Morogoro. Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linafanya uchunguzi wa kina kubaini chanzo cha tukio la kuchomwa moto na kuharibiwa kwa magari mawili katika Wilaya ya Mvomero, tukio lililotokea Desemba 17, 2025.
Kwa mujibu wa taarifa ya Polisi, tukio hilo lilitokea katika kitongoji cha Kilingeni, kijiji cha Lusanga, kata ya Diongoa, Tarafa ya Turiani, ambapo gari aina ya Mazda CX-5 pamoja na gari aina ya Toyota Noah yalichomwa moto na kusababisha hatari kwa maisha ya watu waliokuwapo eneo hilo.
Inaelezwa kuwa magari hayo yalikuwa yakisafirisha mwili wa marehemu Mwanahasa Juma Hamis (18), mfanyakazi wa kazi za ndani na mkazi wa Turiani, aliyefariki dunia na alikuwa akisafirishwa kwenda mkoani Morogoro kwa ajili ya shughuli za mazishi.
Taarifa zinaeleza kuwa wakati taratibu za mazishi zikiendelea, kulitokea taharuki miongoni mwa wananchi kutokana na mashaka kuhusu mazingira ya kifo cha marehemu. Hali hiyo ilisababisha vurugu zilizochochea uchomaji wa magari hayo, pamoja na kuzuia kwa muda wasindikizaji wa msiba kutoa maelezo zaidi.
Jeshi la Polisi, kwa kushirikiana na viongozi wa serikali ya mtaa, waliingilia kati na kufanikisha kuwaokoa wasindikizaji wa msiba waliokuwa hatarini, huku hali ya usalama ikirejeshwa.
Polisi wamesema wanaendelea na uchunguzi wa kina kubaini ukweli wa tukio hilo, wakiwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake kutoa taarifa sahihi kwa vyombo vya dola. Taarifa kamili kuhusu matokeo ya uchunguzi huo itatolewa baadaye.