Dar es Salaam. Katibu Mkuu Kiongozi, Dk Moses Kusiluka amewataka maofisa habari wa Serikali, kujipanga kukabiliana na matumizi hasi ya teknolojia ya habari na mawasiliano, ukiwemo upotoshwaji unaofanyika dhidi ya nchi.
Balozi Kusiluka amesema Tanzania imeshuhudia namna teknolojia ya habari na mawasiliano inavyoweza kutumiwa na maadui kuhataratisha usalama wa nchi.
Ametoa kauli hiyo leo, Jumatano Desemba 17, 2025 katika kikao kazi cha kitaifa cha siku mbili cha Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu na maofisa habari wa Serikali kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
“Najua tupo (maofisa habari) wengi zaidi ya 800, lakini leo tupo 500, ila tunashangaa tunapigana kutoka wapi? Tunaambiwa sisi ni jeshi la Serikali, inakuwaje wakati mwingine Serikali inashambuliwa na sisi tumekaa.”
“Naamini hakuna jeshi kubwa kama hili, tumekuja hapa kukumbushana inawezekana hatujitambui au tunafanya kazi vipande vipande. Tumeshuhudia yakitokea, kila mtu anajiuliza watalaamu wetu wako wapi,” amehoji.
Balozi Kusiluka amebainisha kuwa hivi sasa mawasiliano yametawaliwa na matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano, ambayo ni fursa endapo itatumika vizuri, na hatari kubwa ikitumika vibaya.
Hata hivyo, Dk Kusiluka amesema hawajachelewa kwa sababu Tanzania bado ni imara, na Taifa litajengwa na Watanzania wenyewe, akiwataka kuonyesha umahiri katika sekta hiyo.
“, Tunaposema nyinyi ndio tegemeo la Serikali, maana yake hakuna mwingine zaidi yenu,” ameeleza Dk Kusiluka.
Dk Kusiluka amesema maofisa habari bado hawajafanya vizuri katika eneo la kuwaunganisha wananchi na Serikali, hasa kutoa taarifa za sahihi za kazi, sambamba na kutoa ufafanuzi wa haraka zinapotokea taarifa za upotoshaji.
“Hatujafanya vizuri katika kukabiliana na mashambulizi ya wasioitakia mema nchi yetu. Tutumie teknolojia ya habari inayoendana na wakati, mazingira ili wananchi wapate taarifa sahihi,” amesema.
“Kumbukeni mwajiri wenu ni Serikali na taasisi zake, nisisitize tupo hapa ndani, mwajiri wetu ni Serikali. Hakuna mfanyakazi wa kawaida, atakayefanya kazi kinyume na mwajiri wake,” ameeleza.
Kuhusu kikao hicho, Dk Kusiluka amesema kitaimarisha utendaji kazi wa maofisa hao, sambamba na kubadilisha fikra ya namna ya kufikiri ili kutimiza majukumu yao kwa ufanisi.
Awali, Mshauri wa Rais wa Habari na Mawasiliano, Tido Mhando amesema Rais Samia Suluhu Hassan anataka habari sahihi na wa kulitekeleza hilo ni maofisa habari hao, waliopo katika maeneo mbalimbali nchini.
“Matarajio yetu popote mtakapokuwepo, mtahakikisha mnatupatia habari sahihi zitakatoa mwanga mzuri wa kutoa sura sahihi nchini na duniani,” amesema,
“Sasa hivi dunia ina mambo mengi, teknolojia imeshachukua nafasi yake, nyinyi ndio wakati wenu wa kutupatia yanayoendelea katika maeneo hayo,” amesema Mhando ambaye ni mwanahabari mkongwe.
