Mbeya. Imeelezwa kuwa jumla ya wanafunzi 686 wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mbeya (CUoM), wameshindwa kuhitimu masomo yao kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za vifo, utoro na kushindwa kutimiza vigezo vya kitaaluma.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano, Desemba 17, 2025 na Kaimu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Romuald Haule, wakati wa mahafali ya 10 yaliyofanyika mkoani Mbeya, mgeni rasmi akiwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Wanawake na Makundi Maalum, Maryprisca Mahundi.
Profesa Haule amesema katika mahafali hayo jumla ya wahitimu 2,819 wamehitimu masomo yao, wanaume 1,376 huku wanawake wakiwa 1,443.
Amesema sababu za wanafunzi 686 kushindwa kuhitimu katika mwaka wa masomo 2024/2025 ni utoro, kushindwa kukidhi vigezo vya kitaaluma na vifo, hali ambayo imeathiri takwimu za wahitimu wa chuo hicho.
Hata hivyo, Profesa Haule amesema chuo hicho kimeendelea kufanya vizuri kwa kuwa asilimia 80 ya wanafunzi wake wamenufaika na mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB).
“Tuna kila sababu ya kuishukuru Serikali kwa kuendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta ya elimu ya juu, hatua inayochangia kuongeza ubora wa taaluma pamoja na maboresho ya mitaala ya masomo ili kukidhi mahitaji ya sasa ya soko la ajira,” amesema Profesa Haule.
Naibu Waziri, Mahundi amesema Serikali inaendelea kuboresha mitalaa ya elimu ya juu pamoja na mfumo wa utoaji wa mikopo kwa lengo la kuhakikisha Taifa linazalisha nguvu kazi yenye ujuzi na maarifa stahiki.
Amesema mafanikio ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Mbeya ni miongoni mwa vichocheo vya ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Mbeya na mchango wake kwa maendeleo ya Taifa kwa jumla.
“Tunaendelea kutambua mchango mkubwa wa vyuo vya elimu ya juu nchini, na kwa niaba ya Serikali tunahakikisha changamoto mbalimbali, ikiwamo upatikanaji wa mikopo kwa wakati, zinaendelea kufanyiwa kazi,” amesema Mahundi.
Naye Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya, Godfrey Mwasekaga amewataka wahitimu kuepuka utegemezi kwa wazazi wanaporejea katika jamii, akiwahimiza kutumia elimu waliyoipata kama chachu ya kujiajiri, hasa kutokana na changamoto ya ukosefu wa ajira nchini.
Askofu Mwasekaga ameiomba Serikali kuangalia upya mfumo wa utoaji wa mikopo ya elimu ya juu, akieleza kuwa baadhi ya wanafunzi hukosa mikopo au hupata kiasi kisichokidhi mahitaji yao.
Aidha, baadhi ya wanafunzi wa chuo hicho wameiomba Serikali kuliangalia kwa jicho la pili suala la ajira, wakieleza kuwa idadi kubwa ya wahitimu hukaa majumbani kwa muda mrefu wakitafuta ajira, licha ya juhudi na gharama kubwa zinazotumika na wazazi katika kugharamia elimu yao.
