Kariakoo ‘imechangamka’ | Mwananchi

Dar es Salaam. Haijalishi ni asubuhi, mchana au jioni, Kariakoo kwa misemo ya mtaani ‘imechangamka.’

Kila hatua ni msukumo, kila pumzi ni ushindani wa kutafuta nafasi ya kupita au kupenya ili kufanikisha lile lililokufikisha hapo.

Si msongamano wa kawaida, ni umati unaosaka mahitaji muhimu ya sikukuu za mwishoni mwa mwaka na matarajio ya mwaka mpya. Wapo wanaofanya ununuzi wa mahitaji yao binafsi na wengine kwa ajili ya kwenda kuuza maeneo mengine ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam na mikoani.

Ndani ya barabara nyembamba za mitaa ya Kariakoo, wapo wazazi wanaokokota watoto wao mkono kwa mkono, wengine wakiwa wamewabeba mgongoni, wakijaribu kuwapenyeza kati ya makundi ya wanunuzi.

Macho yakiwa mbele, wazazi hao wanahaha kulinda usalama wa watoto wao katika mazingira yasiyotabirika, ambako msukumo mmoja tu unaweza kumtenganisha mtoto na mzazi au kumuangusha chini bila huruma.

Wazazi wakiwa wameongozana na watoto wao kwa ajili ya manunuzi ya bidhaa mbalimbali katika mtaa wa Muhonda, Kariakoo, jijini Dar es Salaam

Mazingira yenyewe ni hatarishi. Kwa baadhi ya maeneo, ujenzi wa majengo mapya unaendelea.

Chini ya miguu ya wapita njia kuna msururu wa bidhaa zilizopangwa. Hapo unakuta nguo, viatu, vyakula na vifaa vya nyumbani. Zipo zilizotandazwa chini ardhini, nyingine juu ya meza na hata juu ya toroli.

Kila kona ni duka, tena limepanua mipaka yake hadi barabarani kwa kutandaza midoli ya kutangaza bidhaa zilizopo ili kuvuta macho ya wateja.

Wakati huohuo, ndani ya barabara hizohizo, shughuli za usafirishaji hazisimami. Malori na magari madogo yanashusha bidhaa katikati ya msongamano. Baadhi ya madereva wana subira, lakini wengine wanapiga honi kwa kelele ili kupata nafasi.

Pikipiki za magurudumu mawili na zile za matatu haziko nyuma, madereva wanapambana katikati ya msongamano wakihamisha mizigo kutoka upande mmoja kwenda mwingine.

Makuli nao wako kazini. Wakiwa wamebeba mizigo mizito juu ya mabega au vichwani, wanachonga njia kwa nguvu na sauti wakitafuta ujira wa siku.

Katika harakati hizo, asiye makini hujikuta akiangukia vilivyo jirani naye, iwe ni boksi, toroli au kusukumwa pembeni ili kutoa nafasi.

Hata midoli inayotumika kutangaza bidhaa haijasalimika, mingine huangushwa, hali inayozua malalamiko na vurugu za hapa na pale.

Hata hivyo, hakuna anayesimama kwa muda mrefu. Kila mmoja ana haraka ya kukamilisha ununuzi ili kujiondoa katika msongamano huo, unaoathiriwa zaidi na hali ya hewa ya joto katika kipindi hiki. Hii ndiyo Kariakoo, kitovu cha biashara mkoani Dar es Salaam.

Mwananchi limepita mitaa kadhaa ya Kariakoo leo Desemba 18, 2025, na kushuhudia ile ya Msimbazi, Congo, Uhuru na Nyamwezi ikiongoza kwa kuwa na msongamano.

Baadhi ya wafanyabiashara wanasema mazingira ya Kariakoo kwa sasa yanaweka watoto katika hatari kubwa.

Mbali na kukanyagwa, kusukumwa au kugongwa na vyombo vya usafiri kutokana na wingi wa watu, watoto wamekuwa wakipotea na kutangazwa hadi kwenye misikiti iliyo jirani.

Mfanyabiashara wa viatu, Jabir Shaka, anasema ameshuhudia matukio ya watoto kulia baada ya kupotezana na watu walioongozana nao, huku wengine wakinusurika kugongwa na maguta.

Umati wa watu wakiwa katika mtaa wa Nyamwezi, Kariakoo kwa ajili ya kupata mahitaji mbalimbali kuelekea msimu wa Sikukuu ya Christmass na Mwaka mpya 

Hali iliyopo imekuwa chanzo kwa wazazi wasio na subira kuwakaripia watoto wao wakidai hawako makini wanapotembea.

Kama hilo halitoshi, wapo wanaodiriki kuwashushia kichapo watoto wao. Kabla mtoto hajatahamaki, mara kapigwa kofi, mwingine konzi na hata kufinywa.

“Mzazi akiwa ‘bize’ anachagua bidhaa, mtoto anabaki akitazama huku na kule. Wakati mwingine wazazi husahau kama walikuwa na watoto, wanaondoka na kuwaacha kwenye maduka,” anasema Shaka akieleza aliyoyashuhudia.

Hamisi Ally, dereva wa bajaji, anasema wiki hii imekuwa na watu wengi wanaoingia na kutoka Kariakoo.

“Wateja wamekuwa wengi, sehemu ya kupita ni ndogo na wafanyabiashara wamesogea hadi barabarani, hivyo hali ya usalama kwa watembea kwa miguu, hususan watoto, ni ndogo. Ajali inaweza kutokea muda wowote,” anasema.

Ni mtazamo wa baadhi ya wazazi kuwa, wanakwenda na watoto Kariakoo ili wachague wanachohitaji na kuwa na uhakika wa vipimo vyao, kukwepa uwezekano wa kurudi kubadilisha bidhaa pale itakapokuwa haimwenei au imebana.

“Sipendi kuja na mtoto, lakini kinachonitesa ni kutojua kipimo sahihi cha watoto wangu, hivyo nawabeba wote na nafika mapema kuepuka msongamano na shida ya usafiri,” anasema Neema Yohana.

Sebastian Katembo anasema amewabeba watoto ili kuwapatia mahitaji ya shule, lakini kubwa zaidi ni kuwapa nafasi ya kuchagua wanachotaka.

“Nimekuja kununua vifaa vya shule, vikiwamo madaftari na mabegi. Nahitaji kila mtoto achague na abebe mzigo wake mwenyewe,” anasema.

Tofauti na hao, Sikuzani Masoud anasema amembeba mwanaye kwa sababu ya kukosa mtu wa kumwachia.

“Sipendi kutembea na mtoto kila ninapokwenda, lakini nimekosa mtu wa kukaa naye,” anasema.

Wasindikizaji wasionunua bidhaa wanatajwa kuchangia uwepo wa msongamano, ikielezwa kuwa watu huingia dukani kwa makundi, lakini mnunuzi huwa mmoja.

Inaelezwa baadhi ya wasindikizaji huingia dukani, wengine husimama mlangoni au kuzunguka kuangalia bidhaa bila kununua.

“Unakuta duka dogo lina watu 10, wakati wanaonunua ni wawili tu. Wengine wamesimama wanazungumza au wanapiga simu,” anasema Salum Msemo, mfanyabiashara wa nguo.

Wasindikizaji hao wanaelezwa kuchelewesha huduma kwa wateja wengine kwani wakati mwingine huuliza maswali mengi, huku wakisitasita kununua bidhaa yoyote.

“Tunawaomba wanunuzi kupunguza idadi ya wasindikizaji au wakae nje ya maduka ili kupunguza msongamano, kurahisisha huduma na kuwezesha biashara kuendelea kwa utulivu,” anasema Msemo.

Ndani ya kundi la wasindikizaji, inaelezwa wapo wanaokwenda kama kikundi kununua zawadi, hivyo huchukua muda mrefu kujadiliana kabla ya kuafikiana bidhaa ya kununua. Kundi hilo likiwa dukani hujadili kuhusu rangi, ubora na bei.

Kwa mujibu wa wafanyabiashara, kundi hili hununua zaidi nguo za sare, mapazia, vifaa vya jikoni, vijora, vitambaa, viatu na vifaa vya mapambo ya ndani ya nyumba.

Mzazi akiwa anavuka barabara ya Msimbazi, Kariakoo na watoto wake wakielekea madukani kwa ajili ya kupata mahitaji mbalimbali kuelekea msimu wa Sikukuu ya Christmas na Mwaka mpya

“Wanawake wanakuja wengi kwa pamoja, wanataka kushauriana, kulinganisha bidhaa na bei. Kibiashara ni nzuri, lakini duka linajaa haraka,” anasema Asha Msuya, mfanyabiashara wa mapazia katika Mtaa wa Mchikichi na Sikukuu.

Rehema Kalinga, mnunuzi wa bidhaa, anasema huenda wengi ili kupata mawazo na kufanya uamuzi sahihi kuhusu wanachohitaji wakiwa kwenye kikundi.

“Ukija peke yako unaweza kukosea, lakini ukiwa na wenzako mnashauriana rangi, bei na matumizi. Ndiyo maana tunakuja pamoja,” anasema.