Dar es Salaam. Wakati Serikali ikikamata madumu 23,755 ya mafuta ya kula yaliyoingizwa nchini kinyume na taratibu, wananchi wamepaza sauti zao wakitaka watumishi waliopo bandari ndogo ya Kunduchi, kuangaliwa kwa kile wanachodai wamekuwa wakikwamisha biashara.
Kukwamisha huduma huko kumetajwa kuchangiwa na watumishi kuchagua watu wa kufanya nao biashara, hali inayofanya wengine kukwepa kushusha mizigo katika bandari hiyo na kuwakosesha kazi za kufanya.
Wametoa malalamiko hayo wakati Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda, alipofanya ziara katika Bandari ya Kunduchi jijini Dar es Salaam kukagua utendaji kazi, baada ya shehena ya mafuta yaliyoingizwa hapo kwa magendo kubainika.
Akitoa kero yake, Salum Athuman amesema hawana imani na watumishi wa TRA waliopo katika bandari hiyo, akidai wanawaua kwa njaa.
Amesema urasimu uliopo bandarini hapo umefanya wafanyabiashara wengi kushusha mizigo yao maeneo mengine, jambo linalofanya ofisi hiyo kufanya kazi mara chache, hata mara moja kwa mwezi.
“Tangu Novemba 27 walipofanya kazi, walikaa hadi Desemba 7 ndipo tukafanya kazi tena. Hadi tunapoongea leo, hakuna kazi yoyote iliyofanyika. Watu tunategemea kazi hii, tuna watu wanaohitaji kula, na hapa ndiyo sehemu ya kupata fedha, lakini hakuna kazi,” amesema.
“Ukiwauliza wafanyabiashara kwa nini hawashushi mizigo hapa, watakwambia watumishi hawa wana watu wao. Hii ni mbaya. Bandari nzima wanaoshusha mizigo wako wawili, si haki. Walikuja wengine kufanya kazi wamekimbia. Ifike wakati muangalie hili, tumechoka, tutakufa njaa,” amesema.
Alimtaka kamishna kuongea na watumishi wake ili wabadilike na wawe tayari kufanya kazi na kila mfanyabiashara anayetaka kushusha mzigo katika bandari hiyo, au waondolewe na kuwekwa wafanyakazi wapya wanaojua kufanya kazi na kila mtu.
Hassan Mbunda ameunga mkono hoja hiyo, akisema kukosekana kwa biashara katika bandari hiyo kumesababisha ofisi hizo kufungwa siku nyingi za kazi, akitolea mfano Agosti kuwa haikufanya kazi hata siku moja.
“Mwezi wa Agosti haikufanya kazi hata siku moja, Septemba ilifanya kazi siku mbili, Oktoba ilifanya kazi siku moja. Angalieni hili, ilhali kuna watu wanalipwa mishahara kila siku,” amesema.
Mohammed Omary ametaka TRA kuangalia namna ya kulinda mali za watu zinapokamatwa, akidai mara nyingi mizigo imekuwa ikirudishwa ikiwa pungufu.
“Mali zikikamatwa hazirudi kamili. Hatufahamu kuna shida gani; kama zilikuwa madumu 500, hazirudi kamili. Au ukiomba namba ya malipo unaambiwa utoe hela. Kamishna, unalijua suala hili?” amehoji.
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Yusuph Mwenda, akizungumza mara baada ya kufanya ziara katika Bandari ya Kunduchi jijini Dar es Salaam kukagua utendaji kazi
Akijibu malalamiko hayo, Mwenda amewatoa hofu wafanyabiashara akisema ofisi hiyo ni kwa ajili ya Watanzania wote, si kwa ajili ya wachache.
“Kwa sababu mmeeleza hili, nalichukua na nitalifanyia kazi. Nitakutana na wafanyabiashara wote wanaoleta mizigo yao, tuwape elimu ya kodi na tusikilize matatizo yao, tuone namna tunavyoweza kuwawezesha walete mizigo yao bila kutumia magendo,” amesema.
Akizungumzia mafuta yaliyokamatwa, Mwenda amesema kati ya madumu 23,755 ya mafuta ya kupikia yaliyoingizwa kinyume na taratibu kupitia Bandari ya Kunduchi, madumu 5,000 pekee ndiyo yaliyokuwa na nyaraka.
Amesema baada ya kukagua mzigo huo katika eneo la Magofu, Ubungo, ulikokuwa umefichwa, aliwataka wananchi kufuata taratibu wanapotaka kuingiza bidhaa, kwani kutokufanya hivyo kunaathiri uchumi.
“Bidhaa za magendo zimekuwa tishio kwa uchumi wa nchi, kwa kuwa zinapunguza mapato ya Serikali na kudhoofisha ukuaji wa viwanda vya ndani,” amesema.
Mbali na athari za kiuchumi, amesema bidhaa hizo zinaweza pia kuhatarisha afya za walaji, hivyo ni wajibu wa kila mmoja kushiriki katika kuzizuia.
Akieleza namna mizigo inavyopaswa kuingia nchini, Kamishna wa Forodha wa TRA, Juma Hassan, amesema ipo mizigo ya aina mbili inayoingia nchini; ipo inayohitaji kibali kama vyakula na madawa, na ipo isiyohitaji vibali, isipokuwa kulipa kodi, akitolea mfano nguo zinazotoka Zanzibar.
“Hivyo ni lazima zifuatwe taratibu ikiwemo kujaza fomu na kupita katika bandari iliyo rasmi; kinyume cha hapo, zinakuwa zimekiuka sheria na kuhatarisha usalama wa nchi,” amesema.
Kamishna wa Upelelezi wa Kodi wa TRA, Hashim Mgoda, amesema mzigo wa mafuta ulikamatwa baada ya wasamaria wema kutoa taarifa kuhusu uingizwaji wake bila kufuata taratibu.
“Tulipofuatilia tulibaini haukulipiwa kodi. Ilikuwa ni doria ya siku moja, na ikibainika hawakufuata taratibu, tutaukamatia na kuutaifisha mzigo huo. Pia watalipa faini ya asilimia 50 ya kodi iliyopaswa kulipwa,” amesema.
