Shinyanga. Kufuatia nyumba zaidi ya 200 ikiwemo zahanati ya kijiji cha Mwanase Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga kubomolewa na mvua usiku wa kuamkia Desemba 13,2025, Serikali mkoani humo imeielekeza Halmashauri ya Msalala kufikisha mara moja misaada ya kibinadamu katika eneo hilo.
Mvua hizo zilisababisha kuezuliwa kwa mapaa katika nyumba 127 huku nyumba 80 zikibomoka kabisa na wananchi kubaki bila makazi, vyakula, mazao shambani na mifugo vikisombwa na maji.
Agizo hilo limetolewa leo Jumanne Desemba 16,2025 na Mwenyekiti wa kamati ya maafa mkoani humo, Mboni Mhita, baada ya kuzitembelea baadhi ya familia zilizopata maafa na kuzungumza na baadhi ya waathiriwa hao.
Mboni ambaye ni mkuu wa mkoa huo, amemwelekeza mhandisi wa ujenzi katika Halmashauri ya Msalala, Juma Magoto, kupeleka wataalamu wa ujenzi kutoa elimu ya ujenzi wa nyumba bora zinazoweza kustahimili mvua na upepo mkali kwa wananchi hususani wanaoishi vijijini.
Akieleza chanzo cha maafa hayo amesema halmashauri hiyo ni eneo la kilimo cha mpunga na udongo ni wa mvinyanzi, huku kukiwa ni makazi ya watu hali inayosababisha kubomoka kwa nyumba pale matofali yanapolowana kidogo.
“Tunaendelea kutoa elimu namna bora ya kuboresha ujenzi wa nyumba bora ikiwemo kuchoma matofali, wataalamu wetu wanaendelea kutoa elimu kwa wananchi.”
Mmoja wa walioathiriwa na mvua hizo, Catherine Daudi amesema, “huyu mjukuu wangu alikuwa amejiviringisha kwenye chandarua kitandani, matofali yalivyoanza kuporomoka akaniita bibi bibi niokoe, ndipo nikakimbia kumtoa. Nashukuru Serikali kutufikia, lakini sina unga, nile nini? Kila kitu kimesombwa ndani, sufuria, vyakula vyote sina.”
Magoto amesema gharama ya ukarabati wa zahanati ya kijiji cha Mwanase iliyoezuliwa paa ni Sh3.4 milioni.
“Jumla ya Sh3.4 ndio gharama ambazo tumebaini zinaweza kurejesha hali ya hili jengo, lakini vile vile tumefanya tathmini nyingine kwamba akina mama wanaohitaji kujifungua watatumia zahanati ya kijiji jirani ambayo haipo mbali kutoka hapa.”
Awali Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwanase, Musa Lubugu alisema kuwa kwa sasa wananchi waliopata athari katika nyumba zao wamepewa hifadhi kwa majirani zao.
Amesema, “hakuna madhara ya kibinadamu yaliyojitokeza, wengi vyakula vyao vimeloana ila kwa kipindi hiki ambacho mvua inanyesha wanahitaji kupatiwa msaada wa haraka ili waweze kujikimu na hali hii.