Siku moja Mwalimu Nyerere alisema kuwa aliona wakubwa wakienda kufanya azimio Zanzibar. Alipowaona wakirudi kimya kimya na sera za uchumi zikibadilika kufuata matakwa ya WB na IMF, akawa na uhakika kuwa ndoto zake za Azimio la Arusha zilikuwa zimefikia ukingoni. Mwenyewe alijua fika kuwa Azimio la Arusha lilikuwa ni chukizo kubwa kwa wakoloni na wanyonyaji.
Kimsingi Nyerere hakupenda sera za wababe wa uchumi wa dunia. Aliziona jitihada zao za kuua uchumi wa Afrika, wakitumia nyenzo za misaada na mikopo. Mwanzoni sikumwelewa lakini baada ya mashirika hayo kukataza utoaji wa ruzuku kwa wakulima Waafrika, wakati yakiwapa ruzuku wakulima wazungu nikaanza kuelewa. Mwisho wa siku sisi tukose mazao na wao ndio watuuzie chakula.
ANC walikuwa na msimamo thabiti uliotaka uwezeshwaji wa raia weusi wa Afrika ya Kusini. Hii ilikuwa na maana kubwa kwao baada ya kutawaliwa na kunyimwa elimu kwa muda wote.
Uhuru pekee usingewapa maendeleo kwani wasingeweza kutumia fursa yoyote, bado wangelikuwa mbumbumbu na tegemezi kiuchumi. Hiki ndicho kitu ambacho Mwalimu alikiita “Uhuru wa Bendera”.
Kwa uelewa wangu, kuendeleza vipawa kwa wazawa masikini ni kuwakomboa kiuchumi kwa kiasi kikubwa sana. Kinyume chake ni kuwanyima haki zao za kimsingi. Nawaona vijana wa Kitanzania sawa na wale waliokosa elimu kabisa.
Wao walitanguliwa na babu zao walioishi kwa kunyimwa elimu chini ya tawala za kikoloni. Lakini wengi kati ya waliopata elimu ya kikoloni, walifundishwa kutumia elimu kwa ajili ya kuwatumikia wazungu.
Siri ya elimu ni kumkomboa mtu kifikra. Humwongezea upeo wa kutambua yeye ni nani na afanye nini. Lakini watu wetu walifuata minyororo ya kikoloni. Hawakuwekewa mazingira ya kujinufaisha wenyewe, wala kutambua kuwa vipawa vyao vingeweza kuwainua kiuchumi.
Kwa njia hii, hata wazee hawakuweza kukubali kuendeleza vipaji vya watoto wao. Hakukuwa na mazingira rafiki.
Ilifikia mahala mtoto aliyeulizwa na wazazi wake “unataka kuwa nani?” aliogopa kusema anavutiwa na ufundi au michezo. Ustaarabu ulikuwa ni kufanya kazi ofisini.
Hivyo na vijana hawa wakasomea fani zisizo chaguo lao ili mradi waonekane kuwa nao ni wasomi. Na bahati mbaya zaidi hawakuweza kujua kuwa ulimwengu wa teknolojia utakuja kuziingilia kazi hizo na kupunguza thamani yao.
Umuhimu wa kuendeleza vipawa unaonekana zaidi wakati huu wa ukosefu wa ajira. Vijana wengi waliosoma na wasiosoma, wapo mtaani wakikosa shughuli za kuwaingizia kipato.
Miongoni mwao wamo wenye vipawa (talents) ambavyo vingepatiwa mwendelezo, vingeweza kuzaa mamilioni ya ajira binafsi. Wanaojiajiri wangeweza kuwaajiri wenzao wenye uelekeo unaofanana na tatizo lingepungua kama sio kwisha kabisa.
Mifumo kutokuwa rafiki ni tatizo lisilotazamwa kwa umakini. Mara nyingi tulisikia watu wakikamatwa kwa kutengeneza bidhaa nyeti bila kuwa na vibali. Bidhaa zingine zilikuwa za hatari kama magobore. Lakini wengine walikwamishwa kuendeleza bunifu zao kwa visingizio vya kuepusha muingiliano.
Kwa mfano, wabunifu wa helikopta, vituo vya mawasiliano walionekana kusumbua mamlaka za anga na mawasiliano.
Kwa mtazamo wangu, watu hawa wangeendelezwa kwa kupatiwa elimu sahihi juu ya viwango na vibali, tungeinua uchumi kwa kasi kubwa zaidi.
Badala ya kutumia fedha za kigeni kuagiza bidhaa hizo, sisi tungeingiza fedha kwa kuuza nje ya nchi. Vilevile uzalishaji wa bidhaa hizo ungepunguza tatizo la ajira. Kila mmoja wetu anakiri kuwa tunawahitaji sana wabunifu kama hawa, lakini ni lazima kuwatengenezea mifumo yenye urafiki nao.
Nasema hivi kwa sababu maendeleo yana gharama zake.
Uzalishaji wa ndani una tija kwa Taifa, lakini unawakwaza wazee wa kuongeza sufuri kwenye matumizi ya kodi za watanzania. Wapo watu wanaoombea Tanzania ya leo iagize hata maji ya kupikia kutoka nje.
Mtu asiye mzalendo ataongeza gharama za manunuzi kwa faida binafsi. Hapo ndipo utajua kuwa tupo na mumiani wanaofanya jitihada za kuupoteza uzalendo.
Nakumbuka marehemu Magufuli aliwahi kubadili mpango wa kupeleka ndege nje ikapigwe rangi. Ndege ikahudumiwa hapa na kuokoa mamilioni ya shilingi.
Kwa akili ya kawaida nalifananisha hili sawa na mtu anayeokoa fedha ya kung’arisha viatu kwa fundi, akafanya mwenyewe kila siku. Elfu moja kila siku ni fedha nyingi kwa mwezi, na ni nyingi zaidi kwa mwaka.
Mpaka sasa najiuliza masomo ya Stadi za Kazi, Sayansi Kimu, Sanaa, Ubunifu na Michezo yalikufa vipi.
Zamani wanafunzi walishiriki mashindano ya Umishmta na Umiseta. Mashindano haya yaliibua vipaji vipya kila mwaka, hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa uhitaji wa wachezaji wa kigeni.
Kwa hiyo ziara za wakubwa kwenda kusaka wachezaji, na kusaini mikataba yenye sufuri za nyongeza ilikuwa ngumu.
Sio siri, ipo haja ya kuirejea historia. Wakati Wizara ya Vijana ikiwapambania wenzao waliokosa ajira, izingatie kuwatafuta na kuwawekea mifumo rafiki wale waliokwamishwa ndoto zao. Hata kama anatengeneza bunduki apewe msaada na maelekezo.
Ijulikane kuwa shujaa na gaidi ni mtu mmoja, ila inategemeana na upande aliosimamia. Mandela alikuwa shujaa wa wazalendo, lakini akawa mhaini kwa Serikali ya kibaguzi.
