Kampuni ya Buckreef Gold imezidi kuimarisha ushirikiano wake na Halmashauri ya Wilaya ya Geita kupitia makubaliano ya Uwajibikaji kwa Jamii yenye thamani ya TZS 600,000,000, yanayo lenga kuboresha huduma za afya, elimu, maji na usafi wa mazingira kwa jamii zinazoishi maeneo yanayo zunguka mgodi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martine Shigella, aliipongeza kampuni ya Buckreef Gold kwa namna inavyo tekeleza maendeleo ya jamii kwa nidhamu na kwa kuzingatia sheria. “Buckreef imeonyesha umakini katika kutekeleza wajibu wake kwa kupanga, kutenga bajeti na kutekeleza miradi yake ya Uwajibikaji kwa Jamii kwa kuzingatia matakwa ya serikali. Muhimu zaidi ni jamii kuona matokeo ya wazi na ya kudumu kupitia maendeleo ya shule, vituo vya afya na huduma za maji zinazo boresha maisha ya kila siku.”
Maeneo ya uchimbaji madini mkoani Geita yanaendelea kushuhudia ongezeko kubwa la idadi ya watu kutokana na shughuli za kiuchumi kuvutia wafanyakazi na familia. Katika kata kama Rwamgasa, ambako idadi ya watu inazidi wakazi 60,000, huduma za umma zinaendelea kuwa chini ya shinikizo. Zahanati zinahudumia wagonjwa wengi kuliko uwezo wake. Shule zinafanya kazi zikiwa na uhaba wa vyumba vya madarasa na miundombinu ya vyoo. Upatikanaji wa maji safi bado ni changamoto ya kila siku kwa kaya, shule na vituo vya afya.
Ni ndani ya uhalisia huu ndipo mpango wa sasa wa Uwajibikaji kwa Jamii umebuniwa.
Katika sekta ya elimu, ujenzi wa madarasa na vyoo haujibu tu mapengo ya miundombinu. Unaondoa mazingira ya kujifunzia yasiyo salama, unapunguza msongamano na kurejesha heshima kwa wanafunzi. Madarasa mapya katika shule ya msingi Isunganghoro na uboreshaji wa miundombinu katika shule ya msingi Lubanda vitawawezesha watoto kusoma katika mazingira salama na yenye afya zaidi, hivyo kusaidia mahudhurio na matokeo ya elimu ya muda mrefu.
Katika sekta ya afya, uwekezaji katika zahanati za Rwamgasa, Lubanda na Ibisabageni unajibu moja kwa moja ongezeko la mahitaji ya huduma. Ujenzi wa majengo ya wodi, nyumba za watumishi, mifumo ya maji na miundombinu ya vyoo unalenga kuboresha huduma kwa wagonjwa huku ukiwaimarisha wahudumu wa afya wanaozihudumia jamii hizi. Kuwepo kwa makazi ya watumishi karibu na zahanati kunaimarisha uendelevu wa huduma na kuboresha mwitikio wa dharura.
Miradi ya maji na usafi wa mazingira, ikiwemo kisima cha maji safi katika zahanati ya Lubanda, ni suluhisho la moja ya mahitaji muhimu zaidi katika eneo hili. Upatikanaji wa uhakika wa maji safi husaidia kudhibiti maambukizi, kuimarisha huduma za wakina mama na mtoto, pamoja na usafi wa msingi hasa wakati wa kiangazi ambapo upungufu wa maji huwa mkubwa zaidi.
Meneja mkuu wa kampuni ya Buckreef Gold, Bw. Isaac Bisansaba, alisema kampuni inaona kuboresha huduma za jamii kama jukumu la msingi ili kuboresha maisha ya wananchi waliozunguka mgodi. “Shughuli zetu zinafanyika ndani ya jamii halisi. Kadri uzalishaji unavyoongezeka, ndivyo wajibu wetu kwa jamii hizo unavyoongezeka. Miradi hii inalenga afya, elimu na maji kwa sababu hapo ndipo athari chanya huhisiwa moja kwa moja na familia.”
Zaidi ya miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii , Buckreef Gold pia inachangia maisha ya uchumi wa kila siku Geita kupitia ajira na ununuzi wa bidhaa na huduma ndani ya nchi. Ajira mgodini huziwezesha familia kukidhi mahitaji, kuendeleza elimu na kuimarisha ustawi wa kaya, huku ununuzi kutoka kwa biashara za Tanzania ukiwapa wasambazaji wa ndani fursa ya kukua, kuwekeza na kuzalisha ajira zaidi. Kwa pamoja, manufaa haya ya kiuchumi yanaendana na miradi ya jamii, yakihakikisha uwepo wa mgodi unatafsirika kuwa thamani inayoonekana na ya kudumu kwa mkoa.
Mwaka uliopita, Buckreef Gold iliwekeza TZS 420,000,000 katika miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii , ikiwemo ujenzi wa madarasa yaliyobadilisha miundombinu isiyo salama kuwa salama, ukamilishaji wa vituo vya afya na kazi za barabara zilizoboresha upatikanaji kati ya vijiji wakati wa msimu wa mvua.
Tangu kuanza kwa shughuli za mgodi, jumla ya TZS 1,860,300,000 zimewekezwa katika miradi ya maendeleo ya jamii kote Geita. Miradi mingi kati ya hiyo inaendelea kuhudumia maelfu ya wakazi, kupunguza shinikizo kwa huduma za umma na kuimarisha miundombinu ya kijamii.
Kupitia makubaliano haya mapya ya Uwajibikaji kwa Jamii, Buckreef Gold inaendelea kuonyesha kuwa uchimbaji madini unaowajibika unajengwa juu ya watu, ushirikiano na vitendo vya msingi vinavyoleta matokeo na kutoa thamani ya kudumu kwa jamii za Geita.
Mgodi wa Buckreef Gold unaendeshwa kupitia ubia kati ya TRX Gold Corporation na STAMICO, shirika la madini la serikali ya Tanzania. Muundo huu unaunganisha utaalamu wa kimataifa wa uchimbaji madini na ushiriki wa moja kwa moja wa Serikali, hivyo kuhakikisha uwekezaji wa jamii unaendana na vipaumbele vya kitaifa na mipango ya maendeleo ya wilaya.






