DAR ES SALAAM – Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetangazwa kuwa Mdhibiti Bora wa Mwaka katika Tuzo za Ubunifu katika Utumishi wa Umma (PSIA) 2025, kwa mchango wake katika kuimarisha ubora wa huduma, ubunifu na usimamizi wa viwango nchini.
Tuzo hiyo ilitolewa Jana wakati wa hafla ya PSIA 2025, iliyoandaliwa chini ya kaulimbiu “Kuendeleza ubora katika utumishi wa umma kupitia ubunifu na ushirikiano”, ikilenga kutambua taasisi zinazotekeleza majukumu yao kwa weledi, ubunifu na ufanisi.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Bi. Ashura Katunzi, alisema heshima hiyo itaongeza hamasa kwa watumishi wa shirika hilo kuendelea kubuni na kuimarisha taaluma katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Tuzo hii ni chachu ya kuongeza uwajibikaji na ubunifu katika kazi zetu, hususan katika kuunga mkono ukuaji endelevu wa sekta za viwanda na biashara kupitia usimamizi bora wa viwango,” alisema Bi. Katunzi.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi na Ajira Zanzibar, Bw. Khamis Suleiman Mwalimu, aliwataka wadau wa maendeleo kuimarisha ushirikiano na taasisi za umma ili kuongeza ubunifu na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, akisisitiza kuwa taasisi imara ndizo msingi wa maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa PSIAB, Bw. Steven Mkomwa, alisema TBS ni miongoni mwa taasisi zilizodhihirisha ubora wa kiutendaji, uadilifu na ubunifu, jambo lililoipa ushindi wa tuzo hiyo muhimu.
Tuzo ya PSIA 2025 inalenga kuhimiza taasisi za umma kubuni suluhisho bunifu, kuongeza ufanisi na kushirikiana kwa karibu kwa manufaa ya maendeleo ya taifa.









