Msuva, Samatta wainogesha Stars kambini

KAMBI ya timu ya taifa, Taifa Stars iliyopo Misri imeizidi kunoga baada ya kuwasili kwa mastaa wakubwa wa timu hiyo inayojiandaa kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 inayoanza Jumapili.

Simon Msuva anayekipiga Iraq ametua jana Jumatano, akiwa ametanguliwa na Novatus Dismas na nahodha Mbwana Samatta anayekipiga katika klabu ya Le Havre ya Ligue 1 huko Ufaransa, Tarryn Allarakhia na Alphonce Mabula waliokuwa na jukumu katika klabu wanazotumikia huko England na Azerbaijan mtawalia.

Stars imepangwa Kundi C sambamba na Uganda The Cranes, Nigeria (Green Eagles) na Tunisia na itaanza mechi zake Desemba 23 dhidi ya Nigeria kabla ya kuvaana na Uganda Desemba 27 kisha kumaliza mechi za kundi hilo na Tunisia siku ya Desemba 30.

Hii ni mara ya nne kwa Tanzania kushiriki fainali hizo baada ya zile za 1980 kule Nigeria, 2019 zilizofanyikia Misri na fainali zilizopita za 2023 Ivory Coast na mara zote haijawahi kutoka na ushindi katika hatua ya makundi achilia mbali kuvuka kwenda hatua inayofuata ya michuano hiyo.

Safari hii, Stars ipo chini ya kocha Miguel Gamondi ambaye mwanzo kabla ya timu kuondoka alifichua mipango aliyonayo kwa timu hiyo na kulizungumzia kundi hilo linaloonekana kuwa gumu kutokana na kuwa na vigogo Tunisia na Nigeria, mbali na majirani zao wa Uganda wanaoisumbua.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Timu hiyo kwa sasa imepiga kambi huku Misri ikiwa na kundi la wachezaji wengi wanaocheza Ligi Kuu Bara ambao imesimama tangu Desemba 7 na Gamondi alinukuliwa akisema mapema dhamira aliyonayo katika fainali hizo zinazofanyika Morocco ni kuleta ‘kitu cha kipekee’ kwa Watanzania.

Kocha huyo raia wa Argentina alisema; “Tunahitaji kufanya jambo muhimu kwa taswira ya soka la Tanzania na kuthamini juhudi kubwa zinazofanywa na wachezaji pamoja na taifa kwa ujumla. Hili ni shindano kubwa, lakini hakuna kisichowezekana. Tunapaswa kuota ndoto na kuamini.”

Kuhusu kikosi hicho, Gamondi alisema “Tumeunda mchanganyiko wa vijana wanaojifunza kutoka kwa wazoefu na wazoefu wanaopata nguvu mpya kutoka kwa hamasa ya vijana. Kambi hii ni maabara ya kujifunza, si kwa wachezaji pekee bali kwa kila anayehusika.”

Akizungumzia fursa ya kuiongoza Tanzania katika AFCON, Gamondi alisema:

“Ninaheshimika sana kuwakilisha Tanzania na beji ya taifa ina maana kubwa zaidi ya alama, inaakisi imani ya mamilioni ya watu. Nchi hii imekuwa sehemu ya moyo wangu,” alisema Gamondi aliyeita kikosi cha wachezaji 28 wakiwamo wakongwe, Samatta, Msuva, Shomary Kapombe na wenye damu changa kama kina Morice Abraham, Pascal Msindo na wengine ambao wanaendelea kujifua kambini.

Stars itaondoka leo asubuhi mara baada ya mazoezi kwenda Morocco kuwahi fainali hizo zinazoshirikisha timu 24.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Msuva, aliliambia Mwanaspoti kutoka kambini akisema; “Unajua ni heshima kubwa tena kuivaa jezi ya taifa kwenye mashindano makubwa kama AFCON. Tumekuja na malengo makubwa, tunajua changamoto zilizopo, lakini tunaamini safari hii tunaweza kufanya vizuri zaidi.”

Kwa Msuva, mashindano ya mwaka huu yatakuwa ya tatu kwake kushiriki fainali za AFCON, baada ya mara ya kwanza 2019, Misri ambako Stars iliburuza mkia katika msimamo wa kundi C baada ya kupoteza mechi zote tatu, Msuva alifunga bao moja katika fainali hizo.

Fainali nyingine ni za 2023 Ivory Coast, ambako alikuwa mmoja wa wachezaji waliobeba matumaini ya mashabiki wa soka la Tanzania.

Akizungumzia mashindano yaliyopita kule Ivory Coast, Msuva alikiri kuwa kikosi kimejifunza kutokana na matokeo waliyoyapata ambapo Stars ikiwa kundi F ilianza kwa kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Morocco, ikatoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Zambia kabla ya kumaliza kwa suluhu dhidi ya DR Congo.

“Safari hii tunataka kubadilisha taswira, kuvuka hatua ya makundi na kuwapa Watanzania sababu ya kutabasamu,” aliongeza.

Bao pekee la Taifa Stars katika fainali hizo za 2023 lilifungwa na Msuva mwenyewe katika sare ya 1-1 dhidi ya Zambia, rekodi inayomfanya aingie kwenye michuano ijayo akiwa mmoja wa wachezaji muhimu wa Stars katika safu ya ushambuliaji.