Na Dulla Uwezo
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Kagera Mhe. Samira Khalfan amefanya Dua Maalum ya Shukrani pamoja na Kuwarehemu Wazee wake waliotangulia mbele ya Haki, ikiwa ni Siku chache tangu arejee nyumbani mara baada ya kuapishwa kuwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa Kagera.
Dua hiyo maalum imefanyika Desemba 18,2025 Nyumbani Rulenge Wilayani Ngara, ikiwa na lengo la kushukuru Mwenyezi Mungu kwa kumvusha katika mchakato mzima wa Uchaguzi tangu alipoanza mbio za kuwania kiti cha Ubunge Viti Maalum.
Akizungumza na Mamia ya waliohudhuria Dua hiyo Mhe. Samira amewashukuru Sana Wananchi wa Jimbo la Ngara na Biharamulo kwa namna walivyojitokeza kumchagua Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwamba yeye pamoja na Wabunge wa Majimbo mengine watawalipa wapiga kura maendeleo.
Aidha Mhe. Samira amewasisitiza Wananchi kuendelea kushikamana, kuoendana na kulinda Amani ili Maendeleo yaendelee kuletwa Jimboni Ngara, kwa kushirikiana na Mbunge.
Kwa Upande wake Mbunge wa Jimbo la Ngara Mhe. Dotto Bahemu ambaye amehudhuria Dua hiyo, amemshukuru Mhe. Samira kwa tendo jema alilolifanya la kushukuru kwa Dua, huku akiwakumbusha Wananchi kuwa, mara nyingi Binadamu tumekuwa wasahaulifu wa kushukuru zaidi ya kuomba, na hivyo tuwe na utamaduni wa kushukuru pale tunapotendewa mema na kubarikiwa.
Dua hiyo maalum imehudhuriwa na Viongozi Mbalimbali wakiwemo Masheikh wa Wilaya za Ngara na Biharamulo, Walimu na Maulamaa, Viongozi wa Serikali, Waheshimiwa Madiwani, Madrasa za Ngara na Biharamulo pamoja na Wananchi.






