Waziri Mchengerwa auongoza ujumbe wa Tanzania kwenye uzinduzi wa mkutano wa pili wa Dunia wa Tiba Asili

Na John Mapepele, New Delhi

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Omary Mchengerwa leo ameuongoza ujumbe  wa Serikali ya Tanzania katika uzinduzi wa Mkutano wa pili wa dunia wa Tiba Asili unaoratibiwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwenye ukumbi wa kimataifa wa  Bharat Mandapam jijini New Delhi  India.

Mhe. Mchengerwa  amepongeza  juhudi  zinazofanywa na  WHO za  kuileta  dunia pamoja ili kujadili suala  la Tiba  Asili  na kupata  ufumbuzi katika  masuala kadhaa  ikiwa ni pamoja  na

utawala na udhibiti wa tiba asili, utafiti na ushahidi wa kisayansi, ujumuishaji wa tiba asili  katika mifumo ya afya, matumizi endelevu  ya raslimali za kiasili na uendelezaji wa raslimali watu kwenye eneo la Tiba Asili.

Mkutano huo umefunguliwa rasmi na Mheshimiwa Prataprao Ganpatrao Jadhav, Waziri wa Nchi (Independent Charge), Wizara ya Tiba Asili (AYUSH), na Waziri wa Nchi, Wizara ya Afya na Ustawi wa Familia ya Serikali ya India, mbele ya Mheshimiwa Jagat Prakash Nadda, Waziri wa Afya na Ustawi wa Familia wa Serikali ya India. Hafla hiyo imewakutanisha Mawaziri, watunga sera wakuu, na wadau wa sekta ya afya kutoka mataifa mbalimbali duniani.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus akitoa  hotuba  yake kwa njia ya video  kwenye ufunguzi  huo amewasihi wajumbe wa mkutano  huo  kujadili kwa kina  mada mbalimbali ili kubadilishana  uzoefu na kwamba  kwa  sasa  Tiba Asili bado itaendelea kuwa  na  mchango  mkubwa kwa wanadamu kwa kuzingatia kuwa  tiba asili ni sehemu ya  tamaduni za watu katika mataifa yao.  

Pembezoni mwa mkutano huo, Tanzania inatarajia kusaini Hati mbili za Makubaliano (MoU) na Serikali ya India kuhusu ushirikiano katika sekta ya afya na tiba asilia (Ayurveda), hatua itakayosaidia kuimarisha ushirikiano wa kitaasisi, kuongeza uwezo wa rasilimali watu, na kuimarisha matumizi salama ya tiba asilia nchini.

Kusainiwa kwa hati hizi mbili za makubaliano ni hatua muhimu kwa Tanzania, kwani kutaimarisha ushirikiano wa kitaasisi na India katika maeneo ya kipaumbele ya sekta ya afya, kuongeza uwezo wa rasilimali watu wa sekta ya afya, kuimarisha udhibiti na matumizi salama ya tiba asilia, pamoja na kuchangia jitihada za Serikali katika kuimarisha mifumo ya huduma za afya na kufikia Bima ya Afya kwa Wote.

Ushiriki wa Tanzania katika mkutano huu unaakisi dhamira ya Serikali kupitia Wizara ya Afya katika kukuza tiba asilia salama, yenye ushahidi wa kisayansi na inayosimamiwa kwa misingi madhubuti ya udhibiti, sambamba na kuendeleza ushirikiano wa kimataifa kwa maendeleo endelevu ya afya kwa watu wote.

Mkutano huo wa siku tatu unatarajiwa kufungwa na Desemba 19, 2025 na  Waziri Mkuu wa India, Mheshimiwa Narendra Modi, jambo linaloonesha uzito na umuhimu mkubwa wa mkutano huo katika ngazi ya juu ya kisera.