MKUTANO WA COP30 WAILTETEA NEEMA TANZANIA, YAPATA MAMILIONI YA DOLA

…………..

Tanzania inatarajia kunufaika
na Dola za Marekani milioni 447.12 na Euro 500,000
kutokana
na ushiriki wake katika Mkutano wa 30 wa
Nchi Wanachama wa Mkataba Mabadiliko ya Tabianchi (COP30) uliofanyika Belem,
Brazil hivi karibuni.

Pia, Tanzania itapata kiasi cha Dola milioni 5 hadi 20
kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kukabiliana na mabadiliko
ya tabianchi, kupitia Mfuko wa Upotevu na Hasara.

Hayo yamebainishwa na Naibu
Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Prof. Peter Msoffe leo Desemba
17, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa Wadau wa Kupokea
Taarifa ya Ushiriki wa Tanzania katika Mkutano COP 30, kwa niaba ya Katibu Mkuu
Ofisi ya Makamu Wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja.  

Prof. Msoffe ameeleza kuwa lengo
la mkutano huo kuangaza na kujadili fursa mbalimbali katika kuuisaidia jamii katika
kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia miradi ya mazingira
inayotekelezwa na Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na wadau.

Aliongeza kuwa Tanzania
imeendelea kuimarisha hadhi yake kimataifa kupitia nafasi yake kama Mwenyekiti wa Kundi la Majadiliano la Afrika
(AGN) ambapo
imewezesha
kujadiliwa na kukubalika kwa ajenda ya Nishati Safi ya kupikia, kukubalika kwa
hoja ya upatikanaji wa umeme wa bei nafuu kwa watu wote (Mission 300).

“Tumeona hatua nzuri
kupitia mkutano huo kama vile Tanzania kufikia maamuzi ya nchi wanachama,
kuwezesha Ofisi ya Kanda ya Santiago Network on Loss and Damage ambayo
itafunguliwa Dar es Salaam. Tukumbuke hii ni nafasi ya nishati safi ya kupikia
kimataifa ni ajenda inayopewa nguvu na uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu
Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.

Kwa upande wa Biashara
ya Kaboni, Prof. Msoffe alibainisha kuwa imefanikiwa kupata ufadhili wa misitu
ya kitropiki kupitia Mfuko wa Tropical Forest Forever Facility (TFFF).

Ili kuunga mkono juhudi
za Serikali katika kuimarisha usimamizi wa biashara ya kaboni, alitoan wito kwa
sekta binafsi kuongeza ushiriki kwenye masoko ya biashara hiyo kwani ina uwezo
mkubwa wa ubunifu.

Halikadhalika,
aliwaomba wadau hao kuendelea kuandaa miradi ya kimkakati itakayoweza
kufadhiliwa chini ya utekelezaji wa Dira 2050 na maamuzi ya COP30, hususan miradi
ya uhimilivu, mifumo ya tahadhari mapema, nishati safi ya kupikia na
teknolojia, biashara ya kaboni, uhufadhi na usimamizi wa misitu, maji, kilimo
na taka.

Kwa upande wake Mshauri
wa Rais katika masuala ya Mabadiliko ya Tabianchi na Mazingira Dkt. Richard
Muyungi alisema kuwa miongoni mwa agenda kuu za katika mkutano huo Tanzania
iliwasilisha ni pamoja na kupata fedha za mabadikliko ya tabianchi.

Dkt. Muyungi ambaye ni
Mwenyekiti wa AGN alisema nchi zilizoendelea zinawajibika kutimiza ahadi zao za
kutoa fedha na sio mikopo hizo kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.