Msanii maarufu wa muziki wa Bongo Fleva mwenye ladha ya R&B na Afro-pop, Christian Bella, amepewa rasmi uraia wa Tanzania, hatua inayothibitisha mchango wake mkubwa katika sekta ya muziki na uhusiano wake wa muda mrefu na taifa hili.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Alhamisi, Desemba 18, 2025, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene, amesema Christian Bella ni miongoni mwa wahamiaji waliokidhi vigezo na taratibu zote za kisheria za kupewa uraia wa Tanzania.
Waziri Simbachawene ametoa kauli hiyo katika maadhimisho ya Siku ya Wahamiaji Duniani, akieleza kuwa Tanzania ina idadi kubwa ya wahamiaji kutoka mataifa mbalimbali, ambapo baadhi yao wamekuwa wakipewa uraia baada ya kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.
Amesisitiza kuwa utoaji wa uraia ni haki inayotolewa kwa watu wanaokidhi masharti, huku akionya kwamba uraia unaweza kufutwa endapo mhusika hatazingatia sheria na taratibu za nchi.
“Uraia ni haki yenye wajibu. Mtu anaweza kupewa uraia na pia anaweza kufutiwa endapo atakiuka sheria au kushindwa kuzingatia masharti ya nchi,” amesema Simbachawene.
Christian Bella, ambaye amekuwa akiishi na kufanya kazi nchini Tanzania kwa miaka mingi, amejizolea umaarufu mkubwa kupitia nyimbo zake za mapenzi na kushirikiana na wasanii mbalimbali wa Kitanzania, hali iliyomfanya kupendwa na mashabiki wengi wa muziki wa Bongo Fleva.
Hatua ya kumpa uraia msanii huyo imepokelewa kwa furaha na wadau wa sanaa na burudani, wakieleza kuwa ni uthibitisho wa namna Tanzania inavyothamini mchango wa wageni wanaoleta maendeleo katika sekta mbalimbali.
