganisha viongozi wakuu wa nchi.

“Jenista pamoja na kwamba amelala, ila yupo hai amewaleta viongozi mbalimbali wakuu na wabunge wenziye ili waweze kuona changamoto ambazo wananchi wake wanapitia licha ya utajiri mkubwa wa makaa ya mawe waliojaaliwa kwenye eneo lao, hivyo naimani changamoto hizo zitafanyiwa kazi na viongozi wetu,” amesema Askofu Ndimbo.

Naibu Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Chesco Msaga, amesema Jenista atakumbukwa kwa imani yake, unyenyekevu na kuwa kiungo muhimu kati ya Serikali na madhehebu ya dini.

Pia, amesema msiba huo ni wa Taifa zima, si familia pekee.

 Waziri wa Viwanda na Biashara na Mbunge wa Mbinga Vijijini, Judith Kapinga amesema maisha ya Jenista yalijaa uongozi wa kweli ambao haukupimwa kwa madaraka bali kwa wema ambao ameuacha katika mioyo ya watu.

Licha ya umbali mrefu na ubovu wa barabara kutoka Viwanja vya Nane Nane hadi Ruanda wilayani Mbinga, maelfu ya waombolezaji kutoka mikoa mbalimbali nchini hawakuzuiwa kusafiri zaidi ya kilomita 120 kwenda kumpumzisha Jenista katika nyumba yake ya milele.

Tangu saa 11 alfajiri ya Desemba 16, 2025, msururu wa magari ya viongozi wa Serikali, vyama vya siasa, madhehebu ya dini, mashirika mbalimbali pamoja na wananchi wa kawaida ulionekana ukielekea Ruanda kuhudhuria mazishi hayo.

Mkazi wa Njombe, Batazar Andondile amesema wingi wa waombolezaji unaonesha namna marehemu alivyoishi kwa kuwapenda na kuwahudumia Watanzania. Amesema licha ya changamoto ya barabara, wananchi hawakukata tamaa.

Charles Luambano wa Songea Vijijini amesema Jenister aligusa maisha ya wananchi maskini kwa kuwapatia mifugo na pembejeo, hatua iliyowaondolea umaskini na kuwapa matumaini mapya.