Wataalam sekta ya ardhi waoneshwa fursa Dira 2050

Dar es Salaam. Washauri wabobezi, wanataaluma na walimu wastaafu katika sekta ya nyumba, ardhi na makazi wameelezwa watahitajika zaidi kuelekea utekezaji wa Dira 2050 na kutakiwa kujiandaa kwa hilo kuanzia sasa.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Desemba 17, 2025 na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dk Tausi Kida kwenye mkutano wa umoja wa wahitimu wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) uliofanyika chuoni hapo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa  uwasilishaji wa mada yake uliyojikita katika utekelezaji wa Dira 2050, Dk Tausi ambaye alikuwa mgeni rasmi amesema uhitaji wa wanataaluma huo unatokana na kuwepo kwa mahitaji makubwa ya makazi bora ya bei nafuu ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kimazingira.

“Tunategemea ifikapo mwaka 2050 kwa mujibu wa takwimu za Ofisi ya Takwimu (NBS) kutakuwa na Watanzania milioni 118, maana yake uhitaji wa nyumba na makazi utakuwa mkubwa kwa kuwa ongezeko la watu ni fursa pia,” amesema Dk Tausi.

Katibu huyo amesema kwa kutambua umuhimu wa rasilimali hiyo, katika dira hiyo nguzo ya tatu, kipaumbele cha nne kinaeleza kama rasilimali muhimu inayotoa fursa kwa ajili ya kilimo, viwanda, makazi na shughuli nyingine za kiuchumi.

“Kwa kutambua hili, katika dira hiyo yamo matarajio mbalimbali ikiwamo kuwa na nchi iliyopangwa na kuwekwa wazi matumizi ya ardhi yakiwamo ya makazi, kilimo, mifugo, viwanda na hifadhi ukizingatia hadi sasa tuna ukubwa ardhi takribani kilometa za mraba milioni moja.

“Hivyo ukiangalia haya, kunahitajika kuwa na usimamizi bora wa ardhi unaoongozwa na nguvu ya soko la ardhi, mali isiyohamishika na huduma ili kuvutia uwekezaji unaotegemea ardhi na mafanikio haya yote yanategemea mshikamano wa dhati wa kila Mtanzania,” amesema Dk Tausi.

Makamu Mkuu wa ARU, Profesa Evaristo Liwa, amesema mkutano huo ni mara 14 kufanyika ambapo wamekuwa wakiwaalika wataalamu mbalimbali kutoa mada.

Profeaa Liwa amesema malengo ya mwaka huu kumuita Katibu Mkuu huyo ni kuondolewa shaka na kueleweshwa zaidi yaliyopo kwenye dira hiyo ili nao kama wadau waone namna gani watashiriki kuitekeleza.

“Tunashukuru tumeelezwa kuwa tunahitajika sana katika utekelezaji wa jambo hilo, hivyo kazi kwetu kujipanga kuhakikisha hilo linawezekana kwani hatutakuwa tunaiunga mkono Serikali bali kuwasaidia wananchi pia,”amesema Makamu huyo.

Pia, amesema aliyozungumza Katibu huyo na michango itakayotolewa katika mkutano huo kutasaidia katika uboreshaji wa mitalaa yao ya ufundishaji.

Naye  mtaalamu na kiongozi mwandamizi na uchumi wa milki kuu, Andrew Kato, amesema changamoto zilizopo katika sekta ya ujenzi bado hakuna ushirikiano wa karibu wa wataalamu hao huko mtaani hivyo kila mtu kufanya mambo kivyake na mwisho wa siku anayeumia ni mwananchi wa kawaida ambaye jengo lake litakuwa halijajengwa kitaalamu.

Mtaalamu wa mipango Miji Mjini, Mariam Mwampose amesema kuna haja ya wahitimu kubadilika kutoka kwenye kujenga badala yake wanunue nyumba na kueleza hii inatokana na watu wengi hasa wenyeji kuhamia pembezoni mwa miji, hivyo kuwaongezea ugumu wa maisha ikiwamo katika suala la usafiri wanapokwenda kwenye shughuli zao za utafutaji.

“Kutokana na kukua kwa miji, Serikali imekuwa ikiwekeza miradi mikubwa na ya kisasa kama ule wa mabasi yaendayo haraka (BRT), lakini bado kwa baadhi wanaopanda usafiri huo wakifika mwisho wa vituo wanachukua usafiri mwingine kufika majumbani kwao na hivyo kutokuwa na faida kwao zaidi kuwafaidisha wageni,” amesema Mariam.

Mhadhiri wa ARU, Profesa Wilbert Kombe amesema shida ya wananchi kutoweza kununua nyumba mjini ni umasikini huku wengi wanaojenga huwachukua hadi miaka 30 kumaliza nyumba zao.

Mtaalam wa upimaji ardhi na ramani Christina Mshana, amesema kuna haja ya Serikali kuwa na mipango miji inayoendana na wakati wa sasa ili kuepusha migogoro ya ardhi kati ya  wakulima na wafugaji pia.

Zakaria Ngeleja, Mtaalamu wa Mipango Miji, alitaka kuwepo kwa urahisi wa upatinaji wa taarifa za kijiographia kwa kuwa suala mipango miji kwa kiasi kikubwa  linagegemea sana hilo.