Wakulima ‘wang’atwa sikio’ uzingatiaji kilimo cha kisasa

Moshi. Imeelezwa kuwa uzingatiaji wa matumizi ya sayansi na teknolojia za kisasa katika kilimo utawasaidia wakulima nchini kupata mazao bora, kuongeza tija na hatimaye kuchochea mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano, Desemba 17, 2025 na Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Zebadiah Moshi, wakati wa mkutano wa tathmini ya utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na Norwegian Church Aid (NCA) kwa kushirikiana na dayosisi hiyo.

Moshi amesema kilimo kina mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa taifa, hivyo matumizi ya teknolojia za kisasa yatawawezesha wakulima kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa mazao na kunufaika zaidi kiuchumi.

Hivyo, amewahimiza wakulima kuachana na kilimo cha mazoea na kubadili mtazamo kuelekea kilimo cha biashara.

“Tungependa kufunua fikra za watu waingie kwenye kilimo cha biashara. Dhana iliyokuwepo ni kwamba kilimo cha biashara kinahitaji mashamba makubwa ya ekari nyingi, lakini hata ekari moja au mbili zinaweza kutoa uzalishaji mkubwa endapo zitatumika kwa utaalamu,” amesema.

Kwa upande wake, mtaalamu kutoka taasisi inayojishughulisha na afya ya udongo ya Live Support System, Timothy Wafula amesema Tanzania ina ardhi yenye rutuba na rasilimali nyingi za kilimo, lakini changamoto kubwa ipo kwa wakulima wanaolima bila kupima afya ya udongo.

Amesema matumizi ya ardhi kwa muda mrefu bila uchunguzi wa kitaalamu husababisha upungufu wa virutubisho, hali inayochangia mavuno kuwa madogo.

“Kupima afya ya udongo humsaidia mkulima kupanga vizuri uwekezaji wake na kufanya kilimo cha biashara chenye tija. Ni muhimu kupima udongo kila msimu kabla ya kuanza kilimo,” amesema Wafula.

Naye Katibu wa Idara ya Uwakili na Miradi ya NCA, Mchungaji Andrew Munis, amesema kupitia miradi ya kanisa hilo wataendelea kutoa elimu kwa wakulima ili kuhakikisha wanatekeleza kilimo chenye tija na chenye kuleta matokeo chanya kwa maisha yao.

Amesema mkutano huo uliwakutanisha wadau mbalimbali wa Serikali kutoka halmashauri za Babati, Karatu, Siha, Hai, Moshi DC na Rombo, pamoja na maofisa maendeleo ya jamii, kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano katika kuendeleza sekta ya kilimo.