Chama la Wana laanza kujipata Ligi ya Championship

STAND United ‘Chama la Wana’ imeanza kunyanyuka taratibu na kupanda juu katika msimamo wa Ligi ya Championship baada ya kupitia changamoto mbalimbali ikiwamo ukata na kupokwa pointi na Bodi ya Ligi, hii imetokana na ushindi wa bao 1-0 nyumbani dhidi ya Barberian FC.

Ushindi huo uliopatikana juzi katika mechi ya Ligi ya Championship kwenye Uwanja wa Kambarage, mjini Shinyanga umeifanya timu hiyo kufikisha pointi saba baada ya mechi 10 za ligi hiyo inayotoa timu za kupanda Ligi Kuu zikiwamo mbili za moja kwa moja na ile inayovizia kupitia play-off.

Awali, katika mechi tano za kwanza, Stand United ilikuwa inashika mkia katika nafasi ya 16 ikiwa haijashinda wala kupata sare katika mchezo wowote, huku ikiwa inadaiwa alama tatu (-3), ikifunga mabao mawili na kuruhusu 12.

Lakini, kwa sasa baada ya michezo 10, timu hiyo inakamata nafasi ya 12 ikikusanya alama saba, huku ikishinda mechi tatu, sare moja, na kupoteza sita, huku ikifunga mabao sita na kuruhusu 14.

Licha ya mabadiliko hayo, kocha wa Stand United, Feisal Hau amesema bado kikosi chake hakina umakini katika eneo la umaliziaji wa nafasi wanazotengeneza katika michezo yao, huku akiahidi kulishughulikia tatizo hilo mazoezini.

“Kila mechi tunapata nafasi nyingi na sisi benchi la ufundi tunaendelea kujitahidi kuboresha kuzitumia zile nafasi kuwa magoli, lakini bado labda vijana wangu wana presha kutokana na nafasi tuliyopo, lakini naamini tutarudi kwenye uwanja wa mazoezi tutajitahidi tuone mechi zinazokuja zinakuwaje,” amesema Hau.

Kocha huyo wa zamani wa Copco FC, amesema ushindi huo umewapa hali ya kujiamini ambayo itakuwa faida kwao katika mchezo ujao Jumapili dhidi ya Gunners FC, huku akiomba sapoti ya mashabiki wa mkoa wa Shinyanga.

“Naamini kwa matokeo ya mechi hii wachezaji wangu watakuwa wamepata hali ya kujiamini na motisha ya kupambana, hivyo kwa uwezo wa Mungu mechi ya Gunners tutatulia tutapata matokeo,” amesema Hau na kuongeza;

“Tunawaambia mashabiki wetu waendelee kutusapoti waje, tumeanza kutoka chini taratibu naamini kabisa uwepo wao ni nguvu kwetu na kwa wachezaji, Jumapili bila shaka tutaendeleza wimbi la ushindi.”