Dar es Salaam. Jumla ya wanafunzi 115 waliofanya vizuri kwenye nyanja mbalimbali kwa mwaka wa masomo 2024/2025 katika Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), wametunukiwa tuzo na zawadi huku asilimia 60 walioongoza wakiwa ni wanawake.
Hayo yamesemwa leo Jumanne Desemba 16, 2025 na Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Evaristo Liwa kwenye sherehe za utoaji wa zawadi zilizofanyika katika chuo hicho, jijini Dar es Salaam.
Profesa Liwa amesema kati ya wanafunzi hao 115 waliopata tuzo, wanawake ni 63 ikiwa ni sawa na asilimia 60 ya wanafunzi wote waliotunukiwa tuzo hizo huku wanaume wakiwa 52.
“Japokuwa katika kuangalia hatukuwa tunaangalia jinsia, lakini kulingana na matokeo yao ndio imekuja idadi hiyo kuwa asilimia 60 wanawake walifanya vizuri zaidi,” amesema Profesa Liwa.
Hata hivyo, Makamu huyo amesema katika tuzo hizo zipo zilizotolewa na chuo, na zipo zilizotolewa na taasisi, kampuni mbalimbali na watu binafsi ambao huwazawadia waliofanya vizuri katika eneo fulani.
“Tuzo hizi ambazo zimeanza kutolewa miaka 40 iliyopita, zimekuwa na faida sio tu kwa chuo na wanafunzi bali na kampuni na taasisi, ambazo zimekuwa ni rahisi pia kuwapata wanafunzi wanaowahitaji kuwaajiri baada ya kuhitimu masomo yao,”amesema.
Profesa Liwa amewataka wanafunzi kuendelea kujitahidi kusoma huku akiwaomba wadau kujitokeza kwa kuwa mbali ya kutumia kama jukwaa la kujitangaza lakini pia linasaidia kukitangaza chuo na kuongeza udahili.
Awali, Naibu Makamu Mkuu- Taaluma, Utafiti Ushauri wa chuo hicho, Profesa John Lupala, amesema kwa miaka kadhaa sasa, sherehe za utoaji zawadi kwa wanafunzi zimekuwa zikiwezeshwa na wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakijitolea ufadhili wa hali na mali.
Profesa Lupala amesema kwa upande wa mshindi wa jumla, mwanafunzi mmoja ndio ameibuka mshindi kwa kupata GPA ya 4.4 ambayo ni daraja la kwanza la ufaulu.
Naye Meneja wa habari na Uhusiano wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Muungano Saguya, ambao ni moja ya wadau waliotoa zawadi kwa wanafunzi hao, amesema shirika hilo kila mwaka limekuwa likishiriki tuzo hizo kwa sababu wanataka kuchochea ufaulu mkubwa wanafunzi.
Pia Saguya amesema ni katika kuwapa moyo wanafunzi kuweza kujifunza zaidi wakijua hao ndio waajiriwa watarajiwa wa shirika hilo kwa siku zijazo.
‘Kama mnavyojua shirika letu shughuli zake zinauwiana sawia na masomo yanayotolewa na chuo hiki, hivyo sisi tunakuwa hapa kama sehemu ya chachu ya kuwezesha wanafunzi kuongeza juhudi katika masomo yao,” amesema Saguya.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Jefta Clement, ambaye pia ndio mshindi wa jumla, ameupongeza uongozi wa chuo kwa kutambua na kuthamini ufaulu wa wanafunzi.
“Nakipongeza chuo kwa utaratibu wake huu kwa kuwa wangeweza kukaa kimya katika hili, lakini wakaona ni vema kuwatambua wale waliofanya vizuri zaidi ya wenzao, niseme tunashukuru,” amesema.
Aidha Clement amesema tuzo hizo walizozipata sio za kwao peke yao bali ni matokeo ya msaada, malezi, ushauri wa viongozi waliokuwa wanawasaidia wakiwa chuoni hapo.
