Latra: Nauli ya Sh1,000 za mwendokasi ni za mpito

Dar es Salaam. Wakati wananchi wakilalamika upandaji wa nauli ya usafiri wa mwendokasi kutoka Sh750 hadi Sh1,000, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) imeeleza nauli hiyo ni ya mpito na halisi zitatumika baada ya uwasilishaji wa maombi ya nauli mpya.

Mradi huo ambao unatekelezwa kwa awamu sita, mpaka sasa awamu ya mbili zimekamilika na kuanza kutoa huduma ikiwamo ya Kimara na Mbagala, huku awamu ya tatu inayohusisha barabara ya Nyerere tayari ujenzi wake umefikia asilimia 90.

Katika kipindi cha mwaka 2025, mara kadhaa wananchi walikuwa wakipaza sauti zao kutaka kupatikana kwa mshindani mwingine wa kutoa huduma ukiacha Kampuni ya Usafiri wa Mabasi Yaendayo Haraka (Udart).

Kwa mujibu wa kanuni za Latra za tozo za mwaka 2020, watoa huduma wanatakiwa kutoa matangazo ya nauli mpya kwa siku 14 kabla ya kuanza kutumia nauli mpya kupitia vyombo vya habari vinavyowafikia watu wengi.

Akizungumza Desemba 17, 2025 jijini Arusha, Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo amesema nauli ya Sh1,000 iliridhiwa kwa Tangazo la Serikali la Agosti 29,2025 ambayo ilikuwa inawapa uhakika wanaoleta mabasi kwa kuanza na nauli hiyo.

“Hii ilikuwa inawapa uhakika wanaoleta mabasi hadi pale Wakala wa Mabasi yaendayo Haraka (Dart) itakapoleta maombi rasmi ya mapendekezo ya nauli baada ya kukaa na watoa huduma wa usafiri huo,” amesema Suluo.

Amesema kwa sasa nauli hii ya mpito inamwezesha mtoa huduma kutoingia hasara wala kupata faida kubwa kwani ataipata kutokana na wingi wa abiria.

Pia, amesema lengo la kuweka nauli hiyo ni kuwavutia wawekezaji wengine kutoa huduma.

Hata hivyo, amesema mamlaka ilifanya ziara ya mradi wa BRT awamu ya pili kabla ya kutangazwa kwa nauli ya Sh1,000 na kulikuwa na changamoto kwenye uendeshaji zilitatuliwa na huduma za usafiri zikaanza kutolewa.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu Dart, Said Tunda amesema nauli ya Sh1,000 inafaa kwa kuanzia kwani lengo sio kuwaumiza watumia huduma bali ni kuhakikisha abiria wanapata huduma bora na endelevu.

Amesema wakati huduma za BRT hazipo, abiria walikuwa wanatozwa hadi Sh6,000 kwa safari moja walipotumia vyombo vidogo vya usafiri.

“Serikali inawajali wananchi wake ndio maana hata baada ya kuharibika miundombinu iliyosababisha changamoto ya usafiri, huduma zinaendelea katika vituo vingi vya mwendokasi kwa kulipia gharama ya Sh1,000 ongezeko la Sh250 kutoka nauli ya awali,” amesema Tunda.