Mahakama Kuu Yakataa Pingamizi, Kesi ya Uchaguzi Kigoma Mjini Kuendelea

Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Ndogo ya Kigoma, imeamua kuendelea na Shauri la Uchaguzi Namba 28949 la Mwaka 2025, baada ya kutupilia mbali pingamizi la awali lililowasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Clayton Revocatus Chipando, maarufu kama Baba Levo.

Uamuzi huo umetolewa leo Desemba 16, 2025, na Mahakama ikiongozwa na Mheshimiwa Jaji Projestus Khayoza, ambaye amekubaliana na hoja za mawakili wa walalamikaji kwamba shauri hilo lina msingi wa kisheria na linapaswa kuendelea kusikilizwa kwa ushahidi wa msingi.

Walalamikaji katika shauri hilo ni Johary K. Kabourou, Loum H. Mwitu, Pendo D. Kombolela na Luma H. Akilimali, waliokuwa wakiongozwa na Wakili John Seka. Kupitia mawakili wao, walalamikaji waliomba Mahakama itupilie mbali pingamizi la awali, wakisisitiza kuwa hatua hiyo ilikuwa ya mapema kwa kuwa ushahidi haukuwa umefikishwa kikamilifu mbele ya Mahakama.

Hata hivyo, walalamikaji pia walikuwa wameibua hoja kuhusu mapungufu katika hati ya shauri, hususan katika Aya ya Uthibitisho, pamoja na kuomba msamaha wa kulipa gharama za kesi. Baada ya kuyapitia madai hayo, Mahakama imeeleza kuwa hoja hizo hazina msingi wa kisheria.

Katika uamuzi wake, Mahakama Kuu imebainisha kuwa shauri hilo limekidhi matakwa ya Sheria ya Uchaguzi pamoja na Kanuni za Mashauri ya Uchaguzi, hivyo kuruhusu kesi ya Uchaguzi wa Jimbo la Kigoma Mjini kuendelea kusikilizwa kwa ushahidi wa msingi.

Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni muhimu katika kuimarisha uwazi, haki na imani ya wananchi katika mfumo wa utoaji haki, hususan kwenye mashauri yanayohusu uchaguzi nchini.