Aliyekiri kuua kwa kudai kuvuta bangi, ahukumiwa kunyongwa

Arusha. Bingwa wa kupangua adhabu ya kifo anasa, ndivyo unaweza kuelezea namna Kinyota Kabwe aliyepangua adhabu ya kifo mara mbili, alivyotiwa hatiani tena na kuhukumiwa kifo kwa mara ya tatu kwa kosa lilelile alilolitenda miaka 12 iliyopita.

Mara ya kwanza alihukumiwa adhabu ya kifo mwaka 2017 lakini akakata rufaa na mahakama ikaamuru kesi isililizwe upya, na iliposikilizwa alitiwa hatiani tena na kuhukumiwa kifo akakata rufaa tena na kesi ikaamuriwa isikilizwe upya.

Baada ya kusikilizwa tena, Desemba15, 2025, Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, imemtia hatiani na kumuhukumu adhabu ya kifo na kuukataa utetezi wake kuwa alifanya mauaji hayo kutokana na wendawazimu uliosababishwa na kuvuta bangi kupita kiasi.

Ingawa Jaji amemtia hatiani mshtakiwa kwa kosa la mauaji ya kukusudia, nakala ya hukumu iliyowekwa katika tovuti haikutamka adhabu.

Ingawa kwa mujibu wa kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu, adhabu pekee kwa kosa hilo ni kunyongwa hadi kufa.

Kinyota alishtakiwa kwa kumuua Lucia Tekana, mchana kwa kumchoma na mkuki mara mbili kifuani na shingoni.

Hii ni mara ya tatu Mahakama Kuu kutoa hukumu hiyo dhidi ya Kinyota ambapo kwa mara ya kwanza alihukumiwa na Mahakama Kuu Tabora, Juni 5, 2017 na Jaji Julius Mallaba.

Kinyota alikata rufaa Mahakama ya Rufaa ambayo ilibatilisha hukumu hiyo na kuamuru shauri hilo lirudiwe kusikilizwa baada ya kubaini ilikosea kwa kushindwa kutoa maelezo sahihi ya wazee wa baraza, ambapo alikiri kuua kwa bahati mbaya kwa madai ya utetezi wa kuwa na wazimu (changamoto ya afya ya akili).

Baada ya uamuzi wa Mahakama ya Rufaa, Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma iliyorudia kusikiliza kesi hiyo kuanzia Julai 27, 2021 mbele ya Jaji mwingine, mshtakiwa huyo licha ya kujitetea kwa utetezi wa wazimu Mahakama hiyo ilimtia hatiani tena na kumuhukumu kunyongwa hadi kufa.

Kinyota alikata rufaa tena Mahakama ya Rufani, ambapo kesi hiyo iliamuriwa isikilizwe upya licha ya mshtakiwa kuibua suala la ukichaa katika rufaa zote Mahakama ilishughulikia muhtasari wa wazee wa baraza.

Katika kesi ya tatu ya sasa miongoni mwa mambo mengine, Mahakama Kuu iliagizwa kuzingatia hatua tano za kushughulikia wazimu katika kesi kama ilivyoelezwa katika kesi ya MT 81071 Yusuphu Haji dhidi ya Jamhuri katika rufaa ya jinai namba 168/2015.

Jaji Augustino Rwizile, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo ya mauaji namba 105/2014, ametoa hukumu hiyo Desemba 15, 2025.

Hukumu hiyo ya tatu baada ya kesi hiyo kuamriwa kusikilizwa kwa mara ya tatu mfululizo na Mahakama ya Rufaa, baada ya kufuta hukumu mbili za awali na kuamuru irudiwe, inakuwa miongoni mwa hukumu za kihistoria nchini ambapo mara zote mshtakiwa kutiwa hatiani.

Mahakama Kuu ilielezwa na ushahidi wa mashtaka ambao walimwona mshtakiwa akiwa na silaha hiyo na kuwafukuza baadhi yao baada ya tukio hilo.

Mahakama ilielezwa kuwa mshtakiwa alijaribu kujitetea kwa hoja ya wazimu, akidai alikuwa akitumia bangi na kuwa na historia ya ugonjwa wa akili. Hata hivyo ripoti za kitabibu toka kwa madaktari bingwa wa magonjwa ya akili katika Hospitali ya Mirembe zilithibitisha kuwa mshtakiwa alikuwa na akili timamu wakati wa kutenda kosa na alikuwa na uwezo wa kufuatilia kesi na kujitetea.

Jaji Rwizile amesema Mahakama haikuridhishwa na utetezi wa wazimu uliotolewa na mshtakiwa, akieleza kuwa hakuna ushahidi wa kutosha uliothibitisha kuwa alikuwa hana akili timamu wakati wa tukio.

Aidha, Mahakama ilibaini kuwa mshtakiwa alikumbuka kwa undani tukio la mauaji, jambo linalopingana na madai ya wazimu.

Mahakama hiyo ilisema upande wa mashtaka ulifanikiwa kuthibitisha vipengele vyote vya kosa la mauaji ikiwemo kifo cha marehemu, ushiriki wa moja kwa moja wa mshtakiwa na kuwepo kwa nia mbaya awali kwa kuzingatia aina ya silaha iliyotumika, sehemu za mwili zilizochomwa na tabia ya mshtakiwa kabla na baada ya tukio.

“Rekodi inaonyesha mshtakiwa alifanya mauaji mchana kweupe, yeye pia hapingi na alikiri mara kadhaa mbele ya shahidi wa tano, kwa ujumla hakuna shaka kwamba alitenda kosa hilo, hivyo amepatikana na hatia ya mauaji chini ya kifungu cha 196 cha Kanuni ya Adhabu.”

Mauaji hayo yalitokea Septemba 15, 2013 saa tisa alasiri katika Kijiji cha Muzye ndani ya Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.

Mahakama hiyo ilizingatia kesi ya MT 81071, ambapo Mahakama ya Rufaa ilisema inapohitajika kujitetea kwa utetezi wa wazimu pamoja na masuala mengine Mahakama inaagizwa kuahirisha kesi na kuamuru mshtakiwa azuiliwe katika hospitali ya magonjwa ya akili kwa uchunguzi wa kimatibabu.

Nyingine ni baada ya kupokea ripoti ya matibabu, kesi inaendelea kwa njia ya kawaida huku upande wa mashtaka ukiongoza ushahidi ili kuthibitisha shtaka lililofunguliwa na kisha kufunga kesi yake, kisha upande wa utetezi ukiwasilisha ushahidi dhidi ya shtaka ikiwa ni pamoja na ushahidi wa kimatibabu ili kuthibitisha wazimu wakati wa kutenda kitendo kinachodaiwa.   Mahakama kuamua kuhusu ushahidi huo kama umethibitishwa.

Nakala ya hukumu hiyo inaainisha kuwa mwanzoni mwa kesi hiyo, mambo yalionekana kuwa tofauti kidogo na ilikuwa ni maoni ya wakili wa utetezi kwamba mshtakiwa hakuweza kuwasiliana naye ipasavyo na kuwa hakuwa na uwezo wa kufuatilia kesi ipasavyo.

Wakati wa usikilizwaji wa kesi ya sasa upande wa Jamhuri uliwakilishwa na mawakili wawili huku mshtakiwa ambaye alikiri kumuua Lucia bila nia mbaya, akiwakilishwa na wakili mmoja.

Upande wa jamhuri ulikuwa na mashahidi watano ambao ni Maines Nyaumba, Oliva Omary, Nyaumba Ndigeze (mume wa marehemu) , Lazaro Munugwa na Dk Enock Changalawe.

 Shahidi wa kwanza (Maines) alisema kumwona mshtakiwa akiwa na mkuki siku hiyo ya tukio akimkimbilia mama yake na kumchoma mkuki na yeye alijeruhiwa kwa kuchomwa mara mbili begani.

Ushahidi huo uliungwa mkono na mashahidi wengine ambapo shahidi wa pili alikiri kukutana na mshtakiwa akiwa na mkuki na alipojaribu kumkimbiza mshtakiwa alijificha ndani ya nyumba.

Shahidi wa nne, alisema alimshuhudia mshtakiwa akiwa na mkuki wakati akifukuzwa na shahidi wa pili huku shahidi wa tatu akieleza kuwa hakuona mshtakiwa akimchoma mkewe kisu, lakini alionekana nyumbani kwao baada ya tukio hilo na kugundua kuwa mkewe alikuwa akivuja damu nyingi akiwa na majeraha ya kuchomwa kisu kifuani na shingoni.

Nakala hiyo ya hukumu inaeleza kuwa mshtakiwa alipopatikana na kesi ya kujibu, chini ya kifungu cha 232(3) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), alipelekwa katika Taasisi ya Isanga, Hospitali ya Mirembe.

Novemba 18, 2025, kesi ilianza tena, baada ya kupokea ripoti iliyowasilishwa mahakamani hapo, ulikuwa na maoni kwamba kesi inapaswa kuendelea tena kwani mshtakiwa alikuwa anafaa vya kutosha kutoa utetezi wake.

Shahidi wa tano ambaye alimchunguza mshtakiwa kwa awamu ya kwanza na ya pili aliwasilisha kielelezo cha ripoti ya magonjwa ya akili kilichopokelewa kama kielelezo cha kwanza cha Jamhuri.

Dk huyo alieleza kuwa Agosti 15, 2015 alimpokea na kumchunguza mshtakiwa kwa mara ya pili tangu alipofanya hivyo, hapo awali na kwa mujibu wake, alimchunguza kwa siku 18 kupitia uchunguzi na mahojiano.

Alisema kuwa mshtakiwa aliwasiliana vyema na wagonjwa wengine na tabia yake kwa wengine ilikuwa ya kawaida, aliishi vizuri na watu, wauguzi na maagizo ya daktari wake aliyafuata, alikula na kulala vizuri na alipomuhoji alikuwa akijibu vizuri hakuwa na shida.

Alisema angekuwa na tatizo la afya ya akili, asingeweza kukaa vizuri, angekuwa na matatizo ya usingizi, angeshindwa kula vizuri, angezungumza kupita kiasi na kuwa na tabia isiyo ya kawaida na kuhitimisha mshtakiwa hakuwa na ugonjwa wowote wa afya ya akili.

Katika utetezi mshtakiwa alikuwa na shahidi mwingine mmoja, Isack Kagoma.

Akijitetea mahakamani hapo mshtakiwa huyo alieleza kuoana na Theodora Theonisti mwaka 1994 na walibahatika kuwa na watoto saba na kuwa siku ya tukio kulitokea mauaji na alienda kwenye mazishi siku hiyo, na kusaidia kuchimba kaburi.

Alisema alipotoka kaburini alipokuwa akichimba, alihisi maumivu ya kichwa hakuwa anajisikia vizuri hivyo akaamua kurudi nyumbani kwani alihisi kizunguzungu pia, na baadaye mkewe na wanaye walirejea nyumbani na akapewa dawa za kutuliza maumivu.

Alisema kuwa baadaye alisikia watoto nje wakirushiana matusi, akakasirika na kukerwa na kuamua kutoka nje na kufungua mlango na watoto walipomsikia, walikimbia na alipokuwa akirudi, alikanyaga baiskeli na kuanza kutokwa na damu.

Alieleza kuwa alipoteza fahamu na kuanza kupiga kelele na kuwa alikuwa akivuta bangi tangu mwaka 1996 hadi siku ya tukio ambapo baada ya kuvuta, Lucia na watoto wake walifika eneo hilo na kumgusa mgongoni ambapo alikasirika na kumrushia baiskeli.

Alisema Lucia alianza kukimbia, yeye alikimbilia ndani ya nyumba ambapo aliona fimbo kubwa kama mpini wa mkuki  aliichukua na kumfuata mwanamke huyo na kumchoma, na kudai alikuwa akipata ukichaa kwa sababu ya kutumia bangi na aliwahi kulazwa siku 14 na alikuwa akitumia dawa kuanzia 2011 hadi 2012 alipoacha.

Licha ya kukiri kumuua Lucia, alisema kuwa hakuwa na mgogoro naye wala jamaa zake, kilichotokea kilitokana na matumizi ya bangi.

Shahidi wake ambaye ni Ofisa Kliniki katika Hospitali ya Marumba, alisema  Machi 3,2021 mshtakiwa alipelekwa hospitalini hapo akiwa amefungwa kwa kamba mikono na miguu, alilazwa na uchunguzi ulionyesha alitumia pombe na dawa za kulevya (bila kuzitaja ni aina gani)na baada ya kuruhusiwa hakuwahi kurudi tena hospitali.