Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba ameagiza watendaji wa Serikali kuzishughulikia kwa wakati changamoto zote zinazowasilishwa na wananchi badala ya kuwapiga danadana.
Dk Mwigulu ametoa kauli hiyo leo, Alhamisi Desemba 18,2025 wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uyole, jijini Mbeya katika ziara yake kikazi, akitokea mkoani Songwe.
“Umezuka utaratibu wa kujua huyu ni mama, huyu mjane, huyu ni mzee au huyu yatima, ambaye akifikisha jambo lake anapigwa danadana hadi anaishiwa nauli ya kulifuatilia,” amesema Dk Mwigulu.
Dk Mwigulu amesema maelekezo ya Serikali, kama mwananchi amefikisha jambo Serikali na kiongozi husika hana majawabu, mtendaji huyo, anatakiwa kulipeleka ngazi ya juu kisha kumpa mrejesho mwananchi.
“Mbona walimu hawatumi wanafunzi kupeleka fomu kwenye ofisi ya elimu mkoa au Taifa? Kwa nini hizi ofisi zingine tunataka mwananchi ndio afuatilie yeye jambo langu hadi makao makuu?
“Hatukuanzisha ofisi kila maeneo ili kugawana vyeo, ugatuaji wa madaraka unataka mwananchi asogezewe huduma pale alipo,” amesisitiza.
Sababu za Dk Mwigulu kueleza hayo, ni baada ya mkazi wa Mbeya, kusema aliingia ubia na mtu mmoja aliyekarabati nyumba yake na makubaliano walipane kwa njia ya kodi.
“Kweli alikuwa anachukua kodi, lakini ilifika wakati Tanroads, (Wakala wa Taifa wa Barabara Tanzania) wanapita kwa ajili ya upanuzi wa barabara na wakasema wanafanya tathimini ya nyumba hiyo kwa ajili ya fidia. Sisi tukapiga thamani ya ardhi, yeye gharama za kukarabati.”
“Lakini cha kushangaza fedha zote alichukua yule kijana (aliyekarabati) sisi hatukupewa. Tuliambulia Sh400,000, wakati yule kijana alichukua Sh40 milioni,” amesema mkazi huyo.
Hata hivyo, mkazi huyo amesema hata walipokwenda mahakamani hakimu alishangaa kupata kiasi hicho kidogo cha fedha tofauti na aliyekarabati.
“Tukaamua kwenda Tanroads waliotuambia hayo mambo hayawahusu bali wapo viongozi wa Serikali hukohuko, nikasema sawa. Tulikwenda ofisi za Serikali za chini walituzungusha sana… hadi leo nilipomuona Waziri Mkuu nikajieleza,” ameeleza.
Kwa mujibu wa mama huyo, “kijana huyu ana kiburi cha kutosha na ananiambia nina wivu, sasa watu wanamuuliza hizo fedha ameokota barabarani, si amechukua kwenye nyumba yangu?
Kutokana sakata hilo, Dk Mwigulu ameagiza mtu huyo aliyepokea fedha hizo, kesho Ijumaa Desemba 19, 2025 kujisalimisha ofisi ya katibu tawala wa Mkoa wa Mbeya, akibeba nyaraka zote alizopokea malipo.
“Kama kesho hatajisalimisha RPC (Kamanda wa Polisi wa Mkoa), mtafute popote pale mkamate, kama mwizi au tapeli mwingine yoyote na afunguliwe mashtaka,” amesema.
“Hili jambo msimzungushe mama wa watu, viongozi wa Serikali nyie ndio mnaotunza nyaraka hizi, mnaujua ukweli,” ameeleza Dk Mwigulu.
Katika mkutano huo, Dk Mwigulu ameihoji Tanroads kulipa fidia kwa mtu ambaye si mmiliki halali wa nyumba wala haisomi jina lake.
