TBS kuja na viwango ufanisi wa nishati vifaa vya umeme, vinavyoingia nchini

Dar es Salaam. Shirika la Viwango Tanzania (TBS), limeandaa viwango vya ufanisi wa nishati ya umeme kwa vifaa vinavyotumia nishati hiyo.

Vifaa hivyo ni runinga, jokofu, AC, feni za kuzunguka mota za umeme na taa ambavyo vitakuwa na nembo ya TBS inayoonesha kiwango cha matumizi ya umeme.

Akizungumza leo Desemba 16,2025 ofisa viwango wa shirika hilo, Mhandisi wa nishati, Spiradson Kagaba amesema kinachosubiriwa ni kutangazwa katika gazeti la Serikali ndipo utekelezaji uanze.

“Lengo la viwango hivi ni kuwasaidia wananchi kutumia umeme kidogo kupitia vifaa hivi. Mtumiaji atavitambua kupitia lebo maalumu iliyoandaliwa na shirika inayoonesha kiwango cha umeme kupitia nyota zilizobandikwa ili mteja anunue.”

“Ukienda kununua kama unataka kifaa kinachotumia umeme kidogo wewe nunua chenye nyota nyingi za kijani unakuwa umepunguza utumiaji wa umeme na umeokoa mazingira,” amesema.

Amesema viwango hivyo vimeandaliwa na vitatumiwa Afrika Mashariki bila kuharibu biashara ambapo faida yake itaokoa umeme pamoja na kulinda mazingira.

Akifafanua zaidi amesema viwango hivyo tayari vipo hivyo vinasubiriwa kutangazwa na Serikali ili vianze kutumika huku akitaja faida zake ikiwa ni pamoja na kutunza mazingira, umeme na kuboresha maisha ya watu.

“Sasa tumekuja na kiwango hicho cha ufanisi wa nishati ambacho ni cha tatu, vikishakuwa tayari kuanza tutaanza kuratibu,” amesema.

Akitoa wito kwa wazalishaji na waingizaji wa vifaa hivyo nchini amesema wanaweza wakaja tukawapimia kwa hiari tukawawekea lebo waende sokoni wakauze.

“Tukianza utekelezaji baada ya kutangazwa na Serikali basi itakuwa haina mjadala hakuna namna itabidi wafuate utaratibu,” amesema.

Amesema utekelezaji ukianza waagizaji wote watabidi walete vifaa vinavyokidhi viwango. Hata hivyo kwa wale ambao wanavyo tayari wameagiza wanaweza kupewa muda (grace period) wauze vikiisha waagize vyenye ubora.

Kuhusu wale wenye tabia ya kukiuka kila maagizo au utaratibu wa serikali amesema watachukuliwa hatua za kisheria.

Katika hatua nyingine, TBS imewataka Watanzania kushiriki katika uandaaji wa viwango vya taifa katika bidhaa na huduma mbalimbali.

Ofisa viwango TBS, Filbeta Magidanga amesema Watanzania wanatakiwa watoa maoni yao aidha wafike ofisini, watume baruapepe, maoni ya kurasa za kijamii au wapige simu ili watoa maoni yao kuhusu viwango.

“Wanatakiwa wahusike kwenye kutoa maoni na mchakato mzima wa uandaaji viwango ili kufanya viwango vya kitaifa viweze kutekelezeka katika kukuza uchumi na biashara za nchi yetu,” amesema.