Wakulima wa korosho Lindi wavuna Sh82 bilioni

Lindi. Wakulima wa zao la korosho mkoani Lindi kupitia chama Kikuu cha Ushirika Lindi Mwambao tayari wameshapata fedha zao katika minada mitano iliyofanyika.

Akizungumza baada ya kumaliza mnada wa sita wa zao hilo leo Jumanne ,Desemba 16,2025 Kaimu Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Lindi Mwambao, Hassan Dossa amesema kuwa hadi sasa tani 42,000 zimeuzwa katika minada mitano ,ambapo pesa iliyotolewa kwa wakulima ni Sh82 bilioni.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa chama hicho, kinachounganisha Wilaya tatu za Lindi ,Kilwa pamoja na Halmashauri ya Mtama, Ismail Nalinga amesema kuwa jumla ya tani elfu moja za korosho zimeuzwa katika mnada wa sita ambao bei ya chini kwa korosho daraja la kwanza imeuzwa Sh2,110 na bei ya juu Sh2,270 na korosho daraja la pili bei ya chini Sh1,770 ya juu Sh1,830.

Pia amesema malengo ya chama kikuu ilikuwa kukusanya korosho tani 45,000 lakini hadi sasa wamefikisha tani 42,000.

Amesema kuwa changamoto iliyosababisha kutofikisha malengo ni wakulima kupeleka korosho ambazo hazina ubora, na amewataka kujitahidi kuongeza umakini katika uandaaji wa zao hilo,  ili kupeleka zenye ubora zinazoweza kuuzwa kwa bei ya juu kwenye mnada.

Kwa upande wake Ofisa biashara kutoka TMX, Janeth Mhegele amesema kuwa wameuza korosho zote kutoka chama kikuu cha Lindi mwambao tani 1,000, na kuwataka wakulima kuzingatia ubora wa korosho ili kuweza kupata bei nzuri kwa minada iliyobakia.

Naye mkulima kutoka kata ya Mnolela, Nassoro Ally amesema kuwa wameuza korosho kwa bei nzuri kutokana na aina ya korosho walizokuwa nazo na kuwaomba wakulima kuzingatia ubora ili waweze kupata bei nzuri zaidi kwa minada ijayo.