Dar es Salaam. Kutokana na kuongezeka na kukua kwa soko katika sekta ya ardhi, nyumba na makazi, Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), kinatarajia kuongeza kozi nyingine 21 kuanzia mwaka 2026.
Hayo yamesemwa leo Alhamisi Desemba 18, 2025 na Mkuu wa chuo hicho, Othman Chande, kwenye mahafali ya 19 yaliyofanyika chuoni hapo jijini Dar es Salaam.
Chande ambaye pia ni Jaji Mkuu mstaafu amesema kwa kuongeza kozi hiyo, kutafanya kuwa na zaidi ya kozi 80 zinazotolewa chuoni hapo.
“Kadri miaka inavyoenda na kukua kwa miji na maendeleo ya sayansi na teknolojia, uhitaji wa wataalamu katika sekta hii ya ardhi, nyumba na makazi umekuwa ukiongezeka.
“Hivyo na sisi chuo inatupasa kuendana nayo kwa kuongeza kozi nyingi zaidi ili kukidhi mahitaji na kuisaidia Tanzania,” amesema Mkuu huyo wa chuo.
Akizungumzia kuhusu mahafali hayo, Jaji Chande amesema zaidi ya wanafunzi 1,571 wamehitimu kati yao wa shahada ya uzamivu ni 18, shahada ya uzamili ni 70 na shahada ya awali wakiwa zaidi ya 1,300.
Aidha amesema ni jambo kubwa kwa wanafunzi kuhitimu na ni furaha kwa wanafamilia wa chuo hicho, wazazi na walezi wao huku akieleza hana shaka watakuwa wakikimbiliwa na waajiri lakini wenyewe pia kujiajiri.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Evaristo Liwa, amesema wao wamefanya kila wanachostahili kwa wahitimu hao wakati wote walipokuwa chuoni hapo na kueleza ana imani wataenda kuwakilisha vema chuo huko waendako.
“Furaha ya chuo ni kuona mwanafunzi wetu wanatumika, wanaajirika au kujiajiri na pia kuwa na furaha huko anapokuwa,”amesema Profesa Liwa.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Chuo, Balozi Salome Sijaona, amesema chuo hicho kimeshiriki katika kutengeneza Dira ya 2050, hivyo wanajua nini nchi inataka jambo linalowafanya nao kuingia katika mageuzi makubwa ya utoaji elimu.
“Katika kulitekeleza hilo, tayari tumeanza kutanua majengo yetu lakini pia tuna mpango wa kuongeza idadi ya udahili wa wanafunzi hadi kufikia 14,000 kufika 2029 kutoka 7,000 waliopo sasa,” amesema Balozi Salome ambaye pia amewahi kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wahitimu, Bertha Abraham, aliyehitimu masuala ya habari na mifumo, amesema kuongezeka kwa uwekezaji wa mifumo ya mawasiliano ili iweze kusomana kiurahisi, kwani rasilimali watu wa kufanya hivyo wapo wengi waliotengenezwa na chuo hicho.