Dar es Salaam. Watafiti wamethibitisha kuwa mwanamke anapotoa upepo hapaswi kuona haya, kwani harufu kali ya ushuzi anaoutoa huenda ikawa kichocheo cha siri cha afya ya ubongo wake.
Kwa wastani, binadamu hutoa ushuzi hadi mara 23 kwa siku, lakini si mara zote kila ushuzi kuwa na harufu sawa. Utafiti unaonyesha kuwa gesi ya tumbo ya wanawake hunuka zaidi kuliko ya wanaume, na kuna sababu ya kisayansi inayofafanua hali hiyo.
Harufu hiyo huenda ikawa ishara kwamba mwanamke ana uwezekano mdogo wa kupata ugonjwa wa Alzheimer (uharibifu wa taratibu wa seli za ubongo) baadaye maishani.
Ugonjwa wa Alzheimer ni ugonjwa wa ubongo unaoendelea polepole, unaoathiri zaidi kumbukumbu, uwezo wa kufikiri, kuzungumza na kufanya uamuzi. Ni chanzo kikuu cha ugonjwa wa kusahau (dementia), hasa kwa watu wazee.
Akichangia hoja hiyo, mtaalamu wa afya ya jamii, Dk Paul Masua, amesema tafiti nyingi zinaonyesha kuwa ushuzi wa mwanamke huwa na harufu kali zaidi kuliko wa mwanaume, ambapo kwa kawaida harufu ya ushuzi hutokana na gesi ya hydrogen sulfide.
Amesema wanawake huwa na kiwango kikubwa cha gesi hiyo kwenye matumbo yao, hali inayosababisha ushuzi wao kuwa na harufu kali zaidi.
Dk Masua anabainisha kuwa tafiti pia zinaonyesha kuwa kwa kuwa wanawake wana kiwango kikubwa cha gesi hiyo, ambayo kwa kiasi fulani husaidia kulinda mishipa ya fahamu, huwafanya wawe na hatari ndogo ya kuugua magonjwa ya kupoteza kumbukumbu wanapozeeka.
“Licha ya kwamba wanawake wengi hujihisi vibaya au kuogopa wanapotaka kutoa upepo, kufanya hivyo ni sehemu ya kawaida ya maisha ya binadamu. Kwa kawaida, binadamu anapaswa kutoa upepo angalau mara 23 kwa siku,” amesema.
Mwaka 1998, Dk Michael Levitt, daktari bingwa wa magonjwa ya tumbo na mtafiti maarufu aliyefahamika kama “Mfalme wa Ushuzi,” alianza utafiti wa kubaini gesi zipi husababisha harufu ya kipekee ya ushuzi.
Aliwachagua watu wazima 16 wenye afya njema, bila historia ya matatizo ya mfumo wa mmeng’enyo wa chakula, na akawafanya kila mmoja avae kifaa cha kukusanyia ushuzi, ambacho kimsingi kilikuwa bomba la puru lililounganishwa na mfuko.
Baada ya washiriki kula maharagwe ya pinto na kunywa dawa ya kuharisha, watafiti walikusanya ushuzi uliotoka baadaye. Levitt na wenzake walifanya uchambuzi wa gesi kwa kutumia teknolojia ya ‘gas chromatography mass spectrometry’ ili kubaini kwa usahihi aina ya gesi zilizokuwamo ndani ya mifuko hiyo.
Sampuli hizo pia zilipitia “jaribio la kunusa,” ambapo waamuzi wawili waliletwa kupima kila ushuzi kwa kipimo cha kuanzia sifuri hadi nane, ambapo nane ilimaanisha “harufu kali sana.” Waamuzi hao hawakujua kuwa walikuwa wananusa ushuzi wa binadamu.
Matokeo yalionyesha kuwa gesi kuu zinazosababisha harufu ya ushuzi wa binadamu ni misombo yenye salfa, hususan gesi ya hydrogen sulfide, kemikali inayotoa harufu maarufu ya yai lililooza.
Ingawa wanaume kwa kawaida hutoa kiasi kikubwa zaidi cha gesi, utafiti ulibaini kuwa ushuzi wa wanawake una kiwango kikubwa zaidi cha hydrogen sulfide ikilinganishwa na wanaume. Waamuzi walikubaliana kwa pamoja, wakitathmini ushuzi wa wanawake kuwa na ukali mkubwa wa harufu kuliko wa wanaume.
Si ajabu basi wanawake wengi hujihisi aibu zaidi kuhusu kutoa upepo. Utafiti wa mwaka 2005 ulibaini kuwa wanaume wa aina tofauti hawakusumbuliwa sana iwapo wengine wangesikia au kunusa ushuzi wao, ilhali wanawake walionyesha kiwango kikubwa cha kujisitiri na kujihisi vibaya.
Lakini hapa ndipo mshangao ulipo: wanawake huenda wakapaswa kukubali ushuzi wao wenye harufu kali, kwani unaweza kuwa na manufaa kiafya.
Ingawa hydrogen sulfide ni sumu kali endapo itakuwa katika kiwango kikubwa, kiasi kidogo kama kile kinachopatikana kwa wingi kwenye ushuzi wa wanawake kinaweza kusaidia kulinda seli za ubongo zinazozeeka dhidi ya ugonjwa wa Alzheimer.
Ndani ya mwili wa binadamu, hydrogen sulfide ina jukumu katika kazi mbalimbali, ikiwemo kusaidia mawasiliano ya seli za ubongo kwa kurekebisha protini kupitia mchakato unaoitwa sulfhydration.
Kwa hiyo, kina dada, mara nyingine mnapotoa ushuzi, msione haya. Harufu hiyo kali huenda ikawa kichocheo cha siri cha afya ya ubongo wako.