Wakunga, wauguzi waonywa udanganyifu wa mtihani

Dodoma. Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania limeonya vikali dhidi ya udanganyifu wa aina yoyote wakati wa mtihani wa kada ya uuguzi na ukunga utakaofanyika Desemba 29, 2025.

Jumla ya watahiniwa 4,414 katika wanatarajia kufanya mtihani huo wa umahiri.

Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga, Agnes Mtawa amesema mtu yeyote atakayebainika kujihusisha na vitendo vya udanganyifu atachukuliwa hatua za kisheria, ikiwemo kufutiwa mtihani kwa mujibu wa kifungu cha 22 cha kanuni zinazosimamia taaluma hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Desemba 17, 2025, Mtawa amesema mtihani huo utafanyika katika vituo sita nchini na utawahusisha wahitimu wa ngazi za astashahada, stashahada na shahada za uuguzi na ukunga, pamoja na shahada ya uuguzi katika utoaji wa dawa za usingizi.

Amesema usimamizi mkali utawekwa ili kuhakikisha wanaofaulu ni wale waliopata elimu husika, wanaoelewa taaluma yao na wako tayari kutoa huduma bora kwa Watanzania.

“Mtihani huu unafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Uuguzi na Ukunga ya mwaka 2010, kifungu cha 6 (o), kwa lengo la kupima umahiri kabla ya kumruhusu mtaalamu kwenda kutoa huduma kwa jamii,” amesema Mtawa.

Ameongeza kuwa lengo kuu la mtihani huo ni kuhakikisha jamii inapata huduma bora na salama za uuguzi na ukunga zinazotolewa na wataalamu wenye weledi na umahiri.

Kwa mujibu wa Mtawa, vituo vitakavyotumika ni Chuo Kikuu cha Kampala, Dar es Salaam ambako kutakuwa na watahiniwa 1,098; Taasisi ya Afya, Sayansi na Teknolojia (Tandabui) mkoani Mwanza yenye watahiniwa 971; na Chuo Kikuu cha St. John cha Dodoma kilichopangiwa watahiniwa 793.

Vituo vingine ni Chuo Kikuu cha Katoliki Iringa chenye watahiniwa 720, Chuo cha Uhasibu Arusha (549) na Tabora Polytechnic ambako watahiniwa 283 watafanya mtihani.

Msajili huyo amesisitiza watahiniwa kufika katika vituo vyao siku moja kabla ya mtihani kwa ajili ya kupata maelekezo, pamoja na kuzingatia kanuni, taratibu na maelekezo yote yatakayotolewa.

Akizungumza kwa niaba ya watahiniwa, Muuguzi Mwendwa Ashery amesema mtihani huo hauna ugumu kwa kuwa unahusisha kile walichofundishwa vyuoni, akiwataka watahiniwa wenzake kuondoa hofu na kujiamini.

“Binafsi sioni kama kuna mambo magumu. Kilichosomwa ndicho kinachopimwa, hivyo ni suala la kujiamini na kuwa makini,” amesema Mwendwa.

Baraza la Uuguzi na Ukunga ni mamlaka ya kisheria inayosimamia taaluma ya uuguzi na ukunga nchini, iliyoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Nursing and Midwifery Act ya mwaka 2010 pamoja na kanuni zake.