Vijana Mara wafunzwa kujikwamua kiuchumi

Musoma. Baadhi ya vijana katika Manispaa ya Musoma mkoani Mara wamesema licha ya kuelezwa juu ya uwepo wa fursa nyingi za kiuchumi bado wanakabiliwa na ukosefu wa elimu na namna ya kuzitumia, ili ziweze kuwanufaisha na kuwakwamua kiuchumi.

Vijana hao wameyasema hayo leo Jumanne Desemba 16, 2025 mjini Musoma wakati wa kongamano la mabadiliko ya kiuchumi kwa vijana lililoandaliwa na Mbunge wa Musoma Mjini, Mgore Miraji.

Othman Hussein amesema vijana wengi wanashindwa kutumia fursa ambazo wanaelezwa kuwa zipo kutokana na kukosa elimu juu ya namna ya kuzitumia sambamba na utambuzi wa fursa zenyewe.

“Wanasema tukakope sasa unajiuliza nakopa kisha nafanyia nini huo mkopo kwa sababu mwisho wa siku nitatakiwa kuurejesha, hivyo wengi wetu tunaishia kukata tamaa hatujui tufanye nini, mamlaka husika zitoe elimu kwa vijana ili waweze kuwa na uelewa mpana juu ya namna kunufaika na fursa hizo,” amesema.

Mwenyekiti wa madereva bajaji Manispaa ya Musoma, Emmanuel Tuma amesema sio kweli kuwa vijana hawapendi kujituma isipokuwa changamoto za ukosefu wa mitaji pia ni kikwazo kingine kinachosababisha washindwe kufanya shughuli zao ikiwemo kujiajiri.

Miraji amesema lengo la kuandaa kongamano hilo ni kutaka kutafuta suluhisho la kudumu juu ya changamoto zinazowakabili vijana katika jimbo hilo hususan ya ukosefu wa ajira.

Amesema wakati wa kampeni aliahidi kuwa sehemu ya utatuzi wa changamoto za wakazi wa jimbo hilo ikiwepo changamoto kubwa ya ajira na uchumi wa mtu mmoja mmoja.

“Manispaa yetu ina wakazi zaidi ya 160,000 na asilimia 60 ya wakazi hao ni vijana na takwimu zinaonyesha vijana ndio waathirika wakubwa wa suala hili la ukosefu wa ajira, hivyo nimeamua kwa kutumia nafasi yangu niwe sehemu ya kutafuta suluhisho kudumu kwa kundi hili kubwa na muhimu kwa ustawi wa jamii yetu,” amesema.

Miraji amesema hakuna sababu ya vijana kusubiri ajira kutoka serikalini kwa maelezo kuwa ukosefu wa ajira ni changamoto ya dunia nzima, hivyo suluhisho pekee ni kutumia fursa zilizopo ili kuzalisha ajira nyingi kadri iwezekanavyo.

Ametaja baadhi ya fursa zilipo jimboni humo kuwa ni pamoja na ufugaji wa samaki kwenye vizimba, ufugaji, kilimo, utalii na maliasili  ambazo zikitumiwa vema zitakuwa na matokeo chanya kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na jimbo kwa ujumla.

Akifungua kongamano hilo, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka amesema umefika muda sasa vijana waanze kufikiria tofauti ili kuweza kunufaika na fursa zilizopo ili ziweze kuwanufaisha.

“Sasa hivi kila kijana anawaza kuwa bodaboda, hii sio sawa vijana tunatakiwa tuanze kujihusisha na sekta zingine za uzalishaji ili kuwa na wigo mpana yaani wakati wengine wako kwenye usafirishaji wengine wanakuwa kwenye sekta kama ufugaji, kilimo, utalii na ujasiriamali mwingine ili kutengeneza mnyororo mzuri wa kiuchumi.”

“Mimi naamini katika matokeo, kongamano hili liwe mwanzo wa matokeo chanya yaani ni mwendo wa michongo kwa vijana tunapaswa kuwaonyesha fursa zilipo na namna wanavyotakiwa kuzitumia, huu ni wakati wa vijana kumiliki uchumi mkubwa,” amesema Chikoka.