Dar es Salaam. Tanzania iko katika nafasi nzuri ya kutengeneza fedha za kigeni ikiwa itawekeza zaidi katika uzalishaji wa mawese kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.
Hiyo ni baada ya bei yake katika soko la dunia kufikia Sh2.583 milioni kwa tani moja ya ujazo Oktoba mwaka huu.
Ongezeko hili la bei limeshuhudiwa kuanzia Juni mwaka huu ambapo tani moja ya ujazo iliuzwa Sh2.322 milioni ikiwa ni ongezeko kutoka Sh2.253 milioni iliyokuwa ikiuzwa Mei mwaka huu.
Ongezeko hili linatajwa kuchangiwa na kukua kwa mahitaji ya mafuta hayo katika nchi za Asia.
Ripoti ya tathmini ya uchumi ya kila mwezi ya Benki kuu ya Tanzania (BoT) ya Novemba mwaka huu inasema ongezeko la mahitaji sokoni lilishuhudiwa licha ya kuongezeka kwa uzalishaji nchini Malaysia na Indonesia.
Takwimu za bodi ya Mafuta ya Mawese za Malaysia zinaonyesha kuwa uzalishaji katika nchi hiyo uliongezeka kutoka tani milioni 1.69 Juni mwaka huu hadi kufikia tani 2.04 milioni Oktoba mwaka huu.
Ikiwa inasimama kama nchi ya pili duniani katika uuzaji wa mafuta hayo katika masoko la nje wamelenga kufikia uzalishaji wa tani milioni 20 wanapokamilisha mwaka huu.
Hilo linashuhudiwa wakati ambao Indonesia inatajwa kuzalisha wastani wa tani milioni 30 za mawese kila mwaka zinazochangia asilimia 4.5 katika pato la taifa huku ikizalisha ajira kwa watu Zaidi ya milioni 3.
“Mawese tu ya kutumia huku ndani ukiwa unahitaji kwa wingi labda tani moja utachukua muda kuyapata maana utalazimika ukusanye kidogokidogo, kama tumetambua kuwa na soko tungeyaweka mafuta haya mfumo mzuri,” amesema Salum Mhaganamilwa muuzaji wa mawese.
Amesema jambo hilo limekuwa likimuathiri kama mfanyabiashara kwani amekuwa akilazimika kuongeza muda wa ziadi kila anapoagiza mzigo ili kuhakikisha haishiwi bidhaa.
“Kungekuwa na soko la jumla kwenye baadhi ya maeneo yanayozalisha sana na linasimamiwa vizuri tungeiona faida, mtu awe anajua nikitaka mawese mengi nayapata sehemu Fulani na bei elekezi ni hii tofauti na sasa. Pia wakulima wawezeshwe miche ya muda mfupi ili uzalishaji uimarike,” amesema.
Hata hivyo, fursa hii haipo kwa wauzaji wa mafuta hayo pekee kwani hata wanaotumia mbegu zilizo ndani ya ngazi zijulikanazo kama mise watakuwa miongoni mwa wanufaika ikiwa uzalishaji utaongezeka zaidi.
Kadri uzalishaji utakavyokua, ndivyo watapata malighafi zaidi baada ya kukamuliwa kwa mawese ili waweze kutengeneza bidhaa zao.
Mjasiriamali Andrew Mpambazi ni mmoja kati ya wanaotumia mise kutengeneza sabuni na mafuta ambao watakuwa ni wanufaika wa moja kwa moja uzalishaji mawese unapoongezeka.
“Nilishindwa kutumia mawese kwa sababu wanaoyahitaji ni wengi na yanakuwa na bei kubwa ukiyapata ndiyo maana nikaona nitumie mise kwa sababu wanaoitumia ni wachache ila bado tunategemea uzalishaji wa zao la chikichi,” amesema.
Licha ya kuwa na uzoefu katika eneo hilo lakini anakiri kuwa bado hajawaza kuingia katika biashara ya kuuza mawese licha ya kuwapo kwa soko la uhakika huku akisubiri biashara yake ya awali ikue Zaidi.
Haya yanasemwa wakati ambao takwimu za wizara ya kilimo zinaonyesha kuwa uzalishaji wa zao la mafuta la chikichi ulifikia tani 51,834.42 katika mwaka 2024.
Kuhusu mwenendo huo, mtaalamu wa uchumi Dk Lutengano Mwinuka amesema chikichi ni kama zao linalosahaulika kwani haliangaliwi kwa umakini mkubwa wakati ambao linabeba umuhimu katika matumizi ya ndani.
Amesema kwa muda mrefu imekuwa ikiendelea kuagiza mafuta wakati ambao mawese yangeweza kutumika kuziba pengo hilo.
“Jitihada zianzie katika uzalishaji kwa kuangalia mashamba ya mchikichi yenyewe kuhakikisha yanazalisha kwa tija tuwe na teknolojia nzuri ya uvunaji, kuongeza thamani, mafuta yawe mengi na yasindikwe kwa ajili ya kupata kwa ajili ya matumizi ya matumizi ya soko la ndani na nje,” amesema Dk Mwinuka.
Amesema jitihada hizo ziende sambamba na kuunganisha wakulima na wadau wengine katika mnyororo wa masoko jambo linalobeba maana kubwa ikiwemo kuunganisha mikoa inayolima Zaidi zao hilo na mikoa mingine ya karibu, nchi Jirani na za mbali.
“Soko la nje ni fursa lakini la ndani pia lipo. Ni vyema kuangalia soko lipi litalipa zaidi, wakulima wakipata soko la nje hasa la mtu anayetaka kununua mzigo mkubwa ni jambo zuri lakini ni vyema kuangalia namna ya kuongeza uzalishaji kwani nchi inayo maeneo ya kutosha,” amesema.
Katika bajeti ya wizara ya kilimo ya mwaka 2025/2026, Tanzania imepanga kuhamasisha wakulima kuongeza uzalishaji wa mazao ya mafuta kutoka tani 2,181,747.65 mwaka 2023/2024 hadi tani 2,200,000 mwaka 2025/2026. Lengo hilo litafikiwa kwa kutekeleza yafuatayo.
Kusambaza mbegu bora za alizeti tani 2,150 kwa wakulima kwa mpango wa ruzuku, uzalishaji na kusambaza miche ya chikichi 10,000,000 kwa wakulima katika maeneo ya uzalishaji. Mauzo ya nje.
Wakati mawese yakifanya vizuri katika soko la duni, Mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi yaliongezeka hadi dola za Marekani 17.048 bilioni katika mwaka unaoishia Oktoba 2025 ikilinganishwa na dola za Marekani 15.133 bilioni katika kipindi kama hicho cha mwaka 2024.
Mauzo ya bidhaa nje ya nchi yalifikia dola za Marekani 10.13 bilioni ikilinganishwa na dola za Marekani 8.461 bilioni kipindi kama hicho mwaka 2024. Ongezeko hili lilichangiwa na mauzo ya dhahabu, bidhaa za viwandani, tumbaku, korosho na kahawa.
Mauzo ya dhahabu pekee yaliongezeka kwa asilimia 38.9 hadi Dola za Marekani 4.596 bilioni kutoka Dola za Marekani 3.308 bilioni ikichangiwa zaidi na kuongezeka kwa bei ya dhahabu kwenye soko la dunia.
Mauzo ya bidhaa asilia nayo yalifika dola za Marekani 1.438 bilioni sawa na ongezeko la asilimia 25.2. Ongezeko hili lilichangiwa zaidi na mauzo ya tumbaku na korosho sambamba na mabadiliko ya bei na kiasi kilichouzwa.
Mauzo ya nafaka, hususan mahindi na mchele, yaliongezeka kufikia dola za Marekani 312.5 milioni kutoka dola za Marekani 221.6 milioni, kutokana na ongezeko la mahitaji nchi jirani.
Kwa mwezi wa Oktoba 2025, mauzo ya bidhaa nje ya nchi yaliongezeka hadi dola za Marekani 949.2 milioni mwaka 2025, kutoka dola za Marekani 928.3 milioni Oktoba 2024, hali iliyochangiwa na ongezeko la mauzo ya dhahabu na bidhaa za viwandani.
Mauzo ya huduma yaliongezeka kufikia Dola za Marekani 6.91 bilioni kwa mwaka ulioishia Oktoba 2025, kutoka dola za Marekani 6.672 bilioni mwaka uliotangulia. Ongezeko hili lilitokana na kuongezeka kwa mapato kwenye huduma za usafiri na utalii.
Ongezeko la mapato kwenye huduma za kitalii linaashiria ukuaji thabiti wa sekta hii, huku idadi ya watalii ikiongezeka kwa asilimia 11.4 hadi kufikia watalii 2,324,387.
Aidha, mapato yatokanayo na shughuli za usafirishaji, hususan mizigo, yalifikia dola za Marekani 2.47 bilioni ikilinganishwa na Dola za Marekani 2.26 bilioni mwaka ulioishia Oktoba 2024.
Kwa mwezi Oktoba 2025, mapato ya huduma yalikuwa Dola za Marekani milioni 543.2 milioni, yakiwa chini ya Dola za Marekani 606.2milioni katika mwezi Oktoba 2024.