Ulimwengu akumbushia sakata lake, Balozi Bandora kuvuliwa uraia

Dar es Salaam. Mwandishi wa habari mkongwe nchini, Jenerali Ulimwengu amekumbushia namna yeye na wenzake wanne, akiwemo Balozi Timothy Bandora, walivyovuliwa uraia wa Tanzania na utawala wa awamu ya tatu.

Ulimwengu amesema hayo leo Desemba 16, 2025 wakati wa mazishi ya mwanadiplomasia mkongwe nchini, Balozi Bandora ambayo yamefanyika jijini Dar es Salaam.

Bandora alifariki dunia Jumapili, Desemba 14, 2025, akiwa nchini Kenya, ambako alikuwa akipatiwa matibabu.

Akizungumzia katika salamu zake za rambirambi, Ulimwengu, alikumbushia namna walivyofutiwa uraia wa Tanzania na wenzake hao, wakiwamo vongozi wawili wa CCM.

Februari 12, 2002 Serikali ya Tanzania ilitangaza kuwafutia uraia Ulimwengu, Moudline Castico (alikuwa katibu mwenezi wa CCM Zanzibar), Anatory Amani (alikuwa kiongozi wa CCM Mkoa wa Kagera) na Timothy Bandora.

Hata hivyo, Castico, Amani na Bandora walipewa tena uraia, isipokuwa Ulimwengu ambaye alikaa kwa takriban miaka miwili bila uraia.

Ulimwengu amemtaja Bandora kwa namna ya kipekee akianza na maisha yake ya utotoni, akisema alikuwa rafiki yake waliyefahamiana tangu wakiwa wanafunzi huko Tabora.

“Nilifanya naye kazi katika maeneo mbalimbali, baadaye aliteuliwa na Rais Mkapa (Benjamin) katika nyadhifa mbalimbali lakini baadaye alipokwenda kwa Obasanjo (Rais Olusegun Obasanjowa Nigeria) Nigeria, Rais Mkapa alisahau kuwa alimteua yeye, akasema Bandora si raia wa Tanzania.

“Lakini baadaye dunia ilimtambua Bandora akapaa katika diplomasia za kimataifa akashika nyadhifa mbalimbali za kimataifa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa,” amesema Ulimwengu na kuongeza:

Familia ya marehemu, Balozi Timothy Bandora wakiwa na ndugu zao, wakitoa heshima za mwisho kwa marehemu katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga

“Nilimjua Bandora akiwa mtoto mdogo akiwa mwanafunzi pale Shule ya Wavulana Tabora, nilimjua kama kijana mwenye kipaji sana, alikuwa akiongea Kingereza fasaha sana, ndiyo iliyokuwa sifa yake kuu,” amesema Ulimwengu.

Mwili wa Bandora umeagwa katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Msasani jijini Dar es Salaam.

Katika ibada iliyotawaliwa na simanzi kwa waombolezaji na waumini, Bandora ametajwa kama mwanadiplomasia mashuhuri ambaye kifo chake kimeacha pengo kubwa nchini.

Akisoma na kunukuu katika andiko la Biblia, (Matendo ya Mitume 4:12), Mchungaji Kurwa Sadataley amesisitiza imani ya wokovu wa Mungu, akiwasihi wanafamilia na waombolezaji kumtegemea Mungu kwa kuwa yeye ndiye tegemeo la mwanadamu.

“Natoa pole kwa wanadiplomasia wote wastaafu na waliopo kazini, kwani moja ya maktaba imeondoka, tumempoteza mtu muhimu sana, na tunapowapoteza watu kama hawa ni hasara kwa Taifa na kwa kizazi kinachokuja,” amesema Mchungaji huyo.

Mchungaji huyo ameongeza kuwa katika maisha yake, Bandora alikuwa mtu aliyemtegemea Mungu katika kazi zake zote, licha ya mafanikio aliyokuwa nayo.

“Kinyume na watu wengine wanapofanikiwa wanaomwacha Mungu, yeye pamoja na nafasi zote alizopitia alikuwa mtu aliyemtanguliza Mungu katika kila jambo lake.

“Alikuwa mtu akiyekubali na kumfuata Yesu Kristo, watoto msimuache Mungu, kifo hiki kinatukumbusha tu kuwa Mungu yupo, kikubwa tambua kuwa hapa duniani tunaishi muda mfupi tu,” amesisitiza.

Ameongeza kuwa BaloziBandora alikuwa mtu muwazi, aliyenyooka na hakupindapinda kama baadhi ya wengine.

Balozi Bandora ameelezwa kuwa alianza maisha yake ya awali huko Tabora alipozaliwa katika familia ya Mchungaji Paul Bandora na Magreth Bandora. Alianza maisha yake huko Tabora vijijini alikozaliwa na kupata elimu yake ya msingi.

Bandora alisomea Tabora, akipita katika shule za Mirambo na Tabora Boys na baadaye akajiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kusomea fani ya Siasa za Kimataifa na Sayansi ya Siasa.

Mwaka 1976 baada ya kuhitimu masomo yake, alianza utumishi wake wa umma, akichaguliwa kuwa mjumbe wa kudumu Umoja wa Mataifa.

Kati ya nyadhifa nyingi alizohudumu kwenye uhai wake, mbali na kusuluhisha migogoro mingi, alishiriki kuandaa mfumo wa amani na usalama wa Umoja wa Afrika na kuanzisha mpango wa upimaji wa utawala bora Afrika.

Vilevile, alikuwa mjumbe wa Kamati ya Ufundi ya Kuunda utawala na usalama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na mjumbe wa mkutano wa utulivu, usalama na maendeleo ya Afrika.

Bandora pia alihudumu kama mjumbe wa wataalamu wa ulinzi chini kamisheni ya marais wa India, Argentina, Mexico na Tanzania.

Pia alihudumu kama mjumbe wa Kamati ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu mahusiano ya kiutawala.