Arusha. Tasnia ya habari Mkoa wa Arusha imepata pigo baada ya mwanahabari mkongwe, Neema Mhando (53) kufariki dunia leo Jumatano, Desemba 17, 2025 nyumbani kwa wazazi wake eneo la Daraja Mbili jijini Arusha.
Taarifa za kifo chake zimetolewa na Ofisa Habari wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Ally Nyambi kwa waandishi wa habari akisema Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji na watumishi wote wamepokea kwa masikitiko kuondokewa ghafla na mtumishi mwenzao.
“Kwa masikitiko makubwa nawajulisha mwandishi mwenzetu, Neema Mhando amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jumatano.
“Jana tulikuwa naye ofisini ilipofika saa tisa alasiri dereva wa nyumbani kwao alikuja kumchukua na alipofika nyumbani kwao alikuwa chini ya uangalizi wao kisha alikwenda kujipumzisha na ilipofika saa 11 alfajiri alifariki,” amesema Nyambi
Neema hadi umauti unamkuta alikua Ofisa Habari Daraja la Pili wa Halmashauri ya Jiji la Arusha nafasi aliyoitumikia kwa kipindi cha miaka mitatu akitokea Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela (NM-AIST) kilichopo Wilaya ya Arumeru mkoa wa Arusha.
Pia, aliwahi kufanya kazi Shirika la Utangazi Tanzania (TBC).
Baba mzazi wa marehemu, Profesa Peter Mhando akizungumza na Mwananchi nyumbani kwake eneo la Daraja Mbili ameeleza kusikitishwa na msiba wa ghafla uliotokea na kuacha pengo kubwa katika familia hiyo.
“Familia imepokea msiba huu kwa maumivu makubwa, kila kitu tunamwachia Mungu, Neema alikuwa kipenzi cha kila mtu kwenye familia hii, tunamwomba Mungu aipumzishe roho yake mahali pema,” amesema Profesa Mhando.
Mwenyekiti wa Arusha Press Club (APC), Claud Gwandu ameeleza kupokea taarifa za kifo cha mwanahabari huyo kwa masikitiko na kuwa waandishi wa habari waliofanya naye kazi wataendelea kumkumbuka kwa weledi na moyo wake wa kuwasaidia waandishi wanaochipukia kwenye taaluma ya habari.
“Neema alikuwa rafiki wa waandishi wa habari wakati akiwa Ofisa Habari Chuo Kikuu cha Nelson Mandela na alipohamia Halmashauri ya Jiji la Arusha ni mtu aliyekuwa akitoa ushirikiano kwa jambo lolote lililohitaji mchango wake,tumepoteza mtu aliyekuwa anatoa mchango muhimu kwenye tasnia yetu,” amesema Gwandu.
Mwandishi wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Veronica Mheta amesema alimfahamu Neema Mhando tangu mwaka 2005 jijini Dar es Salaam kwenye majukumu ya habari akimwelezea ni mwanataalumu aliyependa kujifunza na kuwasaidia waandishi wachanga kufanya kazi zao kwa weledi.