‘Tuisaidie Serikali kujenga, kurejesha umoja’

Musoma. Askofu Mkuu wa Kanisa la Menonite Tanzania, Nelson Kisare amewaomba viongozi wa dini nchini kuisaidia Serikali kujenga na kurejesha umoja na mshikamano wa kitaifa ili kurejesha hali ya utulivu, amani na usalama nchini.

Askofu Kisare ametoa wito huo mjini Musoma leo Jumatano Desemba 17, 2025 katika warsha ya elimu ya amani kwa viongozi wa dini mkoani Mara iliyoandaliwa na kanisa hilo kwa kushirikiana na Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF).

Amesema hakuna haja ya kulipa kisasi kwa yaliyotokea isipokuwa viongozi wanapaswa kuhakikisha wanasimamia haki ili amani iweze kudumu kwa maelezo kuwa haki inaposhindwa kutimizwa basi amani pia inatoweka.

Askofu Kisare amesema viongozi hao wa dini  wanapaswa kuwoambea viongozi wa Serikali na wa  siasa kutimiza wajibu wao kwa misingi ya sheria  za nchi katika kutekeleza majukumu yao ili kuepusha Taifa na machafuko na vurugu kama ilivyotokea Oktoba 29, 2025.

Amesema ufumbuzi wa hali ilivyo sasa nchini unapaswa kufanyika kwa upatanisho  kwa njia ya amani huku akisema viongozi wa dini wanapaswa kuwa daraja la amani na upendo katika jamii.

“Tuombe amani ya nchi yetu kwa Mungu kwani Mungu amesema tukirudi kwake kwa kutubu na kuomba atatusamehe na ataiponya nchi yetu,” amesema.

Amesema machafuko yaliyotokea yametikisa amani ya nchi, hivyo ipo haja ya wadau wote kwa pamoja kuangalia  ni namna gani amani inarejea huku akisema madai ya haki yasiwe kigezo cha kuvunja amani ha nchi.

“Hata kama tunadai haki basi ipo haja ya kuangalia namna bora ya kudai haki bila kuvunja amani na kwa hali ilivyo, suala la maridhiano ni muhimu sana kwani hata vitabu vitakatifu vinazungumza kuhusu maridhianao pale ndugu wanapotofautiana,” amesema

Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini wa  Taasisi ya Mwalimu Nyerere,  Joseph Butiku amesema kutokana na hali ilivyo suala la maridhiano ni la muhimu na kwamba wadau wote wanapaswa kushirikiana ili kuzuia machafuko na vurugu kutokea tena.

Amesema  mazungumzo kwa pande zote ni muhimu na kwamba msingi wa yote ni haki na kufanya mazungumzo na wananchi kutasaidia  kujua shida iko wapi na kipi kifanyike.

“Tuna kila sababu ya kuhakikisha tunatunza amani ya nchi yetu kwani kila jambo ikiwamo suala la maendeleo linategema amani kama hakuna amani basi hakuna maisha,” amesema Sheikh wa Wilaya ya Musoma Juma Suleiman. Mchungaji wa Kanisa la Anglikan Agutu, Juma amesema bado kuna nafasi ya kurejesha nchi kwenye nafasi iliyokuwapo awali na kuwa bora zaidi endapo kila mmoja atatimiza wajibu wake.