Dar es Salaam. Siku zinaendelea kuyoyoma, huku ukimya ukitawala kuhusu hatima ya Chama cha ACT – Wazalendo, kuingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK).
Hali iko hivyo, wakati Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameacha nafasi nne za uwaziri zinazopaswa kujazwa na ACT – Wazalendo, chama kilichoshika nafasi ya pili kwa kura za urais na idadi ya majimbo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Wizara hizo ni Utalii na Mambo ya Kale, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Wizara ya Afya na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.
Katika uchaguzi huo, ulioshindaniwa na wagombea 11 wa kiti cha urais, Dk Mwinyi wa CCM alishinda kwa kura 448,892 sawa na asilimia 74.8 akifuatiwa na Othman Masoud wa ACT – Wazalendo, aliyepata kura 139,399 sawa na asilimia 23.22.
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, toleo la mwaka 2010, inaeleza ili kuundwa kwa SUK, chama kinachoshinda kitashirikiana na chama chochote cha upinzani kilichoshika nafasi ya pili kwa wingi wa majimbo katika Baraza la Wawakilishi.
Pia, Katiba hiyo iliyofanyiwa marekibisho mwaka 2010, ibara ya 39 (3), kifungu kidogo (1), inaeleza Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, atateuliwa iwapo chama chake kitapata asilimia 10 au zaidi ya kura za urais.
Aidha, ACT – Wazalendo inalazimika kufanya uamuzi wa kuingia SUK,ndani ya siku 90 zilizowekwa kikatiba na muda huo ukipita, Rais Mwinyi anaweza kujaza nafasi hizo kwa kadri itakavyompendeza.
Ingawa hadi sasa kati ya siku 90 zilizotolewa kuhusu ACT – Wazalendo kujiunga na SUK, zimebaki 48, hakuna kiongozi yeyote wa chama hicho cha upinzani aliyetoa kauli au mwelekeo iwapo wataingia SUK au la.
Ukimya huo unaendelea licha kikao cha kamati ya uongozi kilichoketi Novemba 25, 2025, kujadili mwenendo wa uchaguzi iliofanyika Oktoba 29 na tathimini ya hali ya kisiasa nchini.
Kikao hicho kilichofanyika ofisi za ACT -Wazalendo Vuga, Unguja kilichojadili suala la SUK, lakini hakuna kiongozi wala mjumbe aliyekuwa tayari kuzungumza na wanahabari kueleza kilichojiri.
Hata hivyo, Novemba 13, 2025 Othman alibainisha kwamba ACT – Wazalendo imeandikiwa barua na Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Zena Said inayowataka kupeleka jina la anayependekezwa kuteuliwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Kwa mujibu wa Othman, ACT – Wazalendo haikupeleka jina hilo kwa sanani hairidhiki na mazingira ya siasa visiwani humo, suala linazungumzia pia na viongozi wengine wa chama hicho.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumanne, Desemba 16,2025 Makamu Mwenyekiti wa ACT – Wazalendo (Bara), Isihaka Mchinjita amesema tatizo ni kwamna uchaguzi wa Zanzibar hauonyeshi nani ameshinda na nani ameshindwa.
“Kabla ya kuamua kuingia kwenye SUK au kutoingia, kuna matatizo yanayoendelea na yanapaswa kutatuliwa kwanza,” amesema na kuongeza;
“Hii imefanywa kuwa utamaduni, mnakwenda kwenye uchaguzi unavurugwa na baadaye mnapeana nafasi, sasa hapa hatujengi nchi. Kuingia SUK ipo kikatiba, ila malengo gani ya kusimamia kwenye Serikali ya kitaifa ni utashi wa kisiasa,” amesema.
Mchinjita amefafanua kuwa, lazima matatizo yanayohusu uchaguzi yatatuliwe kwanza na kuwekewa misingi, ndipo wafanye uamuzi.
Kuhusu hatua walizofikia za mazungumzo na CCM Zanzibar, Mchinjita ameeleza kuwa zipo juhudi zinazofanyika ndani ya ACT – Wazalendo katika kurejesha malengo ya SUK.
Wakati Mchinjita akieleza hayo, kiongozi mwingine wa ACT – Wazalendo, (jina lake limehifadhiwa) ameidokeza Mwananchi kuwa hatima ya chama hicho ndani ya SUK huenda ikajulikana Januari, 2026.
“Januari ndio tutafanya kikao na moja ya agenda itakuwa SUK,” amedokeza.
Akilizungumzia hali hiyo, mchambuzi wa siasa, Makame Ali Issa amesema siku 90 zilizowekwa hazitamalizika kabla ya ACT – Wazalendo kuwasilisha jina la mwanachama atakayeteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
“Wanachokifanya hivi sasa wanatingisha kibiriti, wasipopeleka jina chama chao kitapata athari kuliko iliyotokea kwa CUF. Wasipopeleka jina watakuwa wanajitengenezea kaburi lao.”
“Katika siasa za siasa unatakiwa kupigana ukiwa ndani ya Serikali hata kama mguu mmoja upo ndani na mwingine nje. Usikubali kupambana nje wakati fursa ipo ya kuunda Serikali pamoja na chama tawala,” ameeleza Issa.
Amefafanua kuwa mwaka 2020, ACT -Wazalendo, kilikuwa na wawakilishi wachache, hivi sasa wamefikia 10, jambo ambalo ni maendeleo makubwa ndani ya chama hicho, hivyo wana kila sababu ya kuingia SUK.
“Kama kweli wana dhamira njema, waingie SUK hata kama wana kidogo, waingie ili kupata kikubwa. Wakisusia, wakumbuke kilichowapata CUF mwaka 2016,” amesema.
Machi 20, 2016, CUF ikiongozwa na aliyekuwa katibu mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad (marehemu), ilisusia uchaguzi wa marudio, ikidai ni batili, baada ya ule wa Oktoba 2015 uliofutwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).
Hata hivyo, uamuzi huo ulionekana kujutiwa na viongozi wa CUF wakati huo, ambao hivi sasa wapo ACT – Wazalendo, wakisema ndio uliotoa mwanya wa kupitishwa sheria mbalimbali ikiwemo ya kura ya mapema wanayodsema si rafiki.
Mchambuzi mwingine, Seif Nassor amesema ACT – Wazalendo ndio chama pekee chenye uwezo wa kuunda Serikali ya kitaifa lakini bado kinasuasua.
“Moja ya matakwa yao ni kutaka majimbo yao wanayoyadai, wanaweza kuyapeleka madai yao mahakamani, lakini kwa hali yoyote ni muhimu waingie SUK,” amesema.
Nassor naye amesema endapo ACT – Wazalendo itaendelea na msimamo wa kutoingia kutakuwa na athari kama ilivyokuwa kwa CUF, iliyosusia uchaguzi wa marudio.