TIMU ya KVZ inayofundishwa na Malale Hamsini, imepokea kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Zanzibar, Mlandege, katika mechi ya ligi hiyo iliyochezwa jana Desemba 16, 2025 kwenye Uwanja wa Mao A, uliopo Mjini Unguja.
Bao lililofungwa na Yussuf Suleiman dakika ya sita, ndilo lililoishusha KVZ kutoka nafasi ya pili hadi ya nne kwenye msimamo wa ZPL.
Mara ya mwisho timu hizo zilipokutana msimu wa 2024-2025, Mlandege ililala bao 1-0, hivyo kipigo hicho ni kama kulipa kisasi.
Malale ambaye Desemba 15, 2025 alitambulishwa ndani ya KVZ, mechi yake ya kwanza kuiongoza timu hiyo ni dhidi ya Mlandege na ameanza na kichapo hicho.
Hii ni mechi ya tatu mfululizo KVZ inapoteza katika ligi msimu huu ambapo mara ya mwisho kushinda ilikuwa Novemba 23, 2025 ilipoichapa New Stone Town mabao 4-1.
Baada ya hapo, imepoteza mechi tatu na sare moja, matokeo yakiwa hivi; Fufuni 1-0 KVZ (Novemba 26), Uhamiaji 1-1 KVZ (Desemba 3), Zimamoto 2-1 KVZ (Desemba 13) na Mlandege 1-0 KVZ (Desemba 16).
KVZ imeendelea kusalia na pointi 23 baada ya kucheza mechi 13, ikishinda saba, sare mbili na kupoteza nne, ikifunga mabao 19 na kuruhusu 13 ikiwa nafasi ya nne kwenye msimamo.
Matokeo ya mechi zingine zilizochezwa jana, Fufuni iliichapa Mwembe Makumbi City bao 1-0 kwenye Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba, huku Polisi Kipanga ikiifunga Polisi bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mao B, Unguja.