Dar es Salaam. Wakazi na wafanyabiashara wa mitaa ya Swahili na Donge, Kariakoo, jijini Dar es Salaam, wanaishi kwa hofu kutokana na ubomoaji wa kuta za nyumba na sehemu ya barabara uliofanyika usiku wa kuamkia Desemba 6, 2024, bila makubaliano wala kibali cha mamlaka husika.
Tukio hilo, lililofanywa na mmoja wa majirani, limesababisha uharibifu wa miundombinu ya majitaka, nyufa katika majengo jirani, hasara za kibiashara na kuibua hofu ya kuhatarisha maisha ya wananchi, hususan katika eneo lenye msongamano wa watu.
Hofu imeanza miongoni mwa wananchi wa mtaa huo, huku wakiwa na kumbukumbu ya tukio la kuporomoka kwa jengo la ghorofa nne katika mtaa wa Mchikichi, Novemba 16, 2024, lililosababisha vifo vya watu zaidi ya 30 na majeruhi zaidi ya 80.
Akizungumza na Mwananchi, Desemba 14, 2025, Shekha Viamungu, mtoto wa mmiliki wa jengo la ghorofa tano lililoathirika, amesema ubomoaji huo ulifanyika bila taarifa rasmi, licha ya familia yao kusisitiza umuhimu wa makubaliano na kuzingatia usalama.
“Tulikuwa tayari kukaa chini na kufikia muafaka, lakini bila makubaliano, fensi ilivunjwa usiku, jambo lililosababisha nyufa kwenye jengo na kutulazimu kuhama kwa hofu ya usalama,” amesema.
Amesema juhudi za kupata zuio la polisi hazikufanikiwa, huku Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam ikitoa amri ya kusitisha ujenzi Desemba 11, 2024, ambayo anadai haikuheshimiwa.
Makubaliano yagonga mwamba
Kwa mujibu wa Shekha, awali walipendekeza kukaa chini na mpangaji pamoja na wahusika wote ili kupata suluhu ya pamoja, ikiwemo kumpa mpangaji fremu ili aendelee na maisha bila kuathiriwa.
“Tulifika hatua ya kusema kama kuna hatari kutokana na ubomoaji kwa mmoja wa wapangaji wetu, atafutiwe fremu ili aendelee na biashara zake, kuliko kumtoa hapo halafu wasijue anakwenda wapi, lakini walikataa,” amesema.
Amesema mjenzi wa eneo hilo amedai mpangaji alitaka pesa nyingi ambazo yeye hawezi kutimiza, hali iliyozidisha mvutano na kufanya pande hizo kushindwa kufikia muafaka, huku ikiibuka hoja ya kuzidisha mpaka wa eneo.
Amesema kutokana na utata huo familia hiyo ilipendekeza kufufua mipaka rasmi kwa kuwaita wataalamu wa upimaji ardhi ili kuthibitisha kama kweli wamezidi eneo.
“Tulisema kama tumekosea au tumezidi hata kidogo, tuko tayari kuachia. Eneo linalodaiwa ni dogo na halina faida ya kuleta mgogoro mkubwa namna hiyo,” amesema.
Baada ya vikao kadhaa vikihusisha mwenyekiti wa mtaa, walikubali kuletwa mtaalamu wa upimaji aliyewasilisha vielelezo, lakini familia iliyobomolewa fensi ilihitaji nao kuleta mpimaji mwingine, wakihitaji ripoti rasmi na muhtasari wa maandishi wa upimaji wa awali.
“Baada ya makubaliano hayo, walimleta surveyor, lakini hatukukubaliana naye kwani hatukumuelewa alipodai kuwa tumezidisha futi tatu. Tuliomba ripoti, lakini alisema hawawezi kutoa kwa wakati huo kwa kuwa hawana utaratibu huo,” amesema Shekha.
Familia hiyo imesema licha ya kutokuwepo makubaliano wala kibali, fensi yao ilivunjwa usiku wa manane mwishoni mwa wiki, na kusababisha nyufa kwenye nyumba yao.
“Usiku walikuja wakavunja fensi, hali iliyotutisha, kwani imelazimu kuhama kwa kuhofia usalama wetu baada ya kuona nyufa.
“Baada ya tukio hilo, tulikwenda kituo cha polisi kutafuta zuio (stop order), lakini tuliambiwa polisi hawawezi kuzuia shughuli hizo bila kibali cha mahakama,” amesema.
Anaongeza kuwa walipeleka malalamiko yao Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, ambapo walidai kupatiwa amri ya kusimamisha ujenzi (stop order) iliyotolewa Desemba 11, 2024, ikimtaka muhusika kusitisha shughuli zote hadi suala hilo litakapopatiwa ufumbuzi wa kisheria.
Licha ya amri hiyo, Shekha amedai muhusika aliendelea na ujenzi hadi usiku wa Desemba 13, hali iliyoibua maswali kuhusu utekelezaji wa uamuzi wa mamlaka husika.
Mfanyabiashara wa eneo hilo, Khalfan Masoud, amesema amepata hasara na anaishi kwa hofu baada ya ukuta wa eneo analofanyia biashara kubomolewa, tukio lililosababisha bidhaa zake kubaki wazi nje bila ulinzi.
“Wakati wanabomoa sikuwapo, nimesikia watu wamekuja kubomoa na kuacha stoo ikiwa wazi, mizigo iko nje, na hatua hiyo inaweka mazingira ya kuibiwa, huku jengo lenyewe likiwa katika mazingira yanayoweza kusababisha ajali,” amesema Masoud.
Athari nyingine za ubomoaji wa fensi na ujenzi huo ni kuathiriwa kwa mfumo wa majitaka pamoja na barabara ya mtaa wa Donge, ambayo imepasuka na kusababisha kuwekwa bati kuzuia madhara zaidi.
Alipoulizwa kuhusu athari hiyo, Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura), Wilaya ya Ilala, John Magori, amesema watakagua ujenzi huo na endapo kutabainika uharibifu wowote, watachukua hatua za kisheria.
“Sina taarifa kuhusu uharibifu wa barabara ya mtaa wa Donge na Swahili, lakini kwa kuwa umeniuliza hapa, nitaomba nifuatilie kesho asubuhi, nikaangalie uharibifu uliofanyika, kisha tutachukua hatua na kutoa adhabu kwa mujibu wa sheria,” amesema Magori.
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) imetoa ufafanuzi kuhusu tukio la kuporomoka kwa chemba ya taka katika eneo la Kariakoo, ikieleza kuwa chanzo chake ni shughuli za uchimbaji wa msingi wa jengo la ghorofa lililokuwa likijengwa karibu na miundombinu hiyo.
Msimamizi wa Dawasa eneo la Kariakoo, Joseph Tillya, amesema chemba zilizopo eneo hilo ni fupi na baadhi yake hupitisha maji taka kutoka maeneo mbalimbali.
“Chemba zetu hapa ni fupi, kuna iliyopo pembeni ambayo hupitisha majitaka kutoka Hoteli ya Cate na nyumba nyingine. Wakati wa kuchimba kwenda chini kwa ajili ya ujenzi, waligusa miundombinu yetu na kusababisha chemba ishuke,” amesema Tillya.
Kwa mujibu wa Tillya, Dawasa ilitoa maelekezo juu ya hatua za kuchukua kabla ya kuendelea na ujenzi, ikiwemo kuziba bomba na kulifanya liunganishwe moja kwa moja bila kupitisha maji takakwenye chemba iliyoharibika.
“Niliwaeleza kabla ya kuendelea na ujenzi, walipaswa kuziba bomba na kufanya muunganisho mpya usiopitia kwenye chemba ile, kisha baadaye wangeweza kuendelea na ujenzi wa ghorofa,” amesema.
Ameongeza kuwa mkandarasi alikubali maelekezo hayo na kuleta watu wa kurekebisha miundombinu. Hata hivyo, kulikuwa na ucheleweshaji wa utekelezaji, kabla ya kufanyika tena ukarabati Desemba 14.
“Miundombinu ya majisafi na maji taka ni nyeti. Ni muhimu kabla ya kuchimba au kujenga, wahusika wawasiliane na Dawasa ili kuepuka uharibifu na hatari kwa jamii,” amesema.
Tillya amesema Dawasa itaendelea kusimamia miundombinu yake na kutoa maelekezo ya kitaalamu ili kuepusha madhara makubwa zaidi, huku akiwataka wajenzi wote kuhakikisha wanashirikisha mamlaka husika kabla ya kufanya uchimbaji karibu na miundombinu ya maji na maji taka.
Naye, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mnanzi Mmoja, Baraghashi Azimio, amesema ofisi yake haikushirikishwa kikamilifu katika hatua za awali za ujenzi wa jengo lililosababisha mgogoro wa ubomoaji wa ukuta na uharibifu wa miundombinu ya majitaka na barabara katika eneo hilo.
Amesema baada ya kupata taarifa, alipita eneo hilo, Desemba 13, na kujionea uharibifu, huku akisubiri siku ya kazi kupeleka malalamiko ofisi ya kata.
“Hatupingi maendeleo, tunachotaka ni taratibu zifuatwe na wananchi walindwe. Serikali ya mtaa iko tayari kushirikiana na kila upande,” amesema Azimio.
Hata hivyo, amesema ofisi yake itaendelea kufuatilia suala hilo kwa kushirikiana na kata na mamlaka husika ili kuhakikisha usalama, afya na haki za wananchi.
Mwenyekiti huyo amesema mtaa hauna vita dhidi ya maendeleo, lakini ni muhimu miradi yote kufuata sheria, taratibu na kushirikisha viongozi wa eneo husika ili kuepusha migogoro na madhara kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mipango Miji Na. 8 ya mwaka 2007, Kifungu cha 31, kinakataza mtu yeyote kufanya ujenzi, ubomoaji au mabadiliko ya miundombinu bila kibali cha mamlaka husika.
Kwa upande wa usalama, Sheria ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2004 inamtaka mwajiri au mkandarasi kuhakikisha mazingira ya kazi ni salama kwa wafanyakazi na jamii inayozunguka eneo la kazi.
Vilevile, Sheria ya Barabara Na. 13 ya mwaka 2007, Kifungu cha 49, kinakataza mtu kuharibu barabara bila kibali cha mamlaka husika.
Kauli ya mkandarasi wa jengo
Mkandarasi wa jengo hilo, Khamis Mkude, amesema hitilafu zilizojitokeza wanazifanyia kazi kwa kujenga upya ukuta wa zege (retaining wall), na wameanza maandalizi ya kurejesha eneo lililoathirika, ikiwemo chemba ya maji taka na kipande cha barabara.
“Tumerekebisha sehemu iliyoharibika kwenye mfumo wa majitaka kwa kurejesha mabomba. Hatua inayofuata ni kujenga tena retaining wall ili kuimarisha eneo lote lililoharibika,” amesema Mkude.
Pia amesema vifusi vilivyowekwa pembeni vitaondolewa na eneo kusafishwa kabla ya kuendelea na uchimbaji na ujenzi kwa utaratibu mpya uliopendekezwa.
Mkandarasi huyo amesema yuko tayari kushirikiana na mamlaka zote husika, akiwemo Dawasa na Serikali za mitaa kuhakikisha ujenzi unaendelea bila kuhatarisha miundombinu ya umma wala usalama wa wananchi.
“Kama kuna tatizo lolote, tuko tayari kupigiwa simu na kufika mara moja. Hatutaki migogoro, tunataka kazi iende kwa usalama na kwa kufuata taratibu,” amesema.
Mkude amesema lengo lao ni kukamilisha mradi huo bila kusababisha madhara kwa jamii inayozunguka eneo la ujenzi.
Mkuu wa Idara ya Ardhi na Mipango Miji wa Jiji la Dar es Salaam, Maduhu Ilanga, amesema ofisi yake ilichukua hatua baada ya kupokea taarifa za awali kuhusu tukio hilo, kwa kuelekeza wahandisi kufanya tathmini ya kitaalamu.
Amesema baada ya kupata taarifa hizo, alielekeza wataalamu kwenda eneo la tukio kufanya tathmini ya kina kubaini hali halisi na chanzo cha tatizo.
Ameeleza kuwa ujenzi wa aina hiyo katika eneo lenye msongamano mkubwa wa watu na majengo kama Kariakoo hauwezi kuchukuliwa kirahisi, kwani unaweza kuhatarisha usalama wa majengo jirani pamoja na maisha ya wananchi.
Kwa mujibu wa Ilanga, jiji linaendelea kufanya uhakiki ili kubaini kama taratibu zote za kisheria zilifuatwa, ikiwemo suala la vibali vya ujenzi, huku nyaraka husika zikiendelea kufanyiwa uchunguzi.
Amesema masuala ya ujenzi, hususan yanayohusisha uchimbaji wa chini ya ardhi, hayapaswi kubezwa kwani yanaweza kusababisha majanga makubwa, yakiwemo kuporomoka kwa majengo na kupotea kwa maisha ya watu.