Wastaafu Dodoma kupatiwa vitambulisho vya kielektroniki

Dodoma. Wizara ya Fedha imetoa wito kwa wastaafu wa Wilaya ya Dodoma Mjini wanaolipwa na Hazina kufika Ofisi za Hazina Dodoma ili kupatiwa vitambulisho vya wastaafu vya kielektroniki.

Wito huo umetolewa na Mhasibu Mkuu kutoka Wizara ya Fedha, Jenipha Ntangeki, katika Ofisi ya Wizara ya Fedha, jijini Dodoma.

Jenipha ametoa kauli hiyo wakati wa shughuli ya kutoa vitambulisho vya kielektoniki kwa wastaafu kutoka Wilaya ya Dodoma Mjini ambao wamefunguliwa dirisha hilo linalotarajia kudumu kwa siku 10.

Katika taarifa iliyotolewa na Kitengo cha mawasiliano Serikali cha Wizara ya Fedha, mpango huo unalenga kuwatambua kikamilifu wastaafu na kuwarahisishia upatikanaji wa huduma bila usumbufu.

‘‘Vitambulisho hivi ni tofauti na vya zamani ambavyo vilikuwa katika karatasi kwani utunzaji wake ulikuwa changamoto ndio maana tumekuja na hivi vya kielektroniki ambavyo ni imara na vitawawezesha wastaafu wetu kupata huduma bila changamoto kwa kuwa taarifa zao zitasomeka kwa urahisi,’’ alisema Ntangeki.

Amesema vitambulisho hivyo vinafaa kwa matumizi rasmi hivyo wastaafu waliokabidhiwa wanaweza kuanza kuvitumia kupata huduma bila changamoto kutokana na kuwa ni vitambulisho vya kisasa na imara.

Akizungumza kwa niaba ya wastaafu waliofika Ofisi za Wizara ya Fedha kwa ajili ya kupata huduma hiyo, Andrew Makulukulu, amepongeza Serikali kwa kuendelea kuwajali hasa kwa kutambua shida wanazokutana nazo, hivyo wakaamua kuwapa huduma rahisi.

Wizara ya Fedha imeanzisha mpango huo wa ugawaji vitambulisho kwa wastaafu na wameanzia Wilaya ya Dodoma Mjini lakini wanaendelea   nchi nzima kwa wastaafu wanaolipwa mafao yao na Hazina katika mikoa yote, mapema Januari 2026 kwa ratiba itakayotangazwa kupitia vyombo vya habari.