CAG aanza mkakati wa kitaifa kuwanoa madiwani wamo waandishi wa habari

Kibaha. Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), imeanza utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa kuwajengea uwezo madiwani na waandishi wa habari nchini, hatua inayolenga kuimarisha usimamizi wa miradi ya maendeleo na uwajibikaji wa matumizi ya fedha za umma katika halmashauri.

Akizungumza kuhusu mkakati huo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya CAG, Focus Mauki amesema Ofisi ya CAG iko mbioni kuanza kutoa elimu kwa madiwani wa mabaraza ya halmashauri nchini, ili kuwawezesha kusoma, kuchambua na kufuatilia utekelezaji wa ripoti hizo za ukaguzi.

Amesema madiwani wana nafasi kubwa katika kusimamia rasilimali za umma, hivyo kuwajengea uelewa wa ripoti za CAG kutasaidia kuimarisha uwajibikaji katika serikali za mitaa.

Mauki amesema mkakati huo ni wa kitaifa na unalenga kuwafikia madiwani wote nchini kwa awamu.

Akifungua mafunzo hayo leo Alhamisi, Desemba 18, 2025, Kaimu Mkaguzi Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Angela Chimagai amesema Serikali inatambua umuhimu wa waandishi wa habari katika kufikisha taarifa sahihi kwa wananchi, hivyo imeona kuna umuhimu wa kuwaongezea uelewa zaidi.

Chimagai amesema mpango huo ni sehemu ya dira ya Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ya kuimarisha uwazi na ushiriki wa wadau katika mchakato wa ukaguzi wa fedha za Serikali.

Amesema waandishi wa habari ni kiungo muhimu kati ya ripoti za CAG na wananchi, hivyo kuwajengea uwezo wa kuandika kwa usahihi kutasaidia jamii kupata taarifa sahihi na zisizopotosha.

“Tunataka waandishi wa habari waelewe majukumu ya CAG, mipaka yake ya kisheria na matumizi sahihi ya ripoti za ukaguzi,” amesema Chimagai.

Katika mafunzo hayo, waandishi wa habari wamefundishwa misingi ya ukaguzi wa serikali, sheria na kanuni zinazoongoza Ofisi ya CAG pamoja na aina mbalimbali za ripoti za ukaguzi.

Mmoja wa wakufunzi, Mary Digogo amesema jukumu la Ofisi ya CAG ni kukagua na kutoa mapendekezo, huku hatua za kisheria dhidi ya ubadhirifu zikichukuliwa na taasisi nyingine ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Baadhi ya waandishi wa habari walioshiriki mafunzo hayo, wamesema elimu hiyo itaongeza uelewa wa umma kuhusu ripoti za ukaguzi na kuchochea uwajibikaji katika ngazi za halmashauri.