-Aelekeza Mikoa yote nchini kusikiliza kero na kusimamia miradi ya maendeleo
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI) Mhe. Prof. Riziki Silas Shemdoe ametoa Pongezi kwa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwa programu yake ya usikilizaji na utatuzi wa kero za wananchi, akiagiza Mikoa mingine kufanya hivyo kama sehemu ya utekelezaji wa Maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Prof. Shemdoe amebainisha hayo leo Jumatano Disemba 17, 2025 alipokutana na kuzungumza na Mkuu wa Mkoa wa Arusha CPA Amos Gabriel Makalla, Jijini Arusha, akimpongeza pia kwa namna ambavyo ameendelea kuhakikisha kuwa Arusha inabakia salama na tulivu ili kuruhusu shughuli za kiuchumi na kijamii kuweza kuendelea.
“Niwapongeze kwa kazi kubwa na nzuri mnayoifanya. Nimefuatilia na kufarijika na kazi ya juzi ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi na hili ni suala ambalo tunatakiwa tulitekeleze kama alivyoelekeza Mhe. Rais kwamba tujitahidi kusikiliza wananchi na kile ulichokifanya umetafsiri maelekezo ya Mhe. Rais na Waziri Mkuu na hii ni faraja sana na ndiyo kile tunachosema turejeshe tabasamu kwa wananchi, tuwasikilize na kutatua kero zao.”
Kwa upande wake Mhe. Makalla awali ameeleza kuwa Mkoa wa Arusha ni salama na tulivu, shughuli za kiuchumi na kijamii zikiendelea kama kawaida sambamba na Mkoa kuendelea kutekeleza kikamilifu maelekezo ya serikali kuu kwa vitendo, akimpongeza Mhe. Waziri Shemdoe pia kwa kuteuliwa kwake kuiongoza TAMISEMI, akisema ni matumaini yake kuwa kwa uzoefu na umahiri wake wataweza kuwatumikia vyema wananchi na kuilinda vyema imani ya Rais Samia katika kuwatumikia wananchi.

