Sowah, Kante wafungiwa mechi tano, Yanga yatozwa faini Sh5 milioni

MSHAMBULIAJI wa Simba, Jonathan Sowah na kiungo wa timu hiyo, Allasane Kante, wamefungiwa kucheza mechi tano kila mmoja kutokana na makosa ya utovu wa nidhamu waliyofanya dhidi ya Azam FC, Desemba 7, mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) leo Desemba 16, 2025, imeeleza kuwa Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa bodi hiyo katika kikao chake cha Desemba 15, 2025 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi na kubaini kwamba, Sowah alifanya kitendo kisicho cha kiuanamichezo kwa kumpiga kiwiko kiungo wa Azam, Himid Mao.

Kwa upande wa Kante, naye alifanya kitendo kisicho cha kiuanamichezo kwa kumpiga teke kwa makusudi kiungo wa Azam, Feisal Salum.

Mbali na kufungiwa, wachezaji hao kila mmoja ametozwa faini ya Sh1 milioni.

“Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 41:21 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji,” imefafanua taarifa hiyo.

Wakati huohuo, refa wa mechi hiyo ambayo Azam ilishinda 2-0, Abdallah Mwinyimkuu kutoka Singida, ameondolewa kuchezesha katika mizunguko mitano ya Ligi Kuu kwa kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu na kushindwa kuchukua hatua kwa vitendo vya ukiukwaji wa sheria za mpira vilivyofanywa na wachezaji hao ambapo adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kanuni ya 42:1(1.6) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.

Nayo Klabu ya Yanga, imetozwa faini ya Sh5 milioni kwa kosa la shabiki wake kuruka uzio na kuingia kwenye eneo la kuchezea (pitch) wakati timu hiyo ikicheza dhidi ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Jamhuri mkoani Dodoma, ambapo shabiki huyo alionekana kufika hadi kwenye goli la Coastal Union na kuinama kama Ishara ya kutafuta, kuchukua ama kuweka kitu.
Adhabu hii ni kwa mujibu wa Kanuni ya 47:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.

“Bodi ya Ligi Kuu Tanzania inazikumbusha klabu zake kuendelea kusisitiza umuhimu wa mchezo wa kiungwana na tabia njema mchezoni kwa wachezaji, viongozi na mashabiki wake. Ukumbusho huu unakuja kufuatia mfululizo wa matukio ya wachezaji kufanya vitendo visivyo vya kiuanamichezo kwa wachezaji wenzao ikiwemo kupiga.

“Pamoja na kuhatarisha usalama wa wachezaji, matukio hayo pia yamekuwa yakileta taswira mbaya kwa Ligi yetu jambo ambalo linaweza kushusha hadhi yake na kwamba licha ya adhabu kali ambazo zimekuwa zikitolewa kwa wachezaji husika, bado matukio hayo yameonekana kuendelea viwanjani,” imefafanua taarifa hiyo.

Katika hatua nyingine, kiungo wa Singida Black Stars, Khalid Aucho naye amefungiwa mechi tano na faini ya Sh1 milioni kwa kwa kosa la kufanya kitendo kisicho cha kiuanamichezo kwa kumpiga na kumsukuma mchezaji Adam Adam wa TRA United wakati Singida Black Stara ikifungwa 3-1 kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar.

Pia refa wa mechi hiyo, Alex Pancras kutoka Dar es Salaam, amepewa Onyo Kali kwa kosa la kushindwa kutafsiri vema sheria za mpira wa miguu na kushindwa kuchukua hatua stahiki kwa kitendo cha ukiukwaji wa sheria za mpira kilichofanywa na Aucho.