MOSHI.
SERIKALI imetenga zaidi ya shilingi Bilioni 63 kwa ajili ya matengenezo na ukarabati wa miundombinu ya barabara mbalimbali ndani ya Mkoa wa Kilimanjaro kwa mwaka wa fedha 2025/2026, hatua inayolenga kuboresha usafiri na kuchochea shughuli za kiuchumi katika mkoa huo.
Akizungumza wakati wa kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Kilimanjaro kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa ya Moshi, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, alisema fedha hizo zitatumika kuboresha barabara pamoja na madaraja katika maeneo mbalimbali ya mkoa.
Alifafanua kuwa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Kilimanjaro umetengewa zaidi ya shilingi bilioni 36.76, huku Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ukitengewa zaidi ya shilingi bilioni 26.77 kwa ajili ya matengenezo na ukarabati wa miundombinu hiyo.
Babu alisisitiza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unapaswa kufanyika kwa kuzingatia viwango na ubora unaotakiwa ili kuhakikisha thamani halisi ya fedha zilizotolewa na Serikali inaonekana kwa wananchi.


.jpeg)
.jpeg)