Watu watano wamefariki dunia, wakiwemo askari wawili wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa Mbeya, na wengine tisa wamejeruhiwa, wakiwemo wanafunzi, katika ajali ya barabarani iliyotokea saa 12:15 jana Desemba 16, 2025 jioni.
Taarifa ya Polisi Mkoa wa Songwe iliyotolewa leo Jumatano Desemba 17, 2025 imeeleza kuwa ajali hiyo ilitokea eneo la Karasha, Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe, kwenye Barabara Kuu ya Mbeya–Tunduma.
Ajali hiyo ilihusisha gari aina ya Mitsubishi Canter, mali ya Security Group of Africa (SGA) Tawi la Mbeya, lililokuwa likitokea Tunduma kwenda Mbeya likiwa na askari Polisi wawili waliokuwa wakisindikiza fedha; pamoja na pikipiki aina ya Fekon na gari aina ya Toyota Coaster lililokuwa likitokea Mbeya kwenda Tunduma.
Taarifa hiyo ya Polisi imewataja waliofariki dunia kuwa ni askari H.7042 CPL Chirungu Misango John na WP.15582 PC Amina Japhari Hamisi.
Mbali na askari hao wa Polisi Mkoa wa Mbeya, katika ajali hiyo watu wengine watatu walifariki dunia, huku wengine tisa (9) wakijeruhiwa na kupelekwa hospitalini kwa matibabu.
Wengine waliofariki ni Adam Martin (38), dereva wa Toyota Coaster; dereva wa pikipiki ambaye jina lake halijafahamika, pamoja na abiria wake ambaye pia hajafahamika.
Aidha, majeruhi katika ajali hiyo ni Mariam Charles Kipangula (30), mkazi wa Mlowo; Getruda Mndulo (20), mkazi wa Chimbuya; MG.291715 Shukrani Nduka (40), mlinzi wa SGA, mkazi wa Mbeya; Gadi Myegeta (46), kondakta wa Coaster, mkazi wa Mbeya, na Mariam Ramadhani (37), mkazi wa Mbeya.
Wengine ni Orines Ngoda (14), mwanafunzi wa kidato cha pili, Shule ya Sekondari Joy Girls, Tukuyu; Hosea Ngoda (7), mwanafunzi wa darasa la pili, Shule ya Msingi Julius, mkazi wa Mbeya; Samwel Mbeyela (42), dereva wa Canter, mlinzi wa SGA, na mwanamke ambaye hajafahamika anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 28 hadi 31.
Polisi wamesema uchunguzi wa awali umebaini chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa Coaster, aliyegonga pikipiki iliyokuwa mbele yake, kisha kupoteza mwelekeo na kugongana uso kwa uso na gari Canter, hali iliyochangiwa na mwendo kasi katika eneo la makazi ya watu.
“Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe linatoa wito kwa madereva wote kuzingatia sheria za usalama barabarani, hususan kuepuka mwendo kasi na kuzingatia alama, michoro na kanuni za usalama barabarani,” imeeleza taarifa hiyo.
Aidha, imesisitiza madereva kuendesha kwa tahadhari katika maeneo ya makazi ya watu, ikitambua kuwa utii wa sheria ni msingi wa kulinda maisha ya watumiaji wote wa barabara.
