Ukame unavyozua hofu ya uhaba wa chakula nchini

Dar es Salaam. Tanzania inatabiriwa kukumbwa na hali ya ukame. Hali hiyo itaathiri uzalishaji wa chakula na kutishia kuliingiza Taifa katika uhaba wa chakula.

Hiyo ni kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), iliyotabiri baadhi ya mikoa kukumbwa na mvua za chini ya wastani na wastani, na vipindi virefu vya ukavu.

Mamlaka hiyo imetaja mikoa itakayokumbwa na hali hiyo kuwa ni Dodoma, Katavi, Kigoma, Singida, Tabora, Iringa, Mbeya, Mtwara, Njombe, Songwe, Rukwa, Ruvuma na Morogoro.

Tishio la uhaba wa chakula linatokana na ukweli kwamba baadhi ya mikoa itakayokabiliwa na hali hiyo ni miongoni mwa ile inayoongoza kwa uzalishaji wa chakula nchini, ikiwemo Ruvuma, Njombe, Mbeya na Morogoro.

Hofu zaidi kuhusu uhaba wa chakula imetokana na kilichoelezwa na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, aliyewataka wakulima kuhifadhi mazao kutokana na utabiri wa uchache wa mvua zinazotarajiwa.

Licha ya tishio hilo, wataalamu wanasema bado kuna nafasi kwa Tanzania kuzalisha vema katikati ya hali ya ukame itakayoiathiri, iwapo wakulima na wafugaji watazingatia mbinu za kitaalamu.

Akizungumzia utabiri huo, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk Ladislaus Chang’a, amesema utabiri huo ulitolewa tangu Septemba mwaka huu.

Katika utabiri huo, amesema ilionesha baadhi ya mikoa itapata mvua za chini ya wastani na mingine itakumbwa na vipindi virefu vya ukavu.

“Hii maana yake mikoa husika itapata mvua kwa uchache na itakuwa na vipindi virefu vya ukavu kwa maana havitakuwa na mvua ya kutosha,” amesema Dk. Chang’a.

Wakulima wazingatie haya…

Kutokana na matarajio ya hali hiyo, Mkurugenzi wa Utafiti na Ubunifu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari), Dk Deusdedith Mbanzibwa, amesema katika nyakati kama hizi, wakulima wanapaswa kuzingatia mambo matatu ambayo ni kuhakikisha wanapanda mazao pale mvua zinaponyesha kwa mara ya kwanza, wasisubiri zaidi.

Pia amesema wahakikishe wanashirikiana na mabwana shamba ili kuwapatia teknolojia zinazohimili ukame ambazo tayari Tari ilishawapatia.

Pamoja na hilo, amesema hata mbegu watakazozitumia wahakikishe ni zile zinazokomaa mapema na kustahimili ukame, na tayari Tari imeshafanya utafiti na kuzalisha mbegu hizo.

“Tari ina mbegu za mahindi za T105 na T104, hizi zimefanyiwa utafiti na kuzalishwa na Tari maalumu kwa ajili ya kustahimili ukame. Mbegu hizo zinakomaa mapema na kuzaa kwa muda mfupi,” amesema.

Mbegu nyingine zilizozalishwa na taasisi hiyo maalumu kwa kipindi kama hiki ni Situka M1 na TMV1, ambazo hufanya zao likomae kwa muda mfupi na kuvunwa haraka.

Sambamba na hilo, amesema wakulima pia wanapaswa kuzingatia mazao yanayostahimili ukame, ikiwemo mihogo kwa maeneo yanayostawi.

“Hizi ndizo mbinu zinazowezesha kuzalisha mazao kwa wingi nyakati za ukame. Ndizo njia za kitaalamu za kuzalisha nyakati kama hizi, hivyo ni muhimu wakulima washirikiane nasi ili kuzalisha kwa wingi,” amesema.

Mkurugenzi Uzalishaji wa Ndani na Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Louis Kasera, amesema mamlaka hiyo imeshapeleka mbolea ya kupandia kwa wakulima.

Kwa kuwa inatambua uwepo wa hali ya ukame, amesema imepeleka mbolea hiyo ili kuwezesha wakulima kupanda mazao mara tu mvua inaponyesha.

Baada ya kupeleka mbolea hiyo, amesema kinachofuata ni kupeleka mbolea kwa ajili ya kukuzia mazao, na kwamba Desemba 15 mwaka huu, wamepokea zaidi ya tani 100,000 za mbolea hiyo.

Mbolea ya kukuzia mazao, amesema, itapelekwa kwa wakulima baada ya mvua kunyesha kwa kuwa yenyewe huwekwa kwa ajili ya kukuza zao.

“Hapa nipo bandarini (Desemba 15, saa 4 asubuhi), tunapokea zaidi ya tani 100,000 ya mbolea ya kukuzia, na mvua zitakaponyesha tutasambaza kwa wakulima kwa ajili ya kuzalisha zaidi,” amesema Kasera.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafugaji Tanzania, Jeremiah Wambura, amesema wenye mifugo mingi, wanapaswa kuipunguza ili kuwekeza kwenye miundombinu ya malisho na maji.

Amesema ukame mara nyingi huathiri malisho na upatikanaji wa maji kwa wafugaji, hivyo wasione tabu kupunguza idadi kadhaa ya mifugo kununua teknolojia za upatikanaji wa malisho na maji.

“Kama una ng’ombe 500, usione hasara kuuza 30 ili uchimbe kisima cha maji na kulima mazao ya malisho ya mifugo. Ukifanya hivyo mara moja inakusaidia kila mwaka ukame utakapofika,” amesema Wambura.

Pia, amesema mvua chache zitakazonyesha wafugaji wazitumie kuzalisha malisho na vyakula vyao binafsi kwa sababu pia wanahitaji kula.

Alipoulizwa uhusiano wa ukame na kupanda kwa bei ya nyama, Wambura amesema mara nyingi mifugo inapokosa malisho na maji, inapoteza nguvu na mingine kupoteza uhai.

“Kipindi cha ukame ndicho ambacho wafugaji tunapoteza mifugo mingi. Huwa inakufa kwa sababu haipati chakula na maji, na magonjwa huwa mengi. Ikitokea hali hiyo, minadani kunakosekana mifugo,” amesema na kuongeza mifugo inapokuwa michache minadani, inauzwa kwa gharama kubwa na kufanya bei yake kupanda.

Hata hivyo, amesema, hatua ya kupanda kwa bei ya nyama sasa haihusiani na ukame, bali ni wingi wa masoko ya bidhaa za mifugo.

Ameeleza kuwa wafugaji sasa wanauza mifugo yao na wanalipwa kwa kilo, hivyo wengi wameacha kupeleka ng’ombe, mbuzi na kondoo minadani.

Mabadiliko hayo amesema yametokana na Tanzania kukidhi matakwa ya kimataifa ya uuzaji wa mifugo, hivyo mingi inasafirishwa kwenda nje ya nchi.

“Mtu hawezi kuleta ng’ombe mnadani akijua bei ni ndogo ukilinganisha na kwenye masoko ya mifugo au kimataifa. Sasa minada ikikosa mifugo, mabucha lazima yapandishe bei ya nyama,” amesema.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Dk Andrew Komba, amesema hata ikitokea Tanzania imeshindwa kuzalisha chakula, ina uwezo wa kujilisha kwa kipindi cha miezi sita.

Hilo linatokana na kile alichoeleza, wakala huo umehifadhi takriban tani 592,000 za mahindi zenye uwezo wa kulilisha taifa kwa kipindi cha miezi sita, hata ikitokea uzalishaji umekwama.

Kiwango hicho kilichohifadhiwa, amesema, ni juu ya kiasi kinachostahili kuhifadhiwa na taifa, ambacho ni tani 300,000, hivyo Tanzania haitapata shida hata ikitokea ukame umeathiri uzalishaji.

“Tuna hifadhi ya kutosha, hatuwezi kupata shida kama litatokea lolote. Sisi kazi yetu ni kuhifadhi, na tumehifadhi tani 592,000,” amesema Dk Komba.

Alipoulizwa iwapo bado wanatoa vibali vya kuuza zao hilo nje ya nchi, amesema ni vigumu kueleza hilo kwa sababu za kiitifaki.

Amesema Tanzania ina washindani katika biashara hiyo, hivyo chochote itakachosema kama inauza mahindi nje au vinginevyo inampa mshindani nafasi ya kufanya kitu.

“Suala la kuuza ni mambo ya ndani, kibiashara sio vizuri kusema kama tunatoa vibali vya kuuza au vinginevyo kwa sababu sisi tuna washindani wa Zambia na Mexico,” amesema.

Katika kikao chake na wakuu wa mikoa, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, amewataka Watanzania watunze akiba ya chakula na waepuke matumizi yasiyofaa kutokana na kuchelewa kwa msimu wa mvua mwaka huu.

Katika maelekezo yake hayo, alirejea taarifa ya TMA, iliyotabiri mwelekeo wa msimu wa mvua za vuli na mvua za msimu kwa kipindi cha Oktoba 2025 hadi Desemba 2025 na kipindi cha Novemba 2025 hadi Aprili 2026 mtawalia.

“Kutokana na utabiri huo, baadhi ya mikoa nchini inatarajiwa kuwa na mvua za chini ya wastani hadi wastani, na kutawaliwa na vipindi virefu vya ukavu na mtawanyiko wa mvua usioridhisha,” amesema.

Amesema utabiri huo unaonesha hali ya kuchelewa kwa mvua inatarajiwa katika mikoa ya Dodoma, Katavi, Kigoma, Singida, Tabora, Iringa, Mbeya, Mtwara, Njombe, Songwe, Rukwa, Ruvuma pamoja na Kusini mwa Mkoa wa Morogoro.

“Pamoja na kuwa hakuna tishio la uhaba wa chakula kutokana na hifadhi ya chakula iliyopo nchini, ni vema wananchi waendelee kuzingatia matumizi sahihi ya chakula. Tuna akiba ya chakula ya kutosha, lakini ninawasihi wananchi waweke akiba na kuepuka matumizi yasiyo ya lazima,” amesema.

Amewataka wakulima waandae mashamba kwa wakati na watumie pembejeo zinazoendana na upatikanaji wa mvua chache, pia wazingatie ushauri wa wataalamu wa kilimo wanaozungumza nchi nzima kutoa elimu kwa wakulima.

Kwa upande wa wafugaji, amewataka waweke mipango mizuri ya matumizi na uhifadhi wa maji na vyakula vya mifugo ili kukabiliana na hali hiyo.