UONGOZI wa Mtibwa Sugar upo kwenye mazungumzo na kiungo mshambuliaji wa Mlandege, Juma Kidawa ‘Pogba’ kwa ajili ya kuongeza nguvu kikosini dirisha dogo.
Pogba ambaye mwanzoni mwa msimu alikuwa akihusishwa kutua Simba kabla ya mpango wake kufa baada ya wekundu hao kumnasa Daud Semfuko kutoka Coastal Union anatajwa kuwa katika hatua nzuri kuibukia Mtibwa Sugar.
Chanzo cha kuaminika kutoka Mtibwa kimeliambia Mwanaspoti kuwa ni kweli wapo kwenye mchakato wa mazungumzo na kiungo huyo ambaye wanaamini ataongeza kitu eneo analocheza.
“Ni kweli kuna mazungumzo yanaendelea baina yetu na mchezaji huyo ,lakini bado hayajafikia hatua ya kuwekwa wazi kuwa ataitumikia Mtibwa Sugar bado ana mkataba wa miezi sita na waajiri wake wa sasa,” kilisema chanzo hicho kutoka Mtibwa na kuongeza;
“Kilichopo ni makubaliano na waajiri wake kabla ya kumfuata mchezaji mwenyewe mambo yakienda vizuri basi anaweza kuwa sehemu ya kikosi chetu.”
Mwanaspoti lilifanya jitihada za kumtafuta mchezaji Pogba ambaye alikiri kupokea taarifa za kupokea ofa kutoka Mtibwa Sugar kupitia kwa meneja wake huku akiweka wazi kuwa hafahamu nini kinaendelea lakini taarifa hiyo anayo.
“Mimi kazi yangu ni kucheza na nipo tayari kucheza timu yopyote ninachoangalia ni maslahi tu ila hapa bado nina mkataba wa miezi sita, unamalizika mwisho wa msimu,” alisema.
“Licha ya kubakiza miezi sita Mlandege pia wameniita mezani kwa ajili ya kufanya mazungumzo ili niweze kuongeza mkataba mpya na ndipo meneja wangu aliponiambia pia ana ofa nyingine kutoka Mtibwa Sugar.”