Arusha. Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), imezindua kampeni maalumu ya utalii yenye vifurushi vya bei nafuu kwa msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka, ikilenga kuongeza idadi ya watalii na kufikia lengo la makusanyo ya Sh350 bilioni katika mwaka wa fedha 2025/2026.
Kampeni hiyo iliyopewa jina la ‘Merry and Wild: Ngorongoro Awaits’, inaongozwa na kauli mbiu isemayo; “Kama unampenda, Utamleta Ngorongoro.”
Lengo ni kuwahamasisha Watanzania na wageni kutoka nje ya nchi kutembelea mojawapo ya maeneo ya urithi wa dunia yanayotambulika kwa mandhari ya kipekee na wanyamapori adimu.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Idara ya Utalii na Masoko wa NCAA, Mariam Kobelo akizungumzia kampeni ya merry and wild : Ngorongoro awaits
Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika leo Alhamisi Desemba 18, 2025 katika Kreta ya Empakai, ndani ya eneo la hifadhi.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Idara ya Utalii na Masoko wa NCAA, Mariam Kobelo amesema hii ni awamu ya pili baada ya tathmini kuonyesha idadi ya watalii wa ndani bado ni ndogo ikilinganishwa na wageni.
“Kwa kushirikiana na kampuni ya Tanzania Smile Safari, tumeandaa vifurushi vyenye punguzo la bei hadi asilimia 50 ili kutoa fursa kwa Watanzania wengi zaidi kujionea utajiri wa urithi wa dunia uliopo ndani ya Ngorongoro,” amesema Kobelo.
NCAA imeweka lengo la kukusanya Sh350 bilioni kutokana na vyanzo vyake mbalimbali, ikiwemo utalii na utoaji wa huduma.
Hatua hiyo inakuja baada ya mafanikio ya mwaka wa fedha 2024/2025, mamlaka ilivuka lengo lake na kukusanya jumla ya Sh269.9 bilioni.
Kwa upande wake, Ofisa Masoko wa Tanzania Smile Safari, Emmanuel Pantaleo amesema kampeni hiyo imegawanywa katika vifurushi vitatu ambayo ni Faru, Tembo na Chui, vyote vikiundwa kukidhi mahitaji ya wasafiri kutoka maeneo tofauti.
Amefafanua kuwa kifurushi cha Faru kinagharimu Sh475,000 kwa mtu mmoja kwa wasafiri wanaoanzia Dar es Salaam, kikiwajumuisha safari ya siku mbili (Desemba 24–25, 2025) inayohusisha usafiri kutoka Mlimani City hadi ndani ya hifadhi, kiingilio, malazi, chakula, mwongoza watalii na huduma ya picha.
Naye Mkuu wa Idara ya Mipango, Uwekezaji na Ufuatiliaji wa NCAA, Gasper Lyimo amesema wageni watapata fursa ya kutembelea vivutio vikuu vikiwemo Kreta ya Ngorongoro, Kreta ya Empakai na Olmoti, pamoja na misitu ya nyanda za juu kaskazini ambayo ni makazi ya wanyamapori wengi kama simba, tembo, faru, nyati na chui.
Ameongeza kuwa mamlaka inaendelea kuboresha miundombinu ya barabara na kuratibu huduma muhimu ikiwemo usalama, ili kuhakikisha wageni wanafika vivutio vyote kwa urahisi na kufurahia mapumziko salama yenye kumbukumbu nzuri.
“Kipaumbele chetu ni kuhakikisha wageni wanapata uzoefu bora wa utalii, mazingira salama na huduma zenye viwango, sambamba na kukuza mchango wa sekta ya utalii katika uchumi wa Taifa,” amesema.