Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amekutana na kero mbalimbali zilizowasilishwa na baadhi ya wakazi wa Mkoa wa Mbeya, zikiwamo changamoto katika mfumo wa utoaji wa haki, upatikanaji wa huduma bora za afya na maji.
Kero nyingine zilizowasilishwa ni masuala ya ardhi, mikopo, michango shuleni, ushuru na kufungwa kwa biashara.
Wananchi hao waliwasilisha hoja zao leo, Alhamisi Desemba 18, 2025, katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Kiwira, Wilaya ya Rungwe baada ya Dk Mwigulu kusimama kuzungumza na kusikiliza changamoto zao.
Wananchi hao waliwasilisha kero kwa hisia na kwa undani, huku baadhi zikipatiwa majibu papo hapo na Dk Mwigulu, huku kero nyingine akiagiza watendaji wa Serikali kuzishughulikia kwa haraka.
Licha ya mvua iliyokuwa ikinyesha mara kwa mara katika mkutano huo, wananchi walieleza kuwa, wako tayari kuvumilia hali hiyo ili kupata fursa ya kufikisha changamoto zao moja kwa moja kwa Waziri Mkuu kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi.
Mwasilishaji wa kwanza alikuwa Evelyn Brown, ambaye amemweleza Dk Mwigulu kuwa bado kuna changamoto katika upatikanaji wa dawa muhimu na za uhakika katika vituo vya afya, licha ya kuwepo kwa maboresho makubwa ya miundombinu ya majengo ya huduma za afya katika eneo hilo.
“Tunajua wajawazito na watoto, dawa ni bure hadi miaka mitano, lakini mkituambia dawa hakuna kwenye vituo vya afya tunashangaa,” amedai.
Sambamba na hilo, Brown alimweleza Dk Mwigulu kuwa, ili kupata dhamana katika baadhi ya vituo vya polisi, mara nyingi inawahitaji kuwa na Sh500,000, jambo linalozusha changamoto kwa wananchi wengi.
“Kuna watu wapo juu ya sheria wanatutesa, anakwambia anapiga simu kwa hakimu, na kutoa maelekezo kuwa huyu mtu mfungeni asirudi. Hii inatengeneza chuki katika Taifa, hawa watu wapo wanajulikana,” amedai.
Mkazi mwingine, Bashiru Matolwa amemueleza mtendaji mkuu huyo wa Serikali kuwa wanakabiliana na kero ya majisafi na salama.
Matolwa amesema eneo la Kiwira halina majisafi licha ya kuzungukwa na mito mitatu, lakini kwenye makazi ya watu hakuna huduma jambo alilodai ni aibu.
Mwingine aliyewasilisha kero ni Stella Hashim aliyekumbushia upatikanaji wa mikopo, akisema licha ya kufuata taratibu ikiwamo kuunda vikundi bado fedha hizo hawajazipata.
“Hatuna mitaji, tuliorodhesha majina, lakini hatujapata mikopo, ni muda mrefu sana hadi sasa mikopo haijafika, mheshimiwa tunaomba ulizingatie hili,” amesema.
Mbali na hilo, Hashim amesema kero nyingine ni ushuru, hata ikitokea mtu amebeba mahindi ya kula nyumbani anatozwa ushuru, akimuomba Dk Mwigulu kuwasaidia.
Kwa upande wake, Amos Mwankenja amesema, “elimu ni bure lakini michango imezidi sana. Jambo jingine ushuru watu wanakamatwa na bidhaa zao, sijui utatusaidiaje?”
Oscar Emmanuel amewasilisha kilio cha eneo la biashara (bar), kufungwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), baada ya kuelezwa kuwa ipo katika hifadhi ya barabara.
“Tunapata shida licha ya kujiwekeza, lakini kuna watu wanaingilia shughuli zetu na kufunga ofisi yetu ya bar iliyopo Tukuyu Mjini, baada ya kuambiwa ipo hifadhi ya barabara, licha ya kufuata taratibu zote zinazotakiwa,” amesema.
Kwa mujibu wa Emmanuel, katika uwekezaji huo wametumia gharama kubwa, baada ya kufungwa kuna watu zaidi ya 100 wamepoteza ajira zao.
Asha Mwakipale amesema licha ya kuambiwa kutofanya shughuli zozote za maendeleo katika eneo wanaloishi, baada ya kufanyiwa tathimini na Serikali bado wapo njia panda, kwa sababu hawajaambiwa lolote.
“Mradi wa umeme umepita katika maeneo yetu na tulithaminiwa na kuelekezwa kutofanya shughuli zozote au kuboresha shughuli za biashara.
“Hadi sasa hatujui hatima yetu tunaomba utusaidie katika hili, hatuelewi twende wapi mheshimiwa waziri mkuu,” amesema Mwakipale.
Katika majibu yake, Dk Mwigulu amesema kuwa ifikapo Januari 2026, mchakato wa bima ya afya kwa makundi ya wajawazito, watoto na wazee wasiojiweza utaanza rasmi.
Amesema mpango huo unalenga kushughulikia changamoto za upatikanaji wa huduma za afya kwa makundi haya nyeti.
Kuhusu watu kuwa juu ya sheria, Dk Mwigulu amesema, “si utaratibu wa kimaadili mtu kuelekeza mtu afungwe. Mambo ya aina hii, yaliyajitokeza ndio maana Rais Samia Suluhu Hassan aliundaTume ya Haki Jinai na moja pendekezo lililotolewa ni kupunguza kamatakamata kwenye Mahakama za mwanzo.”
Kutokana na hilo, Dk Mwigulu amesema badala ya kila mmoja kutoa maelekezo binafsi, wananchi wanapaswa kufikisha malalamiko yao kwa viongozi wa Serikali walioko karibu ili kushughulikia changamoto hizo kwa haraka.
Amesema Rais Samia tayari ametoa kauli kwamba kila kiongozi atapimwa utendaji wake kwa jinsi anavyoshughulikia kero za wananchi.
Dk Mwigulu amesema wananchi wanahimizwa kuendelea kuwasilisha changamoto zao kwa viongozi na kuhakikisha kila hatua wanayopokea inahifadhiwa kwa kumbukumbu ili kuimarisha uwajibikaji.
“Hili la mikopo kuna maeneo matatu tunayoendelea kuyafanyia maboresho, tumeipokea kero yako, hivi tunavyoongea ndani ya siku 100 kuna ahadi inayohusisha mikopo zimetengwa Sh200 bilioni,” ameeleza.
Katika hatua nyingine Dk Mwigulu ameuagiza uongozi wa Halmashauri ya Rungwe kutatua kero ya ushuru na michango shuleni, akisema lipo chini ya mamlaka zao.
Vivyo hivyo katika kero ya ardhi iliyowasilishwa na Evelyn ambapo Dk Mwigulu alimwagiza Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi kushughulikia haraka, punde msafara wake utakapoondoka Kiwira.
Kero ya mradi wa umeme kupita katika maeneo hayo ilichukuliwa na Ofisa Uhusiano wa Huduma kwa Wateja wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Tukuyu, Osward John aliyesema atalifikisha ngazi ya juu kwa utatuzi.
Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu amesema kuanzia Januari 10, 2026 walimu 7,000 na madaktari 5,000 wapya wataripoti katika vituo vyao vya kazi watakavyopangiwa.
Watalaamu hao wa sekta ya elimu na afya 12,000 ni sehemu ya ajira mpya zilizoahidiwa ndani siku 100 na Rais Samia wakati wa kampeni za kunadi sera zake katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29,2025.
Kwa sasa Wizara ya Nchi, Ofisi Rais (Utumishi na Utawala Bora), ipo katika mchakato wa usaili wa vijana waliomba nafasi hizo, ulioanza Desemba 13, Tanzania Bara na vituo mahsusi vya Pemba na Unguja.
“Ifikapo Januari 10,2026 madaktari 5,000 watakuwa katika vituo vya afya na walimu 7,000 wakiwamo wa sayansi na hesabu wataripoti katika shule hizo,” amesema.