Dar es Salaam. Mchakato wa upangaji wa majaji watakaosikiliza kesi za kupinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, katika majimbo manane Zanzibar, sasa unatarajiwa kuanza Desemba 23, 2025 baada ya kukamilika kwa taratibu za ubadilishanaji nyaraka za kesi hizo.
Majimbo hayo ambayo matokeo ya uchaguzi wake yanapingwa ni Kiwani, ambako Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla alitangazwa mshindi, Mkoani, Chakechake, Chonga, Wawi, Kojani, Konde na Micheweni.
Kesi hizo zimefunguliwa na waliokuwa wagombea wa nafasi za uwakilishi katika majimbo hayo kupitia Chama cha ACT-Wazalendo dhidi ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Leo Jumanne, Desemba 16, 2025, kesi hizo zimetajwa mbele Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Zanzibar, Kanda ya Pemba, Chausiku Kuya kwa ajili ya kupokea majibu ya wadaiwa
Kiongozi wa jopo la mawakili wa wadai ambaye pia ni mwanasheria mkuu wa chama hicho, Wakili Omar Said Shaaban, ameieleza Mahakama kuwa tayari wameshapokea majibu ya wadaiwa katika kesi hizo.
Hivyo, wakili Shaaban ameiomba Mahakama wadai wapewe siku saba kupitia hoja za wadaiwa katika majibu yao hayo, kabla ya kuwasilisha majibu yao za ziada dhidi ya majibu hayo ya wadaiwa.
Kiongozi wa jopo la mawakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa niaba ya wadaiwa, Mbarouk Suleiman Othman amesema kuwa hawana pingamizi kwa ombi hilo la wadai kupewa muda huo waliouomba kuwasilisha majibu yao ya ziada.
Naibu Msajili amekubaliana na ombi hilo na kuwapa siku saba wadai kama walivyoomba kuwasilisha majibu yao dhidi ya majibu ya wadaiwa, ambazo zinaishia Desemba 23, 2025.
Hivyo kesi hizo zimeahirishwa mpaka tarehe hiyo zitakapotajwa kuangalia kama taratibu hizo za ubadilishanaji nyaraka zitakuwa zimemilika kwa ajili ya hatua nyingine zinazofuata.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, Shaaban, amesema kuwa tarehe hiyo baada ya taratibu hizo za ubadilishanaji nyaraka kukamilika, Naibu Msajili atawasilisha majalada yote ya kesi hizo kwa Jaji Mkuu kwa ajili ya kupanga majaji watakaosikiliza.
“Tumeridhika na hatua hiyo ya Mahakama na sasa tunajipanga kikamilifu kwa hatua zinazofuata za mashauri hayo. Sisi kama mawakili tunahakikisha kuwa kila kitu kitafanyika kwa mujibu wa sheria na taratibu zote za kisheria zitazingatiwa,” amesema Shaaban.
