Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeandika historia mpya katika sekta ya maliasili baada ya kushinda Tuzo ya Umahiri katika Uhifadhi wa Misitu na Ulinzi wa Bioanwai kwa mwaka 2025, tuzo inayotambua taasisi zilizoonesha matokeo chanya na endelevu katika kulinda rasilimali za asili.
Tuzo hiyo, inayojulikana kama Best Forest Conservation and Biodiversity Protection Award (TPSIA) 2025, imetolewa jana, Desemba 16, 2025, jijini Dar es Salaam katika hafla maalumu iliyofanyika Ukumbi wa Mlimani City.Hafla hiyo iliandaliwa na Tanzania Professional Skills and Innovation Awards (TPSIA) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo na sekta binafsi, kwa lengo la kutambua na kuthamini mchango na jitihada za taasisi za umma katika maendeleo ya taifa.
Mgeni rasmi wa hafla hiyo alikuwa Mhe. Shariff A. Shariff, Waziri wa Kazi na Uwekezaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, aliyewakilishwa na Ndg. Hamis Suleiman Mwalimu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi na Uwekezaji, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ambaye alikabidhi tuzo rasmi kwa TFS.
Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Mkurugenzi wa Huduma Saidizi, Emmanuel Wilfred, alisema ushindi huo ni uthibitisho wa juhudi kubwa zinazofanywa na wakala huo katika kusimamia misitu na kulinda bioanwai kwa manufaa ya taifa na vizazi vijavyo.
“Tunawashukuru waandaaji wa tuzo hizi kwa kutambua kazi kubwa inayofanywa na TFS katika uhifadhi wa misitu, ulinzi wa bioanwai na usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu. Ushindi huu ni ishara kuwa jitihada zetu zinaonekana na kuthaminiwa,” alisema Wilfred.
Aliongeza kuwa tuzo hiyo ni chachu ya kuongeza kasi ya utendaji, ikiwamo kuimarisha mapambano dhidi ya uharibifu wa misitu, uvunaji haramu, pamoja na kuendeleza ushirikishwaji wa jamii katika uhifadhi.
“Tuzo hii inatupa motisha ya kufanya kazi kwa bidii zaidi, kwa weledi na kwa uwajibikaji mkubwa ili kuhakikisha misitu ya Tanzania inalindwa na kuendelea kuwa nguzo ya uchumi, mazingira na ustawi wa wananchi,” aliongeza.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kamati ya TPSIA, Steven Mkomwa, TFS imechaguliwa kutokana na matokeo halisi ya utekelezaji wa sera na mikakati ya uhifadhi, ikiwamo kuimarika kwa ulinzi wa hifadhi za misitu, ongezeko la mapato yatokanayo na misitu, na mchango wake katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mgeni rasmi Mhe. Shariff A. Shariff, Waziri wa Kazi na Uwekezaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (kulia) akimkabidhi tuzo Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Mkurugenzi wa Huduma Saidizi, Emmanuel Wilfred, wakati wa hafla ya utoaji tuzo jana, Desemba 16, 2025, katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
(PICHA NA EMMANUEL MASSAKA MMG)

.jpeg)