SIMBA inakaribia kumaliza mchakato wa kumpata kocha mpya wa kuiongoza timu hiyo baada ya Desemba 2, 2025 kuachana na Dimitar Pantev kwa makubaliano ya pande mbili.
Katika mchakato huo wa kusaka kocha, Simba ilikuwa kwenye mazungumzo na Mohamed Sahli raia wa Tunisia ambaye Mwanaspoti linafahamu upande wa bodi ya wakurugenzi ya klabu hiyo ilimtafuta wakitaka kujua utayari wake wa kuifundisha timu hiyo na masilahi kwa jumla.
Kocha huyo ambaye amewahi kuifundisha US Monastir ya Tunisia, kwa sasa hana timu tangu Julai 22, 2025 alipoachana na Club Africain ya hukohuko Tunisia.
Mtoa taarifa kutoka Simba, aliliambia Mwanaspoti mazungumzo na Sahli yamekwama kutokana na masilahi makubwa aliyohitaji kocha huyo tofauti na bajeti iliyowekwa kipindi hiki ambacho klabu inapambana kubana matumizi.
“Kulikuwa na hayo mazungumzo, lakini ni kama imeshindikana kwa sababu ya masilahi makubwa ya kocha tofauti na bajeti ya klabu iliyopangwa,” amesema mtoa taarifa huyo na kuongeza;
“Kwa sasa uongozi unaendelea na mchakato kuhakikisha kocha anapatikana kwa haraka ili pindi timu ikirudi mazoezini mwisho wa mwezi huu basi kila kitu kiwe kimekamilika.”
Mwanaspoti linafahamu, Simba inahitaji kocha ambaye hana gharama kubwa na angalau akubali kulipwa Dola 15,000 (sawa na Sh37 milioni) kwa mwezi.
Hesabu za Simba kwa Sahli zilikuwa ni kumpata kocha huyo ambaye mbali na ubora wa mbinu zake, pia kuifahamu kwake vizuri Esperance ambayo watacheza nayo Januari mwakani katika mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika Kundi D ugenini na nyumbani kutokana na kuwahi kufundisha soka nchini Tunisia inapotokea klabu hiyo.
Hata hivyo, Simba iliweka mtego, ikimkosa Sahli, basi ibaki anga hizohizo za Ukanda wa Afrika Kaskazini kusaka kocha atakayekuwa anafahamu mbinu za timu za Waarabu iwe rahisi kutoboa watakapokutana na wapinzani wao hao.
YAMGEUKIA GAMONDI, KOCHA WA AZIZ KI
Kushindwana na Sahli, Simba imerudisha majeshi kwa Miguel Gamondi ambaye kwa sasa ni Kocha Mkuu wa Singida Black Stars, pia ni Kaimu Kocha Mkuu wa Taifa Stars akiwa na kikosi hicho kinachojiandaa na fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2025) zitakazoanza wikiendi hii nchini Morocco.
Mbali na Gamondi, Simba inatajwa kumpigia hesabu kocha wa zamani wa Burkina Faso aliyekuwa akimnoa Stephane Aziz KI, Hubert Velud.
Kwa Gamondi, Simba inamlenga kocha huyo kutokana na kulifahamu vizuri soka la Tanzania, hali ambayo kama akitua hapo, haitamchukua muda mrefu kuzoeana na wachezaji, pia ana uwezo mkubwa wa kuiongoza timu katika mashindano ya kimataifa akifanya hivyo alipokuwa Yanga ilipocheza robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2023-2024, kisha 2024-2025 akaifikisha makundi ya michuano hiyo, akasepa kabla hatua hiyo haijaanza. Msimu huu ameiwezesha Singida Black Stars kucheza makundi Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza.
“Gamondi anaifahamu vizuri Simba na wachezaji wengi waliopo, hivyo itakuwa rahisi kwake akipatikana kuja kuifundisha,” kimesema chanzo na kuongeza.
“Kwa sasa Simba inahitaji kocha wa haraka ambaye ataiongoza timu katika maandalizi kuelekea mechi zijazo za CAF, hivyo Gamondi ni mtu sahihi akipatikana.
“Hata yeye mwenyewe ameonyesha nia ya kuja Simba, hivyo anasubiriwa akimaliza majukumu ya kuiongoza Taifa Stars kisha amalizane na waajiri wake wa Singida ili atue kwetu.”
Kuhusu Velud, mtoa taarifa huyo amesema naye anapigiwa hesabu kama mambo yakikwama kwa Gamondi kwani kocha huyo raia wa Ufaransa, amefundisha soka Afrika Kaskazini katika nchi za Tunisia akiinoa Étoile du Sahel na Stade Tunisien.
Pia amekaa Algeria akifundisha timu za ES Sétif, USM Alger, CS Constantine, JS Kabylie na MC Oranna. Akapita Morocco katika timu za Hassania Agadir, Difaâ Hassani El Jadidi na AS FAR.
“Tupo mwishoni, jambo ambalo limenivutia ni makocha waliosalia ni wakubwa ambao tukimpata mmoja tutabadilika,” amesema bosi mmoja wa Simba.
“Kuna mambo tunataka kuyazingatia sana hapa kwenye maamuzi ya mwisho, hatutaki kuchukua kocha mwenye gharama kubwa sana, kuna kocha mnamchukua anawapa mambo magumu sana, tunataka kupunguza matumizi ya fedha.”
Ukiacha hayo kuna masharti ambayo Simba itayataka kocha mpya akubaliane nayo likiwemo suala la wasaidizi wake ambapo Wekundu hao wanataka mkufunzi huyo aje na wasaidizi wasiozidi watatu, huku Seleman Matola awe ndani ya jopo hilo.
“Tunataka aje na wasaidizi wake lakini akija na watu wasizidi watatu, kama msaidizi wake wa kwanza ni sawa lakini wa pili atamkuta hapa, unajua watu hawatuelewi, mnaona alivyoondoka Fadlu (Davids), vipi benchi zima lingekuwa amekuja nalo na maana tusingekuwa na kocha, alivyokuwepo Matola ilitupa nafuu.”
Hadi kufikia hapa, Mwanaspoti linafahamu kuwa, mchakato huo ulikuwa na orodha ndefu ya makocha akiwamo Steve Barker wa Stellenbosch ya Afrika Kusini ingawa inaelezwa amehitaji fedha nyingi kwenye malipo yake, wakaachana naye japo walimuhitaji sana.
