Othman: SUK ni chombo cha kuleta umoja sio kulinufaisha kundi fulani

Pemba. Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman amesema chama hicho kinaiangalia Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK) kama ni chombo cha kuleta umoja, mshikamano na usawa kwa wananchi sio kulinufaisha kundi la watu fulani.

Othman ameyasema hayo jana Jumanne, Desemba 16, 2025 kwa nyakati tofauti wakati akiwashukuru wazee pamoja na wananchi wa kijiji cha Shumba Mjini, Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba. 

Mwenyekiti huyo, amesema Serikali ya SUK inahitaji kuwa chombo kinachoweza kutumiwa na wananchi kwa lengo la kupata haki zao na haipendezi kutumiwa ili kulinufaisha kundi fulani na kuendelea kuwakandamiza wanyonge.

Amesema, katika kuliona hilo ndio sababu ya chama hicho kukutana na viongozi mbalimbali wenye nia njema na kuwatafutia haki zao wananchi kwa njia ya amani.

Amesema, tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu Oktoba 29, mwaka huu bado chama hicho kinaendelea kupigania haki za Wazanzibar kwa njia ya amani ikiwemo mazungumzo na viongozi wanaoitakia mema nchi pamoja na mahakama.

“Tangu umalizike uchaguzi, ambao ulionesha kasoro nyingi, sisi bado tunaendelea kuipigania haki ya Wazanzibari kwa njia za amani yakiwemo mazungumzo na viongozi wanaoitakia mema nchi na pia kwenye mahakama,” amesema Othman. 

Othman ambaye pia alikuwa mgombea urais wa chama hicho, amesema hamasa za wananchi tangu wakati wa kampeni, uchaguzi na baada ya uchaguzi bado zinaashiria mabadiliko ya kutaka nchi iwe mpya yenye umoja na mamlaka kamili.

Mwenyekiti huyo, amesema chama hicho kimekusanya ushahidi wa kutosha kuonesha kuwa uchaguzi huo ulichafuliwa kwa makusudi na tayari wagombea ubunge na uwakilishi wa chama hicho upande wa Zanzibar wamefungua kesi mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi wa Oktoba 2025.

“Mahudhurio yenu ni sauti kubwa inayotupa nguvu katika mapambano haya ambayo kila mmoja ameijua ilivyo, nawanasihi wanachama na wananchi kuzidisha subira pamoja na mshikamano,” amesema.

Othman ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar mstaafu anaeleza hayo, wakati Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameacha nafasi nne za uwaziri zinazopaswa kujazwa na ACT – Wazalendo, chama kilichoshika nafasi ya pili kwa kura za urais na idadi ya majimbo katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Wizara hizo ni Utalii na Mambo ya Kale, Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda, Wizara ya Afya na Wizara ya Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais.

Katika uchaguzi huo, ulioshindaniwa na wagombea 11 wa kiti cha urais, Dk Mwinyi wa CCM alishinda kwa kura 448,892 sawa na asilimia 74.8 akifuatiwa na Othman Masoud wa ACT – Wazalendo, aliyepata kura 139,399 sawa na asilimia 23.22.

Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, toleo la mwaka 2010, inaeleza ili kuundwa kwa SUK, chama kinachoshinda kitashirikiana na chama chochote cha upinzani kilichoshika nafasi ya pili kwa wingi wa majimbo katika Baraza la Wawakilishi.

Pia, Katiba hiyo iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2010, ibara ya 39 (3), kifungu kidogo (1), inaeleza Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, atateuliwa iwapo chama chake kitapata asilimia 10 au zaidi ya kura za urais.

Aidha, ACT – Wazalendo inalazimika kufanya uamuzi wa kuingia SUK, ndani ya siku 90 zilizowekwa kikatiba na muda huo ukipita, Rais Mwinyi anaweza kujaza nafasi hizo kwa kadri itakavyompendeza.

Ingawa hadi sasa kati ya siku 90 zilizotolewa kuhusu ACT – Wazalendo kujiunga na SUK, zimebaki 47, hakuna kiongozi yeyote wa chama hicho cha upinzani aliyetoa kauli au mwelekeo iwapo wataingia SUK au la.

Awali, akitoa neno la ukaribisho, Mwenyekiti chama hicho Mkoa, Rashid Khalid amesema wananchi wa mkoa huo wapo imara na wanaendelea kukijenga chama hicho.

Amesema, wanachosubiri ni kuziona haki zao za uchaguzi mkuu kwa wagombea uwakilishi na wabunge walioshinda ila kunyimwa ushindi huo.